JIFUNZE JINSI YA KUJIKINGA NA MAGONJWA YA ZINAA
Magonjwa ya zinaa ni magonjwa yanayosababishwa na vijidudu ambavyo huenenzwa kwa njia ya ngono isiyo salama. Kuna magonjwa mbalimbali ya zinaa kama, kisonono, kaswende, klamidia, malengelenge na . Maambukizi ya VVU/UKIMWI ni mojawapo ya magonjwa ya zinaa, lakini hupewa uzito wa pekee kutokana na ukubwa wa ugonjwa huu.
Kama yalivyo magonjwa mengi ya kuambukiza, unaweza kujikinga na magonjwa ya zinaa. Mengi huambukizwa kwa njia ya ngono zembe, ingawa baadhi yanaweza kuwa an njia nyingine za maambukizi zaidi ya ngono. Kitu muhimu ni kwamba yanazuilika na unaweza kujikinga usipate magonjwa haya.
Magonjwa ya zinaa yana athari mbalimbali katika mwili wako na yanaweza kuleta ugumba, utasa, maumivu ya kiuno ya muda mrefu, kuharibu muonekano wa sehemu za siri na mengine kuongeza hatari ya kupata saratani za shingo ya uzazi au koo.
Ukiamua kujikinga na magonjwa haya inawezekana. Kitu cha kwanza na muhimu ni wewe kuchukua uamuzi huu na kuusimamia kwa nguvu zako zote. Zipo njia nyingi zitakazokusaidia kufikia hilo kama zinavyojadiliwa hapo chini:
Tumia Kondomu Kila Unapofanya Mapenzi
Hii huitwa ngono salama. Kinyume na hapo ni ngono zembe, kufanya mapenzi na mtu bila kutumia kondomu. Kondomu ni mpira maalum uliotengenezwa kuzuia magonjwa ya zinaa, VVU na mimba. Matumizi sahihi ya kondomu kila unapofanya ngono yatakusaidia kukukinga usipate magonjwa ya zinaa.
Acha ngono zembe, tumia kondomu.
Weka utaratibu wa kupima VVU na magonjwa ya zinaa wewe na mpenzi wako mara kwa mara.
Kupima VVU na magonjwa ya zinaa ni utaratibu mzuri hasa pale mnapoanza mahusiano ya kimapenzi. Utataka kujua kama wewe na mpenzi wako mko salama kabla ya kuanza ngono. Hata hivyo, watu wengi huishia kupima VVU peke na kuacha magonjwa ya zinaa. Ni vizuri mkapima na magonjwa ya zinaa, kwani wakati mwingine yanaweza yasioneshe dalili zozote. Pia muwe na utaratibu wa kurudi kupima mara kwa mara.
Epuka kuwa mpenzi zaidi ya mmoja.
Acha michepuko! Baki njia kuu. Itakulinda usipate magonjwa ya zinaa na VVU.