Anatomy of Obstructive Sleep ApneaAnatomy of Obstructive Sleep ApneaMatibabu haya yameonekana kuwafaidi wagonjwa muda wote siyo usiku tu hadi mchana pia.
TATIZO la kukosa pumzi wakati umelala (Obstructive Sleep Apnoea ‘OSA’) ni hali inayotokea wakati kuta za koo zinapopumzika na kuwa nyembamba, hivyo kushindwa kupitisha pumzi vizuri wakati umelala, FikraPevuinafafanua.
Tatizo hili linaweza kutokea kwa jinsi mbili tofauti: kwanza, ni kukosa pumzi kabisa (apnoea) kwa sekunde 10 au Zaidi, na pili, ni kukosa pumzi kwa asilimia 50 (hypopnoea) kwa sekunde 10 au zaidi.
Watu wenye tatizo hili hushtuka mara kwa mara usiku pale wanapokosa pumzi kabisa.
Pengine mtu anaweza kuhisi anakabwa na watu kishirikina na wengine huita ni ‘jinamizi’. Wenye tatizo hili mara nyingi hukoroma na kutoa mlio wa ajabu kila wanapokoroma. Ni kama gari bovu lilibebeshwa mzigo mzito sana likipanda mlima.
Tatizo hili huathiri wanaume na wanawake, ingawa huathiri sana wanaume. Tatizo linaweza kutokea katika umri wowote, hata hivyo, watu wenye umri kuanzia miaka 30 hadi 60 wako katika hatari zaidi ya kupata tatizo hili bila kujali hali zao za kimaisha.
Nini husababisha kukosa pumzi wakati umelala?
Ni kawaida kwa kuta za koo kusinyaa na kutanuka wakati umelala.
Watu wengi hawapati tatizo la kukosa pumzi ingawa wachache hupata tatizo kutokana na sababu mbalimbali kama kuwa mnene sana, kuwa na shingo pana, kuwa na matatizo ya kimaumbile kama koromeo kubwa, matumizi ya dawa za usingizi, kuvuta sigara au kunywa pombe kabla ya kulala.
Kukosa pumzi wakati umelala kuna uhusiano gani na ugonjwa wa moyo?
Kadiri tafiti mbalimbaili za magonjwa ya moyo zinavyoongezeka kuna ugunduzi mwingi umetokea.
Wataalamu wamegundua uhusiano uliopo kati ya magonjwa ya moyo kama kupanda kwa shinikizo la damu (hypertension), moyo kushindwa (heart failure) na kiharusi (stroke) na kukosa pumzi wakati umelala.
Wataalamu hawana uhakika kama kukosa pumzi vizuri wakati umelala kunaweza kusababisha moja kwa moja ugonjwa wa moyo ila wanadai ikiwa una tatizo hilo sasa kuna uwezekano mkubwa wa kupanda kwa shinikizo lako la damu siku zijazo.
Moja ya changamoto inayofanya kuwa vigumu kuthibitisha moja kwa moja uhusiano uliopo kati ya kukosa pumzi wakati umelala na ugonjwa wa moyo ni kuwepo kwa magonjwa mengine yanayosababisha mtu kukosa pumzi.
Ikiwa utamtibu vizuri mtu mwenye ugonjwa wa moyo kama kupanda kwa shinikizo la damu, tatizo la kukosa pumzi wakati amelala linaweza kupungua au kuisha.
Hii inaweza kuwa sababu nzuri ya kufikiria uhusiano uliopo kati ya ugonjwa wa moyo na kukosa pumzi wakati umelala.
Kwanini shinikizo la damu hupanda unapokosa pumzi wakati umelala?
Shinikizo la damu hupanda pale unapokosa pumzi, kiwango cha hewa safi ya oksijeni hushuka sana kwenye mwili hivyo taarifa hufika kwenye ubongo na ubongo hupeleka ishara kwenye mfumo wa fahamu ili kufanya mishipa ya damu kusinyaa ili kuongeza msukumo wa damu yenye oksijeni kwenye ogani muhimu kwenye mwili ambazo ni moyo na ubongo.
Wakati mwingine shinikizo la damu hupanda wakati wa mchana ambapo mtu hajalala kwa kuwa usiku mwili ulikosa oksijeni ya kutosha na kusababisha mabadiliko mengine katika mwili.
Nini matibabu ya wenye kukosa pumzi wakati wamelala?
Kitu cha msingi katika matibabu ni kubadili mfumo wa maisha unaosababisha upate tatizo, mfano kuacha kuvuta sigara, kuacha kunywa pombe hasa kabla ya kulala, kuwa na uzito unaondena na kimo chako.
Kuna ushahidi mzuri kuhusu kufanikiwa kwa matibabu ya muendelezo chanya wa hewa, kitalaamu hujilikana kama Continuous Positive Airway Pressure (CPAP) therapy.
Matibabu haya yanahusisha kuvaa maski iliyounganishwa na mtungi wa hewa safi ya oksijeni, ambapo humfanya mgonjwa kupata hewa safi wakati wote.
Matibabu mengine yanahusisha kuvaa kifaa maalumu mdomoni (Mandibular Advancement Decive ‘MAD’) ili kutanua njia ya hewa wakati umelala.
 
Top