BINADAMU wote wanahitaji chakula lakini walio wengi wanakula zaidi kwa
mazoea bila ya kujali wanachokula na wanapata nini katika chakula
wanachokula.
Mazingira tunayoishi na tunayofanyia kazi mara nyingi yanatufanya kuishi
na kula kimazoea sana pasina kujali athari na matokeo ya ulaji wetu.
Ni muhimu kwa kila mtu kuzingatia ulaji unaofaa kwa kuhakikisha anakula mlo kamili kwa angalau milo mitatu kwa siku.
Mlo kamili ni ule unaotakana na mchanganyiko sahihi kwa angalau aina moja ya chakula kutoka katika kila kundi la chakula.
Yapo makundi matano ya chakula, la kwanza likiwa ni vyakula
vinavyotokana na nafaka, mizizi na ndizi. Kundi hili huchukua sehemu
kubwa ya mlo na kwa kawaida ndilo linalobeba vyakula vikuu kama chanzo
kikuu cha wanga.
Kundi hili lina vyakula kama mahindi, ulezi, mchele, ngano, mtama,
uwele, viazi, mihogo, magimbi na ndizi. Vyakula vinavyotokana na kundi
hili huupatia mwili nishati inayohitajika kwa viungo mbalimbali na
michakato mbalimbali mwilini. Pia vyakula hivi huzalisha joto
linalohitajika mwilini.
Kundi la pili ni vyakula vinavyotokana na jamii ya kunde na vyakula vyenye asili ya wanyama.
Kundi hili linahusisha vyakula kama maharage, kunde, njegere, fiwi,
soya, karanga, dengu, choroko, nyama, samaki, dagaa, mayai, maziwa na
wadudu wanaoliwa kama senene na kumbikumbi.
Kundi hili linaupatia mwili protini kwa wingi na pia nishati, vitamini
na madini. Protini ni muhimu kwa kujenga mwili, kutengeneza vimeng’enywa
na kujenga upya sehemu za mwili zilizoharibika.
Kwa kundi hili la tatu, vyakula husika ni vya mbogamboga. Kundi hili
linajumuisha aina zote za mboga za majani pamoja na mboga nyingine kama
bamia, karoti, matango, nyanya chungu, pilipilihoho na maboga.
Mbogamboga zinaupa mwili vitamini na madini kwa wingi. Vitamini na
madini ni muhimu mwilini kwani huboresha afya na kuimarisha kinga ya
mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.
Matunda ni kundi la nne ambalo hujumuisha aina zote za matunda na hata
yale matunda pori kama embe ng’ongo, mabungo, ukwaju nakadhalika.
Moja ya kazi kubwa ya matunda ni kuupatia mwili vitamini ambazo husaidia
kukinga mwili zaidi ya magonjwa na ufonzwaji wa virutubisho vingine.
Mafuta na sukari ni kundi la tano la vyakula. Kundi hili la mafuta na
sukari hutupa joto na nguvu mwilini. Kundi hili hujumuisha mafuta
yanayotokana na mimea kama nazi, mawese, ufuta, alizeti, pamba.
Sukari ni pamoja na asali, miwa na sukari yenyewe. Kundi hili pia
hutumika kama viungo, huongeza ladha ya chakula na husaidia uyeyushwaji
na ufonzwaji wa baadhi ya vitamini.
Kula mlo kamili kwa kuzingatia makundi ya vyakula hapo juu huuwezesha
mwili kupata virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika kwani hakuna aina
moja ya chakula inayoweza kukupa virutubisho vyote isipokuwa maziwa ya
mama pekee, na hii inawezekana kwa mtoto tu hasa chini ya miezi sita.
Ulaji wa chakula mchanganyiko huuwezesha mwili kutumia virutubisho
mbalimbali kwa ufanisi kwani mara nyingine virutubisho hutegemeana
katika uyeyushwaji na ufyonzwaji wake.
Kwa mfano vitamini C husaidia ufyonzwaji wa madini ya chuma
yanayopatikana katika vyakula venye asili ya mimea. Na mafuta husaidia
ufyonzwaji wa vitamini A, D, E na K.
Katika kutengeneza mlo kamili kutokana na makundi mbalimbali ya vyakula
ni vizuri pia kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira
tunayoishi na kubadili vyakula kila inapowezekana.
Vyakula vya msimu kama mbogamboga na matunda vitumike ipasavo kwenye
msimu wake kwani upatikanaji wake unakua rahisi na kwa gharama nafuu.
Kiasi cha chakula katika kutengeneza mlo kamili kutoka kila kundi
kitategemea na kiasi cha nishati unachopaswa kupata kila siku. Kiasi
hicho cha nishati hutegemea umri, jinsia, mazoezi au kazi ya mtu
anayoshughulika nayo.
Katika kukamilisha mlo kamili ni vizuri kunywa maji yaliyo safi na
salama kwani husaidia mwili kufanya kazi zake kwa ufanisi. Kitaalamu
inashauriwa kunywa maji angalau lita moja na nusu au angalau glasi nane
kwa siku.
Makala ijayo itajadili madhara yatokanayo na ukosefu wa chakula bora