ATHARI ZA MAGONJWA YA NGONO KWA MTOTO
ATHARI ZA MAGONJWA YA NGONO KWA MTOTO
Magonjwa ya ngono ni magonjwa ambayo hujitokeza katika viungo vya uzazi baada ya mtu (hususani watu waliopo katika umri wa kuweza kuzaa, miaka 15 – 49) kujamiiana bila kinga na mtu ambaye tayari ameambukizwa ugonjwa/magonjwa hayo.

Kuna aina mbalimbali za magonjwa ya ngono, miongoni mwa magonjwa hayo ni kama kisonono, trikomonas na kandida (dalili zake ni kutokwa na usaha au majimaji sehemu za siri, yaani ukeni au uumeni. Magonjwa ya kaswende, pangusa na malengelenge, (dalili zake ni kutokwa na vidonda sehemu za siri). Magonjwa yenye dalili za kutokwa na uvimbe, mitoki na malengelenge mfano ni ugonjwa wa pangusa.
Mpenzi msomaji, dalili za magonjwa ya ngono kwa upande wa wanawake ni kama ifuatavyo: Kuota sundosundo sehemu za siri, kuvimba mitoki, kutokwa na uchafu au majimaji yasiyo ya kawaida au yenye harufu mbaya, maumivu sehemu ya chini ya tumbo yanayoweza kuambatana na homa, kuwashwa sehemu za siri na maumivu wakati wa kukojoa. Kwa upande wa wanaume dalili ni pamoja na uume kutoa usaha au kuvimba korodani, kupata maumivu wakati wa kukojoa, vidonda sehemu za mdomoni vinavyotokana na kufanya ngono ya mdomoni (oral sex) na muwasho mkali sehemu za siri.
Miongoni mwa mambo yanayosababisha maambukizi ya magonjwa ya ngono ni pamoja na kujamiiana bila kondomu kwa njia ya ukeni, haja kubwa au mdomoni, kuzaliwa na maambukizi, kuongezewa damu yenye maambukizi, ulevi wa kupindukia unaomfanya mtu asifanye maamuzi sahihi ya kutumia kinga wakati wa kujamiiana, kurithi wajane au mira na desturi za mwanamke mwenye mali kuoa msichana mdogo na kumtafutia mwanaume wa kuzaa naye watoto (nyumba ntobu) na kujamiiana na watu wanaotumia madawa ya kulevya.
Athari za magonjwa ya ngono ni pamoja na kuharibika mimba mara kwa mara, mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi, ugumba, kuziba kwa mirija ya uzazi, madadiliko ya hedhi, kujifungua kabla ya mimba kutimiza muda wake, kansa ya uume, kupungua nguvu za kiume, utasa, kuziba njia ya mkojo, magonjwa ya akili na maambukizi katika kokwa za mbegu za uzazi. Kwa upande wa watoto magonjwa haya husababisha mtoto adumae, uambukizo wa macho, upofu, kuzaliwa na uzito pungufu pamoja na vichomi.
Mpenzi msomaji, ili kujiepusha na magonjwa ya ngono, ni vyema mtu ukachukua tahadhari hizi, kuepuka ngono katika umri mdogo, kutumia kondomu wakati wa kujamiiana, kujiepusha na vitendo vya ubakaji. Pia ni vizuri kama unatibiwa magonjwa haya, basi na mwenzi wako pia umpeleke akapatiwe matibabu.
 
Top