Jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza, wengi tumekuwa tukiichukulia dawa ya aspirini kama dawa ya hadhi ya chini, hatufahamu kuwa ina uwezo mkubwa wa kitiba mwilini ikiwamo kuzuia magonjwa ya moyo na kiharusi.
Mamilioni ya watu duniani humeza vidonge hivyo kupunguza hatari ya kufa kwa magonjwa ya moyo na kiharusi baada ya kupewa ushauri na wataalamu wa afya.
Tafiti mpya zinaleta tumaini jipya kwa wagonjwa wa saratani, matokeo chanya ya tafiti mbalimbali duniani yanaleta ushahidi mpya ya uwezekano wa dawa hii kuzuia na kutibu saratani mbalimbali.
Kwa mujibu wa taasisi za dawa za ndani na nje ya nchi, dawa hii ambayo ni moja ya dawa zisizo na gharama ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Taarifa za kitabibu na kifamasia zinaonyesha kuwa faida ya kutumia dawa hii ni kubwa kuliko madhara machache yanayojitokeza, ndiyo maana haikuwahi kuzuiwa kwa matumizi ya binadamu.
Miaka ya nyuma dawa hii ilikuwa mwokozi wa kila siku kwa watu wengi, hasa waliopatwa na maumivu ya mwili na homa.
Baadaye matumizi yake yalipunguzwa kutokana na kuingia kwa dawa nyingine za maumivu za kisasa kama Paracetamol, Diclofenac na Ibobrufen.
Mara nyingi, katika vituo vya afya watu huichukulia dawa hii kuwa na hadhi ya chini na wapo wanaofikia hatua ya kulalamika wanaposhauriwa kutumia.
Undani wa Aspirin
Kitabibu, Aspirini ni dawa inayoangukia katika kundi la dawa zijulikanazo kwa jina la Non steroidal Anti inflammatory drugs (NSAIDs). Matumizi makuu ya dawa hizi ni kuondoa maumivu, uvimbe na homa.
Tofauti na baadhi ya watu wanavyodhani kuwa dawa hii inaondoa na kutibu kabisa chanzo cha kuumwa kama vile kichwa pasipo kufahamu, hiki ni kitulizo.
Lazima chanzo cha kuumwa kichwa au homa kifanyiwe uchunguzi wa kina na kutibiwa.
Dawa hii inafanya kazi ya kwenda kuzuia mojawapo ya kemikali zinazozalishwa baada tishu za mwili kupata uchokozi na kutokea mlipuko wa kinga ya mwili ili kujihami na uchokozi.
Utolewaji wa kemikali hizo za kinga ya mwili ndiyo unaotupa hisia za maumivu, uvimbe na homa.
Taarifa ya kitafiti iliyotoka karibuni inaeleza kuwa Aspirini inahusishwa katika uwezo wa kuzuia na kutibu saratani.
Tarifa ya matokeo ya kitafiti yalitolewa jijini Vienna Austria mwishoni mwaka jana, watafiti kutoka Uholanzi katika kongamano la saratani la nchi za Ulaya, walieleza kuwa dawa hii ina uwezo wa kuongeza mara mbili muda wa kuishi kwa wagonjwa wa saratani za bomba la chakula, mfuko wa chakula na utumbo mpana.
Kati ya wagonjwa 14,000 wa saratani waliofanyiwa utafiti kwa kutumia dawa hii, waliongeza mara mbili muda wao wa kuishi baada ya miaka minne wakilinganishwa na wale ambao hawakuitumia.
Dk Martine Frouws ambaye ni mmoja wa waliofanya utafiti huo kutoka Chuo Kikuu cha Leiden cha nchini Uholanzi, alieleza changamoto waliyoipata katika utafiti huo kuwa ni pamoja na kushindwa kuwagundua wale ambao hawakunufaika na dawa hiyo.
Pamoja na changamoto hizo, ushahidi wao wa kitafiti umeishajijenga vema. Utafiti huo unabainisha kuwa utumiaji wa kiasi kidogo cha dawa ya Aspirini (75mg) kila siku kwa miaka mitano kwa watu wenye umri wa kati, kunapunguza hatari ya kupata saratani za mfumo wa chakula kwa asilimia 20. Vilevile inazuia kupata saratani ya matiti, mapafu na tezi dume.
Utafiti ulihusisha wagonjwa 25,000 waliotumia dozi ndogo ya Aspirini kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya moyo, ikagundulika kuwa dawa hii inapunguza vifo vitokanavyo na saratani kwa zaidi ya asilimia 21.
Dawa hii iliyogunduliwa miaka 100 iliyopita, na fomula yake kununuliwa na kampuni ya Kijerumani, ina wigo mpana wa kitiba kwani pia ndiyo inayotumiwa kila siku na wagonjwa wa kiharusi na magonjwa ya moyo.
Utafiti mwingine
Huu si utafiti wa kwanza kufanyika kuhusu dawa ya Aspirini, zipo tafiti nyingine zilizowahi kufanyika hapo nyuma ukiwamo ule uliochapishwa katika jarida la Lancet mwaka 2011.
Katika utafiti huo uliohusisha makundi matano, uliwasaidia wagonjwa wa saratani wanaotumia dawa hii kila siku kwa kuzuia kusambaa maeneo mengine kama kwenye ubongo, ini na mapafu.
Kwa kawaida hizi ni hatua za mwisho za saratani kwa asilimia 30 hadi 40.
Tayari Marekani, kikosi kazi cha huduma za kinga kinafanyia kazi mapendekezo ya matumizi ya Aspirini kuzuia na kujikinga na saratani.
Siyo Marekani pekee, Uingereza pia kupitia taasisi ya afya na tiba (Nice) wameamua nao kupitia na kuchambua taarifa za kitafiti zinazohusu dawa hii.
Habari njema kwa Tanzania
Dk Harith Mapande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, anasema amepitia matokeo mbalimbali ya tafiti kuhusu Aspirini na anaamini yanaleta matumaini mapya.
‘’Kuna matokeo chanya hasa kwa wagonjwa wa saratani ya mfumo wa chakula waliotumia dawa ya aspirini, lakini kwa upande mwingine dawa ya Aspirini inatakiwa itumike kwa dozi ndogo pia wasitumie wagonjwa wenye hatari ya kupata vidonda vya tumbo au ambao t wana vidonda vya tumbo,’’ anasema.
Dk Salehe Khalidi Kijangwa wa hospitali ya Magunga ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, anasema bado kunahitajika tafiti nyingi hasa za ndani ya nchi ili zilinganishwe na tafiti za nje.
Anaonya kuwa matokeo haya ya tafiti za nje yasiwe sababu ya watu kutumia dawa hii kiholela pasipo ushauri wa daktari, kwa kuwa ikitumiwa katika kiwango kikubwa au kutumiwa kila siku, inaweza kusababisha madhara kama kukwangua utumbo na kusababisha vidonda.
“ Wananchi wasiwe na hofu na madhara machache, kwani faida yake kuitumia katika matibabu mbalimbali ni kubwa.
Pia dawa hii ni salama na inapatikana kwa bei ndogo,’’ anasema.