Lishe ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto – hili si jambo geni sana. Lishe bora ni lazima kwa watoto wadogo sababu wanatakiwa kukua vizuri – kimwili na kiakili.
Je lishe bora ni ipi?
Lishe bora ni chakula chenye virutubisho vyote muhimu kwa kiasi na uwiano sahihi ili kuuwezesha mwili wa mtoto kupata siha nzuri (afya bora). Wataalamu wanachambua zaidi kwa kusema kuwa lishe bora ina virutubisho aina sita, ambayo ni: Wanga, Protein, Mafuta, Vitamin, Madini na Maji.
Je vyakula gani ni bora ?
Lishe bora inatakiwa kuwa na mboga za majani, matunda, protini, wanga na madini ya kutosha. Hizi zinapatikana kwenye vyakula aina tofauti, na kuna vyakula vingine vina virutubisho vingi kwa pamoja.
Mfano wa vyakula vyenye lishe bora kwa kiwango kinachofaa ni kama mboga za majani, mafunda, nafaka asilia, vyakula vya protini (mayai, maharage, nyama n.k) na vyakula vyenye mafuta yasiyohifadhiwa mwilini.
Watoto wanagawanywa kwenye makundi ya aina mbili : Kuzaliwa hadi miezi 6 na kuanzia miezi 6na kuendelea. Haya makundi ni muhimu sababu watoto waliopo kwenye makundi haya wanatofautiana aina za vyakula wanavyokula. Ni muhimu kuzingatia hili sababu huu ndio muda muhimu zaidi katika ukuaji wa mtoto.

Lishe ya mtoto mchanga hadi miezi 6

Inashauriwa kuwa mtoto mchanga – tangu anazaliwa hadi afikapo miezi 6 – asipewe kitu chochote zaidi ya maziwa ya mama, hii ikiwa inamaanisha hata maji ya kunywa. Maziwa ya mama yana virutubisho vyote muhimu (pamoja na maji) vinavyohitajika kwenye ukuaji mzuri wa mtoto na kumpa kinga ya magonjwa mbalimbali.
Photo by Google

Lishe ya mtoto kuanzia miezi 6

Mtoto akishafika umri wa miezi 6, anaweza kuanza kula vyakula mbali mbali. Inashauriwa mtoto aanze kupewa vyakula mbali mbali kidogo kidogo ili apate kuzoea. Vyakula hivi lazima view vimepondwa, au viwe kwenye mfumo wa uji au maji sababu mtoto anakuwa hana meno yaliyokomaa au wengine wanakuwa hawajaanza kabisa kuota meno.

Lishe ya Mama

Photo courtesy of Google
Ukizungumzia mtoto hutoweza kuacha kuzungumzia mama. Mama ndiyo chanzo kikubwa cha chakula kwa mtoto tangu anazaliwa hadi anakuwa huru kula chakula cha kawaida. Kwa mwanamke mwenye umri wa kubeba ujauzito au mwenye ujauzito, ni muhimu kula vizuri ili kujenga afya ambayo ndio chanzo kikubwa cha virutubisho kwa mtoto tumboni na baada ya kuzaliwa. Ili kuwa na siha nzuri, vyakula vyote vinatakiwa kuwa na uwiano mzuri wa virutubisho.
Inatakiwa kuzingatiwa kuwa, vyakula vya mtoto viwe vya kuongezea lishe, lakini ni vizuri mtoto akiendelea kunyonya maziwa ya mama hadi atakapofikisha miezi 24. Maziwa ya mama ni muhimu katika kumfanya mtoto akue vizuri, hasa katika miezi 24 ya mwanzo. Inashauriwa kuwa, kama hakuna kikwazo – mfano: ugonjwa wa maambukizi unaoweza kumdhuru mtoto – ni vizuri mama amnyonyeshe mtoto kwa muda mrefu zaidi ya miezi sita (6).
Faida kubwa ya kunyonyesha ni kusaidia ubongo wa mtoto kukua vizuri zaidi sababu maziwa ya mama yanatoa virutubisho kwa wingi kuliko vyakula atakavyokula yeye moja kwa moja. Hii ni kwa sababu, tumbo la mtoot linakuwa halijazoea kusaga vyakula tofauti, hivyo maziwa ni chakula kinacholeta virutubisho vinavyotumika moja kwa moja mwilini.

Umuhimu wa lishe bora

Kama ilivyoelezwa mwanzo, lishe bora ni muhimu. Zifuatazo ni baadhi ya faida apatazo mtoto anayepata lishe bora:
  • Kuimarisha mfumo wa kinga mwilini na kuufanya mwili kupambana kirahisi na magonjwa kama utapiamlo (kwashiorkor) na kiriba tumbo
  • Kujenga siha nzuri (afya bora)
  • Kuleta furaha na Amani
  • Kusaidia ukuaji wa mwili na akili
  • Kuleta nguvu na kusaidia mwili kufanya kazi vizuri

Madhara ya lishe duni

Kama mtoto akiwa na lishe duni, haya yatakuwa madhara yake:
  • Kupata magonjwa mara kwa mara sababu anakosa kinga madhubuti dhidi ya magonjwa
  • Kudumaa kukua mwili na akili
  • Uwezekano mkubwa wa kupata ulemavu sababu mifupa inakuwa laini na haiwezi kustahimili uzito wa mwili.
  • Upungufu wa damu hivyo kudhoofisha afya ya mtoto
  • Kupata utapiamlo (Kwashiorkor)
  • Kupoteza maisha katika umri mdogo
 
Top