lishe ya mtotoNangeriya Nangoro wa Kijiji cha Laalakir, Kiteto, akimnywesha maziwa mtoto wake kwa kutumia kibuyu maalum. (Picha kwa hisani ya tosamawe.blogspot.com.

WAZAZI wengi wanatamani kuwa na watoto wenye afya nzuri kimwili na akili. Ili mtoto aweze kukua vizuri kiafya ana mahitaji mbalimbali kutia ndani lishe na mapumziko ya kutosha.

Mahitaji ya Mtoto Kilishe Yakoje?

Umri hadi Miezi 6

Nyonyesha mtoto wako mara nyingi kadri mtoto anavyotaka mchana na usiku si chini ya mara 10 kwa saa 24. Usimpe chakula au vinywaji vingine.


Miezi 6 hadi Miezi 9

Mwanzishe vyakula vya nyongeza huku ukiendelea kumnyonyesha mara nyingi kadri mtoto anavyotaka. Mpatie uji mzito na vyakula vilivyopondwapondwa. Kwa kuanzia mpe vijiko vya chakula 2 hadi 3 mara 2 kwa siku. Kuanzia miezi 7 ongeza kiasi kidogo kidogo hadi 2/3 ya kikombe chenye mililita 250 kwa kila mlo, mara 3 kwa siku.

Mfano wa vyakula hivyo ni viazi, ndizi, uji wa mchele, mboga za majani, samaki, nyama iliyosagwa, maharage, karanga na jamii nyingine ya kunde. Matunda kama papai, ndizi na maparachichi. Ongeza kijiko cha mafuta kila mlo. Tumia chumvi yenye madini joto ikiwa mtoto hanyonyi mpe kikombe 1-2 vya maziwa kwa siku na milo 2 zaidi kwa siku.

Miezi 9 hadi Miezi 12

Mnyonyeshe mara nyingi mtoto kadri anavyotaka. Mpe chakula laini kilichopondwapondwa ambacho anaweza kumeza. Mpe robo tatu kikombe cha mililita 250 mara 3 kwa siku. Mpe milo 3 kwa siku na mara moja vitafunwa (snacks) kati ya mlo na mlo.

Mfano wa vyakula hivyo ni viazi, ndizi, uji wa mchele, mboga za majani, samaki, nyama iliyosagwa, maharage, karanga na jamii nyingine ya kunde. Matunda kama papai, ndizi na maparachichi. Ongeza kijiko cha mafuta kila mlo. Tumia chumvi yenye madini joto ikiwa mtoto hanyonyi mpe kikombe 1-2 vya maziwa kwa siku na milo 2 zaidi kwa siku.

Mwaka 1 hadi Miaka 2

Mnyonyeshe mara nyingi mtoto kadri anavyotaka. Mpe vyakula vya familia vilivyokatwa katwa vipande vidogo vidogo au kupondwapondwa. Mpe kikombe cha mililita 250 kwa kila mlo. Mpe milo 3 na vitafunwa mara 1 kati ya mlo na mlo.

Miaka 2 hadi Miaka 5

Mpe milo mitatu ya familia kwa siku, vitafunwa (snacks) mara 1 kati ya mlo na mlo. Mfano maziwa, juice na vitafunwa.

Nini Mapendekezo ya Lishe kwa Mtoto mwenye Kuharisha Sugu?

Kama bado ananyonya, nyonyesha mara nyingi, kwa muda mrefu zaidi, usiku na mchana. Kama anakunywa maziwa ya aina nyingine aache na aendelee kunyonyesha zaidi au mpatie mtindi au vyakula vitokanavyo na mtindi au mchanganyie nusu ya maziwa anayotakiwa kunywa na vyakula laini vyenye virutubisho.

Kwa vyakula vingine, fuata mapendekezo ya lishe kwa umri wa mtoto. Mpatie mlo wa ziada mmoja na aendelee kwa mwezi mmoja baada ya kuacha kuharisha. Mpatie Multivitamin.

Desturi Nzuri za Afya na Utayarishaji wa Chakula katika Hali ya Usafi Zikoje?

Nawa mikono kabla ya kuandaa chakula, kabla na baada ya kula. Chakula kiliwe mara baada ya kuandaliwa. Tumia vyombo vilivyo safi kuandaa chakula. Hakikisha matunda yanaoshwa vizuri.

Mahitaji ya Usingizi kwa Mtoto Yakoje?

Wataalamu mbalimbali wa masuala ya usingizi kupitia mamia ya tafiti wamegundua muda mahsusi wa kulala kwa watoto wa umri tofauti ili kuwa na afya njema. Siyo siri kuwa watu wazima hawapati usingizi wa kutosha, na tatizo hili linaweza sababisha matatizo makubwa ya kiafya kama kuongezeka uzito kupita kiasi na magonjwa ya moyo. Hali hii ni sawa kwa watoto pia.

Hata hivyo watoto wanaweza kusinzia haraka wakienda kulala kuliko watu wazima, ingawa maendeleo ya kiteknolojia mfano uwepo wa simu za viganjani (smartphones) na mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram & Twitter imefanya watoto pia kushindwa kulala mapema wakati wa usiku.

Ili kuwasaidia wazazi kutambua ni usingizi kiasi gani unafaa kwa watoto wao, wataalamu 13 wa masuala ya usingizi walikutana Chuo cha Amerika cha Tiba ya Usingizi (American Academy of Sleep Medicine) na kutoa mapendekezo ya muda wa kulala kwa watoto yaliyoidhinishwa na kuungwa mkono na makundi mbalimbali ya kitaaluma kutia ndani Chuo cha Amerika cha Madaktari Bingwa wa Watoto (American Academy of Pediatrics).

Kwa kutegemea tafiti 864 zilizochunguza mwenendo wa usingizi kwa watoto na matokeo yake kiafya, waligundua watoto wanaolala chini ya muda uliopendekezwa wako katika hatari ya kuwa na matatizo ya kujifunza na kitabia, kuwa na uzito kupita kiasi, magonjwa ya moyo na huzuni.

Lakini pia, waligundua kulala kupita kiasi huongeza uwezekano wa magonjwa ya Kisukari na akili na kuongezeka uzito kupita kiasi.

Mapendekezo ya kulala kwa watoto wa umri tofauti ni kama ifuatavyo:-

Watoto wa miezi 4 hadi 12 wanapaswa kulala hadi masaa 16. Watoto wa mwaka 1 hadi miaka 2 wanapaswa kulala kati ya masaa 11 hadi 14. Watoto wa mika 3 hadi miaka 5 wanapaswa kulala masaa 10 hadi 13. Watoto wa miaka 6 hadi miaka 12 wanapaswa kulala masaa 9 hadi 12. Na kwa vijana ni masaa 8 hadi 10.
 
Top