Wakati  leo dunia inaadhimisha Siku ya Kisukari, katika miaka ya karibuni, ugonjwa huo umekuwa tishio kwa mataifa mengi duniani Tanzania ikiwamo.  Aidha, kwa sasa umeelezwa kuwa unashika nafasi ya tatu duniani kwa kusababisha vifo, huku watu milioni moja kila mwa hukatwa miguu kutokana na usugu wa ugonjwa huu.
Katika makala hii, mtaalam wa maradhi ya kisukari, Dk. Mary Magiye, kutoka Kituo cha Kisukari cha St. Laurent cha jijini Dar es Salaam, anaeleza kwa ufasaha pamoja na mambo mengine, dalili za ugonjwa huu, kinga na tiba yake.

Katika makala hii, mtaalam wa maradhi ya kisukari, Dk. Mary Magiye, kutoka Kituo cha Kisukari cha St. Laurent cha jijini Dar es Salaam, anaeleza kwa ufasaha pamoja na mambo mengine, dalili za ugonjwa huu, kinga na tiba yake.
Kisukari ni nini?

Dk. Magiye anafafanua kuwa, kisukari kwa kifupi na kwa lugha ya kueleweka ni ugonjwa unaotokana na kuwa na kiasi kikubwa cha sukari kwenye damu.

Anasema sukari inapokuwa nyingi kwenye damu ya binadamu, hapo ndipo mtu huyo husumbuliwa na maradhi hayo.
Ugonjwa wa sukari unasababishwa na nini?

Kwa mujibu wa Dk. Magiye, baadhi ya sababu zinazosababisha ugonjwa huo ni uzito kupita kiasi, kutokuwa na mpangilio mzuri wa chakula, kutofanya mazoezi na kula kupita kiasi.

"Wengi hatujui ugonjwa huu huletwa na nini ama chanzo chake au dalili zake, tiba na matibabu pia bila madhara yake kiuchumi na kijamii na aina ngapi za kisukari," anasisitiza Dk. Magiye.

Nini kinachoshangia sukari kuzidi kiwango katika damu? 
Dk. Magiye anaeleza kwamba, kila chakula na hasa cha wanga, hutengeza sukari na moja ya kazi ya wanga, ni kuupa mwili nguvu.

"Sasa basi, chakula tunachokula kabla ya kufanya kazi yake, ni lazima kiyeyushwe au kimeng’enywe ili kupata sukari ambayo hutumika na chembe hai za mwili na kuupa mwili nguvu," anafafanua.

Dk. Magiye ansema baada ya chakula kuyeyushwa au kumeng'enywa, hufyonzwa mpaka kwenye mishipa ya damu kwa ajili ya kusafirishwa sehemu mbalimbali za mwili, sukari ikiongezeka kwenye damu, mwili hupeleka taarifa kwenye kongosho (pancreas) kutengeneza kichocheo kiitwacho insulin.

"Kazi ya insulin ni kusaidia sukari kuingia katika seli ili iweze kutumika. Endapo  kiungo hiki kiitwacho kongosho kitatengeneza kiasi kidogo sana cha insulin au kikashindwa kabisa kutengeneza kichocheo hicho, basi sukari ile itashindwa kutumika ipasavyo kwa sababu itashindwa kuingia kwenye seli na husababisha sukari kubaki kwenye mishipa ya damu," anafafanua Dk. Magiye.

Inapofikia hali hiyo, anasema Dk. Magiye, hapo ndipo mtu anapougua maradhi ya kisukari.

Kwa mujibu wa Dk. Magiye, kiwango sahihi cha sukari kwenye damu ni kuanzia 4 mpaka 7mmol/L, na inapozidi hapo, basi mtu huyo anakuwa na kisukari.

Wakati mwingine, kwa mujibu wa mtaalam huyo,  kongosho inaweza kuwa inatengeneza insulin ya kutosha, lakini sukari haiwezi kuingia kwenye chembe hai.Anafafanua kuwa hali hiyo husababishwa na mafuta mengi yanayozunguka chembe hai.

Dk. Magiye anaeleza kuwa inapofikia hivyo,  husababisha hali inayojulikana kitaalam kama ‘insulin resistance’.

"Hii ndiyo sababu kuu inayosababisha watu wenye uzito mkubwa kupata kisukari," anafafanua Dk. Magiye.
Aina kuu tatu za kisukari.

Dk. Magiye anaeleza, aina ya kwanza ya kisukari kwa kitaalam hujulikana kama `diabetes type 1'.

Anasema aina hii ya kisukari humpata mtu yeyote katika umri wowote wakiwamo watoto.

Hali kadhalika, anasema aina hii ya kisukari, mara nyingi waathirika wengi huwa wamerithi katika ukoo au huzaliwa nayo. Anaeleza kuwa tiba au matibabu ya aina hii ya kisukari ni sindano za insulin.

"Mgonjwa atatakiwa kutumia sindano ya insulin kutegemea na maelekezo ya daktari," anafafanua Dk. Magiye.

Aina ya pili ya kisukari ambayo kitaalam kujulikana kama `diabetes type 2' mara nyingi huwapata watu wazima kuanzia umri wa kati na kuendelea, anasema Dk. Magiye. Anafafanua kuwa mara nyingi sababu za aina hii ya kisukari ni umri mkubwa au uzee.

Vile vile anasema husababishwa na aina ya vyakula ambapo katika hali hiyo, kongosho hutengeneza kiwango cha kawaida cha insulin lakini haifanyi kazi kutokana na chembe hai kuzungukwa na mafuta kama ilivyoelezwa hapo awali.

"Matokeo yake kongosho huongeza kutengeneza insulin bila mpangilio mpaka inafika mahali inachoka na kufeli kabisa. Aina hii ya kisukari inaweza kudhibitiwa kabisa iwapo mgonjwa atagundulika mapema kabla kongosho haijafikia hatua ya kufeli na kufuata masharti," anasema Dk. Magiye.

Anayataja baadhi ya masharti hayo kuwa ni pamoja na kurekebisha mpangilio wa chakula na kuacha au kupunguza kula vyakula vyenye sukari na mafuta, kufanya mazoezi na pia kutumia vidonge.

Aina ya tatu ya kisukari kwa mujibu wa Dk. Magiye, ni ile inayowapata wajawazito ambayo kitaalam hujulikana kama `gestational diabetes.
Anafafanua kuwa, hali hiyo husababishwa na mahitaji ya insulin kuongezeka kipindi cha ujauzito.

Hata hivyo, anaeleza kuwa hali hiyo huisha baada ya mjamzito kujifungua.

"Lakini tafiti zinaonyesha kuwa wanawake huwa katika hatari kubwa ya kupata kisukari kadiri umri unavyozidi kuongezeka. Tafiti pia zimeonyesha kuwa aina hii ya tatu ya kisukari inatokana na mama kuwa na unene kupita kiasi," anasema.

Nini husababisha kongosho kutofanya kazi?
Dk. Magiye anaeleza kuwa zipo sababu za kitaalam na  za kijamii.

"Ninaposema sababu za kijamii ninamaanisha kuwa ni zile zinazosababishwa na sisi wenyewe," anasisitiza.

Kwa mujibu wa Dk. Magiye, sababu za kitaalam kongosho inaweza kupata hitilafu kutokana na maambukizi kwa mfano, maambukizi yanayomfanya mtu apate upungufu wa kinga mwilini, kemikali, ulevi au utumiaji wa pombe kupita kiasi na madhara (side effects) ya dawa fulani.

"Sababu zote hizi zinaweza kusababisha kongosho isifanye kazi yake," anasisitiza Dk. Magiye.

Sababu za kijamii, Dk. Magiye anaeleza kuwa ni zile zinazohusisha suala zima la mfumo wa maisha jamii inavyoishi hususan katika suala la lishe.

"Unene uliopitiliza ambao unasababisha kongosho kuzalisha insulin zaidi ya kiwango au zaidi ya uwezo wake wa kuzalisha au kutengeneza insulin, hali hii husababisha kongosho kuchoka na kushindwa kufanya kazi," anazidi kufafanua Dk. Magiye.

Utajuaje kama una ugonjwa wa kisukari?
Dk. Magiye anaeleza: "Watu wengi hatujui dalili za kisukari. Ni vigumu sasa kujua dalili za kisukari au kugundua kama una kisukari mpaka ukapime kwa kuwa si mara zote dalili za kisukari zinaweza kuonekana."

Anasema mtu mwenye kisukari anaweza kuwa na ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka 10 bila dalili zozote.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Dk. Magiye, baadhi ya dalili za kisukari ni kuhisi kiu kali na isiyoisha, njaa kali, kwenda haja ndogo mara kwa mara hasa wakati wa usiku, kupungua uzito kwa haraka, mwili kuchoka na kukosa nguvu. "Kwa hiyo pindi uonapo dalili hizo, ni muhimu kwenda hospitali na kupima," anashauri Dk. Magiye.
Kisukari kina madhara gani?

Dk. Magiye anaeleza kuwa madhara ya kisukari yamegawanyika kimwili, kijamii na kiuchumi.
Anafafanua kuwa madhara ya kimwili ni pale mgonjwa anapoanza kupoteza viungo vyake vya mwili, sukari isipodhibitiwa ipasavyo inaweza kuharibu ufanisi wa figo, mgonjwa hulazimika kutolewa figo, sukari ikiwa juu mgonjwa akipata kidonda si rahisi kupona na kusababisha kukatwa kwa kiungo kama mguu au vidole vya mguu kwa sababu mara nyingi vidonda hivi huwa kwenye miguu.

Vile vile, anasema mgonjwa hupoteza uwezo wa kuona na kusikia, hupoteza nguvu za kiume na mara nyingi husababisha kifo.

Madhara ya kiuchumi, Dk. Magiye anaeleza kuwa gharama za matibabu ya kisukari hasa kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, ni kubwa.

"Hii huathiri watu au wagonjwa wa hali ya chini kiuchumi," anaeleza Dk. Magiye.

Ni jinsi  gani ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa?
Dk. Magiye anasema, kisukari kinaweza kudhibitiwa kwa kufuata masharti ipasavyo, kwa wagonjwa wa kisukari ni muhimu kuzingatia matumizi ya sindano ya insulin au vidonge kama daktari alivyoelekeza.

Pia anaeleza kuwa ni vyema kuzingatia mpangilio wa chakula, lazima kufanya mazoezi ya viungo kila siku na kupima kiwango cha sukari mara kwa mara.

Aidha, anasema kwa wasio na kisukari, wanaweza kudhibiti hali hiyo kwa kuhakikisha kuwa wanadhibiti uzito na vile vile, kubadilisha mpangilio wa maisha; kufanya mazoezi mara kwa mara, kuzingatia mpangilio bora wa chakula na kupunguza au kuacha kabisa unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara.

Kwa upande wake, Mshauri wa Afya ya familia, Dk. Ali Mzige, alisema ugonjwa wa malaria unaongoza na kufuatiwa na ugonjwa wa upungufu wa kinga mwilini yaani Ukimwi huku kisukari kikishika nafasi ya tatu.

Kwa ushauri zaidi piga no.0784 778788

SOURCE: NIPASHE

 
Top