UgumbaUgumba ni hali ya kutoweza kupata ujauzito katika kipindi cha mwaka mmoja au zaidi kwa wenzi ambao wamekuwa wakifanya mapenzi bila kutumia njia zozote za uzazi wa mpango. Hali hii inaweza kutokea kutokana na tatizo kwa mwanaume au mwanamke, ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakidhani wanawake peke yao ndio ambao hupata tatizo hilo. Tatizo la ugumba huweza kupatiwa matibabu na kuisha.

Kuna Tofauti Gani Kati ya Ugumba na Utasa?

Tofauti na ugumba, utasa ni hali ya mwanamke kutoweza kushika ujauzito kabisa au mwanaume kutoweza kusababisha ujauzito kwa mwanamke kabisa.

Mtu tasa hana uwezo wa kupata mimba au kumpa mwenzi wake mimba kabisa, wakati mgumba ana uwezo wa kuja kupata mimba iwapo tatizo litaondolewa.

Nini Husababisha Ugumba?

Kuna sababu mbalimbali ambazo hupelekea ugumba kutokea kwa mwanaume au mwanamke.

Wanaume

Ugumba kwa wanaume hutokana na tatizo katika mbegu za kiume, manii kuwa kidogo, kushindwa kutembea, kuwa na umbo lisislo la kawaida au kuziba kwa mijira ya mbegu za kiume.

Tatizo kwenye mbegu za kiume linaweza kutokana na;

Uvutaji wa sigara
Dawa za kulevya kama matumizi ya bangi kwa wingi,
Mionzi (radiations)
Unywaji wa pombe
Kemikali kama DDT, risasi (lead)
Kufanya kazi mazingira yenye joto kali kama viwanda vya chuma.
Kuziba kwa mirija ya mbegu za kiume kutokana na magonjwa ya zinaa
Wanawake

Tatizo la ugumba husababishwa na sababu kuu mbili:

Kuziba kwa mijrija ya kupitisha mayai
Ovari kushindwa kutoa mayai ya uzazi.
Mirija ya kupitisha mayai inaweza kuziba kutokana na;

Ugonjwa wa Pelvic Inflammatory Disease (PID) ambao unatokana na magonjwa ya zinaa yasiyotibiwa kama kisonono na klamidia.
Mirija ya mayai kujaa maji
Utoaji mimba usio salama (unsafe abortions)
Upasuaji maeneo ya kiunoni
Ugonjwa wa endometriosis
Ovari kushindwa kutoa mayai ya uzazi inaweza kutokana na;

Umri mkubwa wa mwanamke, hasa miaka 35 – 40 na kuendelea.
Uvutaji wa sigara
Saratani ya Ovari
Mionzi (radiations)
Ugonjwa wa Polycystic ovarian disease
Sababu nyingine za ugumba kwa mwanamke zinaweza kuwa;

Makovu katika mji wa uzazi kutokana na kutoa mimba.
Mabonge ya kizazi (uterine fibroids)
Kuziba kwa shingo ya uzazi
Kulegea shingo ya uzazi
Kisukari
Matatizo ya tezi ya shingo (hyperthyroidism)
Kufanya mazoezi ya kupitiliza (excessive exercising)


Vipimo Vya Kujua Ugumba

Vipimo mbalimbali vinapatikana ili kuwezesha kugundua chanzo cha ugumba. Licha ya uwezo wa vipimo hivi, zaidi ya asilimia 10 ya watu wenye tatizo hili chanzo kinaweza kisijulikane kabisa. Ni vizuri kwa wenzi wote wawili wenye tatizo hili kuonana na daktati kwa ajili ya ushauri na vipimo.

Kwa wanaume hufanyika;

Kipimo cha manii (seminalysis) kuona kama manii zipo za kawaida na kwa kiwango kinachoatakiwa. Manii huchukuliwa kwa kondomu maalum wakati wa kufanya mapenzi au kwa kupiga punyeto na kisha kuchunguzwa kwa darubini.
Homoni za kiume kwenye damu; kipimo hiki hupima homoni za testosterone na Follicle Stimulating Hormone(FSH) ambazo huusika katika utengenezaji wa mbegu za kiume.
Kwa wanawake kuna vipimo vingi ambavyo huweza kufanyika, vikiwemo;

Hysterosalpingography – hutazama mirija ya uzazi (falllopian tubes) kama imeziba au la. Pia huonesha kama tumbo la uzazi lina vivimbe.
Ultrasound – kipimo hiki huonesha kama kuna vivimbe kwenye tumbo la uzazi, pia kwenye ovari kama kuna magonjwa yanayoweza kusababisha ugumba kama polycystic ovarian syndrome.
Homoni za kike katika damu – kipimo hiki hupima homoni za oestrogen na Follicle stimulating hormone ambazo huuusika kwenye kuandaa yai la uzazi kutoka kwenye ovari na upandikizaji kwenye mji wa uzazi.
Endometrial biopsy – tishu za mji wa uzazi huchukuliwa kuchunguza kama yai la uzazi limetoka. Pia huweza kuonesha kama kuna saratani ya mji wa uzazi au vinyama kwenye mji wa uzazi.
Matibabu ya Ugumba

Matibabu ya ugumba huhusishwa wenzi wote wawili, mwanaume na mwanamke. Yanahitaji uvumilivu na uelewa kwani wakati mwingine yanaweza yasiwe na mafanikio haraka au kabisa kama tunavyotarajia. Kuna njia mbalimbali za kutibu ugumba, hizi zote zikijumuisha kuondoa tatizo linalosababisha mimba ishindwe kutunga au kutumia njia za kusaidia mimba itunge.

Njia za matibabu ya ugumba hujumuisha:
Upasuaji

Mirija iliyoziba, vivimbe kwenye mji wa uzazi au kuta za uzazi kushikamana huweza kutibiwa kwa njia za upasuaji. Matibabu haya husaidia kuongeza uwezekano wa wenzi kupata mtoto.

Dawa

Matatizo ya ugumba yanayotokana na ovari kushindwa kutoa mayai ya uzazi huweza kutibiwa kwa dawa. Dawa  hizi hutumika kuziwezesha ovari kutoa mayai ya uzazi ili yaywe tayari kurutubishwa. Mara nyingi huweza kusababisha kutoa mayai mengi katika mzunguko mmoja na kusababisha ujauzito wa watoto wengi (mapacha au zaidi) pale yanaporutubishwa.

Teknolojia saidizi za uzazi (assistive reproductive technologies).

Hizi ni njia za kitaalamu ambazo zinatumika kusaidia wenzi kupata ujauzito kutokana na tatizo kwa mwanaume au mwanamke. Njia hizi ni  kama Artificial Insermination na In Vitro Fertilization.

Artificial Insermination. Njia hii hutumika pale ambapo mbegu za kiume zipo kwa kiasi kidogo.  Mbegu za kiume hukusanywa na kuingizwa kwenye mji wa uzazi kwa njia za kitaalamu.
In Vitro Fertilization. Njia hii hutumika hasa pale mirija ya mwanamke imeziba kabisa. Mayai na mbegu za kiume hukusanywa kitaaalamu na kisha yai kuchavushwa. Baada ya hapo yai lililochavushwa hupandikizwa kwenye mji wa uzazi.


Ugumba huathiri wanaume kwa wanawake wa kiwango kinachofanana, hivyo ni muhimu kwa wenzi wote wawili kushiriki katika matibabu.


Ugumba huathiri wenzi wengi kisaikolojia kwa kuleta hasira, majuto, msongo wa mawazo na hata kusababisha mvurugano katika mahusiano yao. Katika nchi zetu za kiafrika, wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa tatizo hili. Ni vizuri wenzi washirikiane katika hili, kwa kupeana moyo na kufuatilia matibabu kwa pamoja. Matibabu yanaposhindwa kabisa kuleta mafanikio, wenzi wanaweza kuasili mtoto/watoto kama watakuwa na utayari.
 
Top