FamilyKWA mujibu wa Shirika la Afya Duniani, matumizi ya njia za uzazi wa mpango yameongezeka sehemu tofauti za dunia hususani katika Bara la Asia na Amerika Kusini lakini matumizi yamebaki kuwa chini kwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.
Aidha, inakadiriwa wanawake milioni 225 katika nchi zinazoendelea wangependa kuchelewa au kuacha kupata watoto lakini hawatumii njia yoyote ya kujikinga kupata mimba. Njia za uzazi wa mpango ni njia zinazozuia mimba hadi wakati uliopangwa kufikia. Njia hizi zinaweza kutumiwa na jinsia zote, kwa kufuata vigezo vya kila njia.
Njia za uzazi wa mpango ni za aina nyingi sana, kulingana na jinsi inavyofanya kazi, itakavyofanya kazi, jinsi inavyotolewa kwa mteja n.k, njia za kisasa za uzazi wa mpango ni kama vidonge vya uzazi wa mpango, vipandikizi, vitanzi, sindano za uzazi wa mpango, kutumia kondomu, kukata mirija ya mbegu za kiume, kufunga uzazi kwa wanawake ambapo baadhi ya njia za asili ni pamoja na njia ya kalenda, njia ya kumwaga nje mbegu na nyinginezo.

Kuna baadhi ya watu hufikiri kuwa na watoto wengi kunakupa furaha, kitu ambacho sio kweli, kwa maana wanasaikolojia wanasema furaha ya mtu itategemea mzazi mwenyewe na jinsi mtoto alivyo.
Kina mama waliozaa watoto bila uzazi wa mpango hukosa furaha hasa pale watoto wasipokuwa na afya njema kwa maana watalazimika kuwapeleka hospitali watoto mara kwa mara na kushindwa kufanya mambo mengine yenye faida kwao.
Fikra potovu na tamaduni mbovu zilizopo maeneo mengi ya vijijini ambapo ndio asilimia kubwa ya watu wanaozaa bila mpango maalumu hupatikana, husababisha kina mama kuzaa mfululizo bila kupumzika kitu ambacho ni hatari kwa afya yao. Ripoti zinaonyesha wanawake wenye watoto zaidi ya wanne wapo katika hatari kubwa ya kufariki kwa matatizo ya uzazi.
Akizungumza katika warsha iliyoandaliwa na taasisi moja ya kimataifa inayojulikana kwa jina la World Lung Foundation, mjini Kigoma, Mchungaji Oberd Kondora, wa Bitale mkoani humo amesema, "Kwa mfano jamii ya Waha wanaona ni vizuri kuzaa watoto wengi sana kwasababu kama sehemu ya majilimbikizi ya kwamba wakifa hawa basi angalau wabaki na hawa. Mungu ndiye ameweza kutuambia tuzae tuongezeke, tuifanye dunia itawalike na maana ya kutawalika ni pamoja na ardhi na sisi watu wenyewe na tunatakiwa tuzae katika hatua ya mpango, maana yake twende hatua kwa hatua, tusiendelee tu kuzaa kwa maana ya kuzaa." alielezea kwa msisitizo Kondora.
Sheikh Madua O. Rezebanga wa Bitale mkoani Kigoma alisema, "Vitabu vya dini vinaasa, kwasababu Mungu mwenyewe baada ya kuwa ametoa utaratibu wa kuzaana, alielekeza kwamba mtoto awe na uwezo wa kunyonya miaka miwili hadi mitatu, akiwa na maana hapo katikati mama atapumzika na ataweza kufanya shughuli nyingine lakini itampa nafasi mzazi au mlezi kumtimizia haki mtoto ikiwa ni pamoja na elimu, malazi na mavazi ili aweze kuishi kwa utaratibu na kwa afya nzuri." alikarirriwa na FikraPevu.
Ameongeza kwa kusema kuwa "Mwenyezi Mungu amesema katika Quran 4 aya ya 29; 'Msije mkaingiza mikono yenu katika mambo ya kujihikilisha' Mwenyezi Mungu ana maana kwamba katika kupanga uzazi utakapokuwa hukufuata utaratibu wa Mwenyezi Mungu anavyopendezwa mkazaa kwa utaratibu mtoto akawa na uwezo wa kunyonya muda ambao Mwenyezi Mungu ameelekeza kwenye Quaran ni maana kwamba mama anaweza kupoteza maisha ikibidi na yule mtoto akapoteza maisha, hivyo kujihikilisha ambako kumetajwa katika aya hii ya 29 ni maana kwamba ni pale ambapo hukufuata utaratibu hatima yake mama atazaa bila utaratibu, atakuwa na afya mbovu, mwisho atapoteza maisha.

Faida za uzazi wa mpango;
Huzuia hatari zinazoambatana na mimba kwa wanawake
Uwezo wa mwanamke kuchagua muda anaotaka kushika ujauzito ni kitu chenye faida kubwa kwa ustawi wake. Njia za uzazi wa mpango zinaruhusu nafasi ya miaka kati ya mtoto na mtoto pia huchelewesha mimba kwa wasichana wadogo waliobalehe ambao wako katika hatari kubwa za kiafya pamoja na kifo kama wakizaa mapema.
Husaidia kuzuia VVU/Ukimwi
Njia za uzazi wa mpango hupunguza hatari ya mimba zisizotarajiwa kwa wanawake wanaoishi na VVU, hivyo kufanya idadi ndogo ya watoto wenye VVU na mayatima. Zaidi ya yote kondomu za kike na za kiume ni njia thabiti ya kuzuia mimba na magonjwa ya ngono ikiwemo VVU.
Huwawezesha watu na kupandisha elimu kiujumla
Uzazi wa mpango huwapa watu uhuru wa kuchagua kuhusiana na mambo ya afya ya uzazi. na huwakilisha nafasi ya wanawake kujiendeleza kielimu, kushiriki katika shughuli za kijamii na za kiuchumi hasa kazi za kulipwa kwenye mashirika tofauti na familia.
Hupunguza mimba za utotoni
Njia za uzazi wa mpango zinapunguza utoaji mimba hasa usio salama. Mimba za utotoni huongeza hatari ya kuzaa watoto njiti au wenye uzito pungufu kitu kinachoweza kusababisha vifo vya watoto wachanga. Wasichana wengi wanaopata mimba utotoni huacha shule, kitu kinachoweza kuathiri maisha yao, maisha ya familia zao na maisha ya jamii kiujumla.
Hupunguza ukuaji wa idadi ya watu hovyo
Itakumbukwa kwamba uzazi wa mpango ni ufunguo wa kupunguza ukuaji mbaya wa idadi ya watu unaoweza kuleta athari mbaya katika uchumi, mazingira na jamii kiujumla. Njia za uzazi wa mpango huwapa watu nguvu na haki ya kupanga idadi na wakati muafaka wa wao kuwa na watoto wawatakao.
Kupunguza vifo vya watoto
Uzazi wa mpango huzuia watoto waliozaliwa karibu karibu, mimba na uzazi usio salama hivyo kupunguza idadi ya watoto wanaokufa. Kwa kuzuia mimba zisizotarajiwa, uzazi wa mpango huzuia vifo vya kina mama na watoto wao.
Nani hutoa huduma za uzazi wa mpango?
Huduma za uzazi wa mpango zinapatikana maeneo mengi kwa urahisi kupitia wauguzi, wakunga na wahudumu wa afya waliopatiwa mafunzo ili kwa yeyote aliyebalehe aweze kupata huduma ya uzazi wa mpango atakapohitaji. Kitu kizuri zaidi, huduma za uzazi wa mpango zinatolewa bure katika kliniki za uzazi wa mpango zilizo karibu nawe.
Baada ya kuona faida lukuki za uzazi wa mpango kupitia gazeti hili mtandao la FikraPevu sasa nakutia moyo kuifuata 'Nyota ya Kijani' yenye maana ya uzazi wa mpango kwa watu wote ikiwemo walio kwenye ndoa na wasio kwenye ndoa, waliokwisha zaa na ambao bado hawajazaa. Jitofautishe, thamini uhai sasa, kwa kupata elimu ya uzazi wa mpango, kuepuka mimba za utotoni kwani huhatarisha maisha yako dada, kuacha utoaji mimba kwa kuwa ni hatari.
Kwa akina Mama ni vyema mkajitofautisha kwa kuweka nafasi katika kila uzazi wako, miaka miwili mitatu au zaidi. Pia jitahidi kufanya hivyo ili afya ya mama na mtoto iwe bora. Jitofautishe kwa kupata elimu yako sasa lakini pia usisahau kuitofautisha kuthamini uhai wako sasa. Fuata uzazi wa mpata uzazi wa mpango ili ubadilishe maisha yako ya kiuchumi pia afya ya mtoto wako pia na mama italuwa bora, watajitofautisha, thamini maisha yako sasa.
 
Top