Jino
Umewahi kufikiria juu ya mtu yeyote anayekuvutia kwa sura yake tu bila meno? Bila shaka kama asingekuwa na meno safi yenye mpangilio mzuri asingekuwa na sura yenye mvuto kwako. Idadi ya meno ya mtu mzima mwenye umri wa kuanzia miaka 21 huwa ni 32 na yanapaswa kudumu muda wote wa maisha yake.


Meno ya binadamu, mbali na kufanya kazi ya kutafuna chakula, humsaidia pia kuzungumza. Meno hutengeneza umbo la mdomo na mashavu, hivyo kuboresha tabasam ya mtu na kuifanya ivutie. Kimsingi, meno ni muhimu na kutokana na umhimu huo, ndiyo maana inashauriwa kuyatunza vizuri muda wote.

Ugonjwa unaosumbua sana meno, ni kuuza. Kwa mujibu wa wataalamu wa magonjwa mbalimbali duniani, baada ya ugonjwa wa mafua, ugonjwa mwingine unaosumbua zaidi watu ni kuoza kwa meno.

Kuoza kwa meno ni nini?

Kuoza meno,  ni hali ya sehemu ya juu na ndani ya jino kutoboka. Hii inatokana na ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vyenye sukari. Vijidudu vya bakteria wanaoishi kinywani humeng'enya mabaki ya vyakula tunavyokula na kutoa tindikali (asidi) ambayo inadhoofisha sehemu ya nje ya jino na kusababisha jino kutoboka.

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 60 na 90 ya watoto wote wenye umri wa kwenda shule duniani kote, wana ugonjwa wa meno kutoboka. Nchini Tanzania, kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka minne hadi sita, kati ya watatu, mmoja ana jino lililotoboka kwa maana ya kuoza.

Mbali na ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, zipo sababu nyingine zinazosababisha meno kuoza. Sababu ya kwanza ni bakteria aina ya Streptococci na Lactobacilli. Mtu anapokula chakula na kuacha mabaki ya chakula mdomoni, baadae mabaki hayo hutengeneza ‘ukoga.’

Ukoga ni utando mwembamba wa bakteria unaotokana na mabaki ya chakula mdomoni na kuota kwenye meno. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), asilimia kati ya 60 na 90 ya watoto wa shule, pamoja na takriban asilimia 100 ya watu wazima duniani kote, wana ukoga katika meno yao.

Bakteria wanapokula mabaki ya chakula mdomoni, hasa sukari, hukibadili chakula hicho kuwa tindikali (asidi). Tindikali hiyo huvamia tabaka gumu la juu la jino (enamel), huozesha na kulifanya liwe na matundu. Matundu hayo yanapobomoka na kuwa shimo kubwa, jino huanza kuoza. Inawezekana mtu asihisi chochote wakati huo, lakini jino linapooza kufikia sehemu zenye neva ndipo mtu anapoanza kupata maumivu makali.

Bakteria wanaotengeneza ukoga wana njia nyingine ya kuleta madhara kwenye meno. Mtu anaposukutua meno kwa mfano, kama ukoga hautasuguliwa na kuondolewa vizuri, ukoga huo unaweza kuwa mgumu na kutengeneza tabaka la vijiwe (calculus) ambayo hufanya fizi zivimbe na kuachana na meno.

Hali hiyo hutokeza nafasi kati ya meno na fizi ambapo mabaki ya chakula hukwama na kuliwa na bakteria wanaoweza kuathiri fizi. Mtu akipuuza tatizo hilo, tishu inayozunguka meno yake inaweza kuharibika kabisa na kufanya meno yang'oke. Watu hupoteza meno zaidi kwa njia hii kuliko hata meno yanayooza.

Ni vyakula gani hasa vinavyochangia meno kuoza?

Vyakula vinavyochangia kwa kasi kuoza meno ni pamoja na biskuti, chokoleti, kashata, Soda, pipi, isikrimu, keki, ubuyu wenye sukari, visheti na vyakula vingine vya aina hiyo vinavyotengenezwa kwa kuchanganywa na sukari.

Baadhi ya dalili au viashiria vya kuoza meno ni pamoja na alama nyeusi sehemu za pembeni za jino au kwenye incha za kutafunia, jino kutoboka (uwepo wa shimo katika jino au meno), kuvimba sehemu ya fizi au shavu upande wa jino linapouma na maumivu katika jino.

Ni njia gani zinashauri kukinga meno yasioze?

Mwili wa binadamu una njia ya asili ya kuzuia kuharibika kwa meno. Njia hiyo ni kutengeneza mate. Mate husaidia kulinda meno kwa kiasi fulani kutokana na bakteria. Msomaji wa FikraPevu baada ya mlo, mate yanahitaji dakika 15 hadi 45 kuondoa mabaki ya chakula na kupunguza kiasi cha asidi kwenye ukoga wa meno.

Muda huo unategemea kiwango cha sukari na mabaki ya chakula yaliyonata kwenye meno. Kwa hiyo, kiwango cha uharibifu unaofanywa kwenye meno, kinategemea ni mara ngapi mtu anakula na kiwango cha vitafunio vyenye sukari anavyotumia, wala si kiasi cha sukari anachokula.

Kwa kuwa kiwango cha mate huwa kinakuwa kidogo mtu anapokuwa amelala usingizi, ni muhimu kabla mtu hajapanda kitandani kulala, akasukutua kinywa na meno kwa mswaki na maji safi na salama.

Madaktari wa meno wanapendekeza uchunguzi wa meno uwe unafanyika walau mara moja au mbili kwa mwaka kutegemeana na hali ya meno. Watu wengi huogopa au husita kumuona daktari wa meno kwa uchunguzi wa meno kwa sababu ya gharama. Wengine wanapuuza tu kutibu meno kwa sababu hawajali na wengine waoga tu.

Hata hivyo, inashauriwa kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa meno, kwa kuwa hiyo itamwepusha mtu gharama kubwa za kutibu au kung’oa jino lililooza. Kwa watu wazima, madaktari wa meno hushughulika kwa kuzuia ugonjwa wa fizi zaidi kwa sababu meno yakiwa na vijiwe ni rahisi kuondolewa.

Meno yenye afya hutegemea chakula anachokula mtu. Lishe bora yenye kalisi na vitamini A, C na D husaidia meno yawe na afya bora kuanzia mtu anapokuwa tumboni hadi meno yanapoota utotoni na kukomaa ukubwani. Inashauriwa kila mtu kujitahidi kula chakula kinachofaa kwa ajili ya ulinzi wa afya bora ya meno. Vyakula vinavyofaa ni pamoja na kuepuka kula vyakula vyenye sukari nyingi.

Njia nyingine rahisi ya kulinda afya ya meno ni kusafisha katikati ya meno kila siku kwa kutumia uzi mwembamba vijiti vya kutoa uchafu katikati ya meno. Kuacha mabaki kwenye meno kunasababisha bakteria walio mdomoni kutengeneza tabaka la chakula na bakteria, tabaka ambalo litafanya iwe rahisi kwa fizi na meno kushambuliwa na bakteria hao hadi kuoza.

Wataalamu mbalimbali wa kinywa na meno wamegundua kwamba sukari ya asili inayoitwa Xylitol, inasaidia kudhibiti ukoga unaofanya meno yaoze. Kwa hiyo, kwa mujibu wa wataalamu hao, mazoe ya kutafuna chingamu au bazoka zenye sukari ya Xylitol, kunasaidia kuzuia kuoza kwa meno.

Inashauriwa pia kusukutua meno kila baada ya mlo au kupiga mswaki kabisa mara mbili kwa siku, kwa maana ya asubuhi baada ya kuamka na usiku kabla ya kabla ya kwenda kulala.

Upigaji wa mswaki una utaalamu wake. watu wengi hawasugui sehemu zote za meno yao. Kwa hiyo, kwa kumuona mtaalamu wa kinywa na meno, kunaweza kusaidia kupata uelewa wa mbinu au njia bora za kupiga mswaki.

Njia bora ya kupiga mswaki

Kwanza, kwa kuwa dawa ya meno hukwaruza na wakati mwingine inaweza kuwa ngumu mara nyingi kuliko jino, inashauriwa kutumia kiasi kidogo cha dawa ya meno.

Pili, pinda kidogo mswaki kutoka kwenye mwisho wa fizi, kisha kwa utaratibu kabisa, piga mswaki kutoka kwenye fizi kwenda chini. Hakikisha kwamba mswaki unapigwa sehemu zote za meno, ndani na nje.

Tatu, piga mswaki pole pole kwenye incha za meno za kutafunia. Ili kusafishe sehemu ya ndani ya meno ya mbele, shikilia mswaki wima na kisha piga mswaki kutoka kwenye fizi hadi kwenye sehemu ya kutafunia. Mwisho, kabla ya kumaliza, hakikisha unapiga mswaki ulimi na sehemu ya juu ya kinywa.

Je, meno yaliyokwishaharibika yanaweza kurekebishwa? Jibu hapa ni ndiyo. Kama meno yameharibika, yameng'oka au yameota vibaya, siku hizi madaktari meno wanazo njia nyingi mpya za kuyarekebisha.

Kwa mfano, kama mtu meno yake ya mbele yamevunjika au yana rangi isiyo ya kawaida, Daktari anaweza akapendekeza yafunikwe kwa kutumia kitu fulani kinachofanana na meno. Kifuniko hicho kinaunganishwa na jino lililoharibika na kulifanya liwe na sura mpya kabisa kwa kutumia dhahabu au kitu kingine kinachofanana na jino la kawaida.

Aidha, kama meno yameng'oka tayari, Daktari anaweza kuweka meno bandia au anaweza kuweka kitu kinachoshikilia meno bandia, ambacho kitaalamu kinaitwa bridge. Kwa mujibu wa WHO, karibu asilimia 30 ya watu wenye umri kati ya miaka 65 na 75, meno yao ya asili yameshang’oka.

Kwa hiyo, ili kulinda umbo la kinywa na mashavu, watu wenye umri huo huweza kuwekewa mdomoni meno ya bandia. Mbinu nyingine ya kurekebisha meno yaliyong’oka inayozidi kuwa maarufu, ni kupandikiza meno. Kwa mfano, meno yaliyoota vibaya, kwa maana ya kutokuwa na mpangilio mzuri, yanaweza kurekebishwa kwa kuwa kuyaacha kama yalivyo, kunaongeza hatari kupata magonjwa.

Ni kosa kubwa kuacha kutibu jino mapema kwa sababu, mbali na kuongeza gharama wakati wa kulitibu, linaweza kumsababishia mtu maumivu makali, linaweza kuvunjika, mtu anaweza akashindwa kutafuna vizuri chakula na zaidi akajisikia ukakasi au ganzi kila unywapo vitu vya baridi au vya moto, jino linaweza kutoa usaha kinywani na pia kupungua kwa ubora wa maisha.
 
Top