Wanaume hufanya kazi zaidi na kutembea umbali mrefu zaidi ukilinganisha na wanawake, hivyo hutumia nguvu nyingi kufanya mambo haya, hali inayomletea uchovu mkali wa mwili. 
Yawezekana kuwa tuna majukumu mengi na tunafanya kazi sana ili kujipatia kipato, lakini katika kufanya kazi huko huwa tunafanya kazi nzito ambazo zinauchosha mwili kupita kiasi.
Kwa uhalisia wanaume wanafanya kazi ngumu zinazochosha mwili ikiwamo za kuendesha magari makubwa na kusafiri nayo umbali mrefu, kazi za ujenzi, kubeba mizigo mizito kama ilivyo kwa makuli wa bandarini na sokoni.

Kazi zingine ni pamoja na za kutumia akili zaidi ikiwamo ya uhandisi wa mawasiliano na kazi za usanifu majengo.

Wanaume hufanya kazi zaidi na kutembea umbali mrefu zaidi ukilinganisha na wanawake, hivyo hutumia nguvu nyingi kufanya mambo haya, hali inayomletea uchovu mkali wa mwili.

Uchovu na mashinikizo ya kimwili ni mojawapo ya mambo yanayochangia wanaume wengi kupungukiwa na nguvu za kiume. Unapokuwa katika hali hii ni vigumu kupata msisimko wa kimwili inayochochea kufanya tendo la ndoa.

Kutumika sana kwa viungo vya mwili, ikiwamo ubongo, misuli ya mwili, baadaye humfanya muhusika kubaki na uchovu mkali mwilini. 
Utakumbuka hili ni jambo la tatu kulizungumzia katika mazingira ya kawaida kusababisha upungufu wa nguvu za kiume. Katika mfululizo wa makala hizi, siku za nyuma nilizungumzia vyakula pamoja na mazingira ya mtu kisaikolojia kama mojawapo ya mambo yanayoweza kuchangia tatizo hili. 

Uchovu au mwili kuchoka sana, huchangia mtiririko wa tendo la ndoa kuathirika na hata vichocheo vya mwili kupungua. 

Mwili unapochoka, unashindwa kuwa na nguvu za kiume za kutosha hivyo kushindwa kwenda mizunguko kadhaa ya tendo la ndoa. 

Kama tulivyoona katika makala za mwanzoni kuwa tendo hili linalohusisha mfumo wa fahamu, yaani ubongo, uti wa mgongo, mishipa ya fahamu, mfumo wa damu, moyo na misuli ya mwili. 

Misuli hiyo ikiwamo ile ya uume, homoni za mwilini pamoja na kemikali zilizomo katika damu na sehemu za mwilini, navyo vinahusika. 

Uchovu mkali uliotokana na kufanya kazi ngumu bila kupata usingizi au mapumziko, huwa na mwingiliano na mtiririko mzima wa tendo hili kiujumla. 

Kuupumzisha mwili kwa kulala usingizi kuna faida kubwa sana kiafya. 

Kitaalamu kulala kunawezesha mwili ulio na uchovu kuweza kurejewa na nguvu upya. Kulala peke yake, kunaupa nafasi mwili kupata utulivu, kuukarabati na kuujenga mwili. Vilevile hii ni namna ya kupambana na maradhi na hitilafu mbalimbali zilizojitokeza mwilini. 

Tafiti mbalimbali za kiafya zimeonyesha kuwa kulala kwa zaidi ya saa sita kuna faida kubwa kiafya kwani husababisha kiwango cha homoni ya kiume iitwayo Testosterone mwilini huongezeka. 

Kupanda kwa homoni hii ni faida kubwa kwa mwenye upungufu wa nguvu za kiume na hata asiye na tatizo. Hivyo hili ni jambo muhimu kwa kila mtu. 

Homoni hii ndiyo inayosababisha tabia zetu za kiume, ikiwamo ya kuweza kupata hisia za tendo la ndoa na kufanya kuwa imara. 

Kitaalamu mwanadamu anatakiwa kupumzika kwa kati ya saa sita hadi nane. Muda huo ndiyo unaoonekana kisayansi unatosheleza mwanadamu kupumzisha mwili wake na kuepukana na uchovu. 

Ni vyema wale wenye tatizo la upungufu wa nguvu za kiume kujijengea mazoea ya kulala kwa saa nyingi ikiwa ni mojawapo ya mbinu rahisi za matibabu kabla ya kumfikia daktari. 
 
Top