Teknolojia Saidizi za Uzazi

Teknolojia saidizi za uzazi au kuzaa zikijulikana kama Assistive Reproductive Technologies kwa kingereza ni mbinu ambazo hutumika kusaidia wenzi wenye tatizo la ugumba kupata watoto pale ambapo imeshindikana kwa njia kama matibabu ya dawa au upasuaji. Njia hizi hujaribu kuruka vizuizi vinavyochangia mimba kutotunga kwa kutumia teknolojia. Njia hizi zilianza kutumika mwaka 1978, ambapo mtoto wa kwanza ‘test tube baby‘ alizaliwa kutokana na mimba iliyotungwa kwa njia hii.

Teknolojia saidizi za uzazi hujumuisha;

Upandikizaji mbegu – Artificial Insemination.
Upandikizaji wa kiinitete – In Vitro Fertilization (IVF).
Upandikizaji mbegu – Artificial Insemination

Njia hii hutumika kutibu ugumba kutokana na matatizo mengi, hasa mbegu za kiume kuwa kidogo sana au kushindwa kuogelea kufikia yai. Pia hutumika pale ambapo shingo ya uzazi ya mwanamke imeziba au ute wa shingo ya uzazi unaua manii.

Mbegu za kiume hutolewa kwa kupiga punyeto, kuwa concentrated kwa vifaa maalum na kisha kuingizwa kwenye mji wa uzazi kwa kutumia sindano maalamu. Njia hii hufanyika pale ambapo yai la mwanamke limetoka au wakati mwingine mwanamke hupewa dawa za kuchochea  ovari kutoa mayai ya uzazi siku kadhaa kabla ya njia hii kutumika.

Wanawake wasio na wapenzi na wanataka watoto au wanaume wenye manii zenye matatizo, huweza kupata manii kutoka kwenye benki za manii (sperm banks) na kisha kupandikiziwa.

Njia hii huchukua masaa kadhaa kufanyika, mara nyingi haizidi masaa mawili na huwa haileti maumivu kwa mwanamke.

Mafanikio ya njia hii ikifanyika kwa usahihi ni asilimia 15 mpaka 20. Huweza kurudiwa mara 3 – 4 kwenye mizunguko mingine ya hedhi kama haikufanikiwa kwa mara ya kwanza.

Upandikizaji wa kiinitete – In Vitro Fertilization (IVF)

Upandikizaji wa kiinitete  maarufu kama IVF hutumika kutibu ugumba kutokana na matatizo kwa mwanaume au mwanamke kama manii kuwa kidogo au kuziba mirija ya kupitisha mayai.

Njia hii ilianzishwa mwaka 1978, na ni kati ya njia zenye ufanisi mkubwa. Takwimu zinaonesha 1 kati ya watoto 50 nchini Swedeni, 1 kati ya 60 nchini Australia na 1 kati ya 80 nchini Marekani wanazaliwa kwa njia hii.



Kinachofanyika katika njia hii ni;

Mayai ya kike hukusanywa kwa mwanamke hupewa dawa za kusaidia kutoa mayai kutoka kwenye ovari na kisha mayai hutolewa kwa kifaa maalum.
Mayai huchanganywa na manii kwenye kidishi maalum cha maabara na kurutubishwa.
Yai likisharutubiwa na manii, huachwa likue kidogo kwa siku 2-3  kuwa kiinitete ambacho huchukuliwa na kisha kupandikizwa kwenye mji wa uzazi wa mwanamke.
Kiinitete hiki hujishikiza kwenye mji wa mimba na kukua kutengeneza ujauzito.
teknolojia saidizi za uzazi
teknolojia saidizi za uzazi
teknolojia saidizi za uzazi – IVF

Kabla ya njia hii kuanza kutumika, vipimo hufanyika kwa wenzi hawa ikiwemo vya manii, homoni, hysterosalpingography, ultrasound ya kizazi na ovari.

Ufanisi wa IVF
IVF ni kati ya teknolojia za uzazi zenye ufanisi mkubwa. Njia hii ina ufanisi wa asilimia 15 mpaka 38. Ufanisi huu hupungua kadri ya umri wa mwanamke unazidi miaka 35.

Faida za IVF

Kutumia manii za mwanaume mwingine kupata ujauzito kama manii za mwenzi wa mwanamke zina matatizo kiasi cha kushindwa kusababisha mimba.
Kupata ujauzito kwa mwanamke asiye na mayai kwa kutumia mayai ya mwanamke mwingine.
Hasara za IVF

Ujauzito wa watoto wengi (mapacha au zaidi), karibu ya asilimia 31 ya mimba kutokana na IVF zinakuwa ni za mapacha na asilimia 3 ikiwa ni watoto 3 au zaidi.
Mtoto kuzaliwa njiti (preterm delivery).
Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo sana.
Mtoto kuzaliwa na matatizo. Asilimia 6 ya mimba zinazotokana na IVF huweza kupata matatizo hayo ukilinganisha na asilimia 4 kwa mimba za kawaida.
Gharama kubwa za kutumia teknolojia hii.
 
Top