Lehemu na Hatari ya Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu
Lehemu hujulikana kama cholesterol kwa Kiingereza. Ni aina ya mafuta ambayo ni sehemu muhimu ya ufanyaji kazi wa mwili wa binadamu. Lehemu hubebwa kwenye damu na aina ya protini iitwayo lipoprotini. Kutokana na uzito wa protini hizi kuna Low Density Lipoprotein (LDL) na High Density Lipoprotein (HDL).  Kati ya hizi HDL ni lehemu nzuri na LDL ni lehemu mbaya.

LEHEMU INAVYOATHIRI MWILI

Kiasi cha lehemu ya kwenye damu kinapoongezeka na kuwa juu, huongeza hatari ya magonjwa ya moyo kama shambulio la moyo, shinikizo la damu na magonjwa mengine kama kiharusi. Aina ya lehemu ambayo huathiri mwili vibaya ni LDL au Low Density Lipoprotein, hii inapoongezeka sana ndio huongeza hatari ya magonjwa haya.

Lehemu ya LDL inapoongezeka sana kwenye damu, hujikusanya ndani ya mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo na ubongo. Kadri inavyozidi kujikusanya ndipo inavyopunguza tundu la mishipa ya damu. Hali hii huitwa atherosclerosis kwa kitaalamu. Inapotokea damu imeganda basi huziba sehemu ya mshipa lehemu ilipo jikusanya na hivyo shambulio la moyo au kiharusi hutokea.

NJIA ZA KUPUNGUZA LEHEMU MWILINI

Kudhibiti kiasi cha lehemu mwilini mwako ni sehemu muhimu sana ya kukabiliana na hatari ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. Unaweza ukazingatia yafuatayo kukusaidia kufanikisha hili.

Fanya mlo wako uwe na mboga za majani, matunda, nafaka zisizokobolewa, mafuta ya mimea na nyama nyeupe zisizo na mafuta.
Fanya mazoezi ya mwili. Pata angalau nusu saa kwa siku kukimbia, kuruka kamba, kuendesha baiskeli, kuogelea, kutembea haraka, kucheza au vingine unavyopenda kufanya ili mradi umuvike na utoe jasho!
Usivute Sigara
 
Top