
Hoja yangu hiyo imethibitishwa hivi karibuni na timu moja ya Uingereza ambayo ilifanya utafiti na kuchapisha utafiti huo katika Makala ya Tiba ya Uingereza. Wanatimu hiyo wamesema, kutegemea tu maziwa ya mama pekee kwa watoto hadi miezi sita sio vizuri na hayatoshi. Wamesema maziwa ya mama yanaweza kuwa na faida iwapo watoto wataanzishwa vyakula vinginevyo mapema hasa baada ya miezi minne. Huko nyuma wataalamu walishauri kuwa mtoto apewe maziwa ya mama pekee hadi miezi sita lakini hivi sasa wamebadilisha msimamo huo na wanashauri mtoto aanze kupewa chakula kingine akiwa na miezi minne huku akiendelea kunyonyeshwa. Miaka 10 iliyopita Shirika la Afya Duniani lilitoa muongozo kwamba, watoto wachanga wanyonyeshwe maziwa ya mama pekee hadi miezi 6!
Utafiti mwingine umeonyesha kuwa, watoto wachanga wanaocheleweshwa kuanzishwa chakula kigumu hupatwa na upungufu wa damu au anemia kuliko wale wanaoanzishwa vyakula vingine wakiwa na miezi minne hadi 6. Hata hivyo wazazi na walezi wametakiwa kuzingatia aina ya vyakula wanavyowapa watoto wao wachanga pale wanapofikia muda wa kuanza kula, kwani baadhi ya vyakula huwasababishia allergies na pia kufanya wakose choo.