Kila mtu hupenda aonekane vizuri na hali ya kupendeza sana. Kitu ambacho asilimia kubwa ya watu hivi sasa wanakiheshimu kwa hali ya juu ni nywele na ndio sababu kubwa ya urembo wa mtu awe mwanaume au mwanamke na ndio maana utaona wengi huchonga staili mbalimbali ya nywele zao kama vile panki, viduku na staili nyinginezo na huku wakiweka piko au superblack katika nywele zao ili ziwe na weusi wenye kung’aa na kuvutia.

Lakini sasa nywele hizi huanza kuota mvi haraka sana na kusababisha vijana wengi kujisikia vibaya kuona kama wanazeeka hali ya kuwa na umri mdogo. Je? Umeshajiuliza kuwa nini kina sababisha kuota mvi hizi wakati wa umri mdogo? Zifuatazo ndio sababu:-

Kuwa na msongo mkubwa sana wa mawazo:

Maisha ya kisasa pamoja na faraja zote hizi tulizonazo lakini bado vijana huwa na msongo mkubwa wa mawazo kutokana na mambo au matatizo mbalimbali yanayowakumba katika maisha yao, iwe ni matatizo ya kikazi, kimapenzi au hata kimasomo. Hali hii husababisha afya kuwa duni na ndivyo utaona hata nywele sasa kuanza kuwa na mvi.

Kurithi

Ule umri ambao nywele zako zinaanza kubadilika na kuwa nyeupe hutegemea pia ukoo wako jinsi ulivyo, hii ni ile hali ya kurithi kimaumbile. Kama vile mtu anavyoweza kurithi urefu au ufupi wa mzazi wake yeyote, au kurithi rangi ya ngozi vilevile anaweza kurithi na mabadiliko haya ya nywele kwani kama mzazi wako alikuwa na mvi katika umri mdogo basi hata wewe pia uwezekano huo upo.

Mlo mbaya

Mlo kamili huchukua nafasi kubwa sana katika kuboresha afya yako ambayo pia inahusika na nywele. Ukosefu wa Vitamin B12 ni sababu kubwa hasa ya kufanya nywele kuota mvi, hivyo ili kuweza kurekebisha tatizo hili ni vema ukajitahidi kula vyakula vyenye hivi Vitamin B12 kama vile Samaki wakubwa, Nyama, Mayai, Maziwa na kadhalika.

Ulevi wa Sigara na Pombe

Mvi zinaweza pia kusababishwa na uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe. Hii ni kwasababu vitu hivi huleta athari katika mfumo mzima wa mwili hivyo hufanya afya yako kutetereka na hatimaye kusababisha mvi kutokea.

Kuzidisha unywaji wa baadhi ya vinywaji

Unywaji uliokithiri wa chai, kahawa, vyakula vya kukaanga husababisha mvi,  hivyo ili upunguze au uepukane na hili ni vema kutozidisha utumiaji wa vitu hivi.

Mshtuko wa kihisia

Wakati mwingine Mvi hutokea kwa muda mfupi tu pale mtu anapokuwa katika hali ya mshtuko fulani kihisia. Lakini hili ni jambo la muda mfupi tu kisha mtu akiwa katika hali ya kawaida mvi hizi hutoweka baada ya muda fulani.

Ukiangalia sababu kubwa ya mvi utaona zimeegemea sana katika suala zima la Afya, hivyo ni bora mtu kuwa makini na Afya yako, Itunze Afya yako vyema, kula mlo kamili, pumzisha akili yako kwa kulala muda mrefu usiopungua masaa 8. Hakika siri kubwa ya urembo na uzuri wa mtu ni Afya na si vinginevyo. Afya ndio msingi wa uzuri wa mtu mambo mengine hufuatia tu.

Nashukuru kwa kusoma makala hii na ikiwa una lolote la kuongeza, maswali, ushauri jisikie huru kutuandikia kwani tuko pamoja katika kuelimisha jamii yetu. Ahsante.
 
Top