UJUE UGONJWA WA KIFUA KIKUU: SABABU, DALILI, VIPIMO NA NJIA ZA KUJIKINGA
Ugonjwa wa kifua kikuu ni ugonjwa wa mapafu unaosababishwa na vijidudu vya bakteria aina ya Mycobacterium tuberculosis. Kifua kikuu hujulikana kwa kiingereza kama Pulmonary Tuberculosis au PTB kwa kifupi. Pamoja na kushambulia mapafu na kusababisha kifua kikuu, vijidudu hivi huweza kushambulia sehemu nyingine za mwili kama utumbo, uti wa mgongo, mifupa na kuleta homa za TB huko.
Kifua kikuu ni ugonjwa unaotibika na ukapona kabisa. Ni muhimu kuwahi kwenye kituo cha afya ili upimwe na upate matibabu stahili haraka. Matibabu yake huchukua muda wa miezi 6.
SABABU ZA UGONJWA
Ugonjwa wa kifua kikuu husababishwa na vijidudu vya bakteria viitwavyo Mycobacterium tuberculosis. Pia bakteria wanaopatikana kwenye maziwa waitwao Mycobacterium bovis husababisha ugonjwa huu endapo mtu atatumia maziwa yasiyochemshwa.
NJIA ZA MAAMBUKIZI
Zaidi ya watu milioni 8 hupata kifua kikuu kila mwaka. Kifua kikuu huambukizwa kwa njia ya hewa.
Mtu anayeumwa kifua kikuu anapopiga chafya bila kuziba mdogo, vijidudu vya kifua kikuu hutoka pamoja na chembechembe ndogo sana za mate (aerosols) ambazo husambaa hewani. Mtu aliye karibu anapovuta hewa hiyo, huvuta pamoja na vijidudu vya kifua kikuu. Vijidudu hivi vinapofika kwenye mapafu, huingia kwenye seli za mapafu ambapo hudhibitiwa na kinga ya mwili. Idadi kubwa ya watu ina maambukizi ya vijidudu vya kifua kikuu (latent infection) lakini hawana dalili kwani kinga ya miili yao ipo imara kuzuia vijidudu visizaliane.
Pia maambukizi ya vijidudu vya TB yanaweza kutokea endapo utatumia maziwa ya ng’ombe yasiyochemshwa.
VITU VINAVYOHATARISHA MTU KUUMWA KIFUA KIKUU
Zaidi ya theluthi ya watu duiniani wana maambukizi ya TB lakini hawana dalili za kifua kikuu, asilimia 10 tu ndio huja kupata ugonjwa wa kifua kikuu. Hii ni kwa sababu kinga ya mwili huwa imara na kuzuia vijidudu vya TB kuzaliana na kushambulia mwili. Vitu vifuatavyo huchangia kutokea kwa kifua kikuu kwa mtu aliyepata maambukizi ya TB:
UKIMWI/VVU
Upungufu wa kinga mwilini kutokana na dawa au magonjwa mengine ukiacha UKIMWI.
Kisukari
Utapiamlo
Uvutaji wa sigara sana
DALILI ZA KIFUA KIKUU
Baada ya kupata maambukizi ya vijidudu vya TB unaweza usiwe na dalili zozote za kifua kikuu. Asilimia 10 ya walioambukizwa vijidudu vya TB huenda kupata ugonjwa wa kifua kikuu, hii ni kutokana na kinga ya mwili kudhoofu kutokana na sababu mbalimbali. Kinga ya mwili ikidhoofu vijidudu vya TB vinapata nafasi ya kuzaliana na kushambulia mwili, hapa ndipo ugonjwa wa kifua kikuu hujitokeza.
Dalili zinaweza kuwa kali au za kawaida kwa muda mrefu. Unaweza kupata dalili zifuatazo:
Kukohoa kwa kipindi cha wiki 2 au zaidi. Ikiwa unapata kikohozi kisichoisha kwa wiki 2 au zaidi licha ya kutumia dawa za matibabu basi inaweza kuwa dalili ya TB.
Kukohoa makohozi yenye damu. Mara nyingi watu wenye kifua kikuu hupata makohozi meupe ambayo mara nyingine yanaweza kuwa na damu damu.
Homa za mara kwa mara. Unaweza ukapatwa na homa mara kwa mara, hasa ikipanda zaidi wakati wa usiku. Hii inaweza kuambatana na kutokwa na jasho jingi hasa wakati wa usiku, kiasi cha kuweza kulowesha shati, blauzi au shuka ulilolalia. Homa inaweza kuwa ya kujirudia rudia kwa zaidi ya mwezi au miezi kadhaa.
Kupungua uzito. Unaweza ukaona nguo zinakupwaya, uzito unapungua au unakonda bila sababu maalum.
Kutokwa na jasho kali usiku.
Kukosa hamu ya kula na kujisikia vibaya.
Maumivu ya kifua.
Ugonjwa ukiwa umekuwa mkubwa unaweza kuleta dalili nyingine kama:
Kupumua kwa tabu
Maumivu ya kifua
Pamoja na kushambulia mapafu mara nyingi, TB huweza kusambaa na kushambulia sehemu nyingine za mwili na kusababisha TB ya mifupa, tumbo, uti wa mgongo, maji kujaa kwenye mapafu, usaha kujaa kwenye mapafu na TB ya moyo.
VIPIMO
Ili kuthibitisha ugonjwa wa kifua kikuu pale mtu anapokuwa na dalili za ugonjwa vipimo vifuatavyo vinaweza kufanyika.
Kipimo cha damu cha Erythrocyte sedimentation rate (ESR).
Uchunguzi wa makohozi kwa darubini (AFB Staining)
Kipimo cha picha ya kifua (Chest X-ray)
Kuotesha makohozi (sputum culture)
Vipimo vingine vinavyoweza kufanyika ni Full Blood Picture (FBP).
ATHARI ZA KIFUA KIKUU
Mara nyingi kifua kikuu hushambilia tishu za ndani za mapafu na baada ya matibabu mgonjwa hupona. Wakati mwingine kutokana na ukali wa ugonjwa au kuchelewa matibabu, kifua kikuu inaweza kuleta madhara yafuatayo:
Maji kujaa kwenye mapafu (pleural effusion).
Kuvimba kwa tezi za limfu shingoni
TB ya uti wa mgongo (TB meningitis)
TB kusambaa mwilini (miliary TB)
TB ya mifupa
KUJIKINGA
Chanjo ya TB hutolewa kwa watoto wote wanaozaliwa. Muhimu khakikisha mtoto wako anapata chanjo hii baada ya kuzaliwa. Kama amezaliwa nyumbani muwahishe hospitali haraka.
Unapokohoa hakikisha unaziba mdomo ili kuzuia kusambaa kwa vijidudu kwenye hewa.
Hakikisha unaishi sehemu yenye mwanga na hewa ya kutosha.
Unapoona dalili zinazofanana na za kifua kikuu wahi hospitali mapema kwa ajili ya vipimo na matibabu.