SERIKALI
mkoani Kilimanjaro imesema magonjwa ya minyooo na kichocho ni tishio
kwa afya ambapo mwaka jana pekee wagonjwa 57,014 waliofika katika vituo
vya afya mkoani humo waligundulika kuugua magonjwa hayo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliyasema hayo wakati akifungua
warsha ya uhamasishaji juu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTD) kwa
wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri, wataalamu wa afya na
elimu wa wilaya za mkoa huo.
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Alfred Shayo, alisema magonjwa ya
minyoo na kichocho yanaongoza kwa kuathiri afya za wakazi wengi
kutokana na kutochukua tahadhari.
Alisema Wilaya ya Hai inaongoza kwa wagonjwa 12,012 wa minyooo.
“Rombo
inashika nafasi ya pili ya wagonjwa 10,753 waliotambulika, kati yake
wagonjwa 1,445 waligundulika kuwa na kichocho na wilaya ya Same ilikuwa
na wagonjwa 529 na Manispaa ya Moshi iliyokuwa na wagonjwa 359."
Mhandisi
Shayo alisema magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni magonjwa ambayo
yanaathiri jamii ya watu wenye kipato cha chini wanaoishi katika maeneo
duni ambayo upatikanaji wa huduma za afya na maji safi na salama ni
mgumu.
Aliyataja
magonjwa mengine kuwa ni pamoja na matende, mabusha, usubi, trakoma,
minyoo ya tumbo, homa ya malale, kichaa cha mbwa, tauni na tegu ambapo
alisema athari za magonjwa hayo yasipotibiwa mapema ni pamoja na
saratani ya kibofu cha mkojo, ugonjwa wa ini, upofu, utumbo kujifunga
pamoja na dalili za kifafa.