YOUTH
 UJANA ni kipindi cha mpito kutoka utegemezi wa utoto hadi utu uzima huru na ufahamu wa kutegemeana kwetu kama wanachama wa jumuiya.

Hata hivyo, umri ni njia rahisi ya kufafanua kundi hili, hasa katika uhusiano na elimu na ajira.

Kipindi hiki huanza baada ya kubalehe kufikia utu uzima. Jamii nyingi hukiona kipindi hiki kama kipindi ambacho mtu sio mtoto wala siyo mtu mzima. Hivyo basi, ujana ni kati ya umri wa miaka 15 hadi 24.

Hata hivyo, mkataba wa vijana Afrika unataja ujana kama umri kati ya miaka 15 na 35. Idadi ya watu Tanzania inakadiriwa kufikia watu milioni 50, huku idadi ya vijana ikiwa ni angalau asilimia 35 kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Vijana.

Utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS Tanzania) uliongozwa na Mtakwimu Mkuu, Bi Ruth Minja, umebaini kwamba asilimia 71 ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 35 wanatumia muda wao mwingi kwenye shughuli zisizo za uzalishaji mali mfano kujihudumia kwenye gesti, baa, kulala na katika shughuli za starehe.

Serikali imesema hali hii inaichelewesha Tanzania kuingia katika kundi la mataifa yenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

Kulingana na Utafiti wa Nguvukazi 2014 (2014 Integrated Labour Force Survey) idadi ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni milioni 14.8 ambapo milioni 12.5 sawa na asilimia 84.5 wana uwezo wa kufanya kazi za kiuchumi na milioni 2.3 sawa na asilimia 15.5 hawana uwezo wa kufanya kazi za kiuchumi.

Kati ya hao wenye uwezo wa kufanya kazi za kiuchumi, milioni 11.0 sawa na asilimia 88.3 wameajiriwa na milioni 1.5 sawa na asilimia 11.7 hawajaajiriwa.

Ni Matatizo Gani ya Afya huwepo kipindi cha Ujana?

Majeraha ya Kukusudi na Yasiyo ya Kukusudia

Majeraha ya kukusudia yanatia ndani kujidhuru au kumdhuru mtu na kujinyonga au kumnyonga mtu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) vijana 180 hufa kila siku kutokana na ghasia za ana kwa ana. Asilimia 30 ya vijana wa kike wa umri kati ya miaka 15 na 19 hunyanyaswa na wapenzi wao duniani kote.

Kukuza malezi na mahusiano bora kati ya wazazi na watoto mapema katika maisha, kutoa mafunzo ya stadi za maisha, na kupunguza upatikanaji wa pombe na silaha za moto vinaweza kusaidia kuzuia vurugu.

Majeruhi yasiyo ya kukusudia ndiyo sababu kubwa ya vifo na ulemavu miongoni mwa vijana.

Kulingana na WHO, mwaka 2012, vijana 120,000 walikufa kutokana na ajali za barabarani. Ajali nyingi za barabarani hutokana na matumizi ya pombe na vilevi vingine. Ajali kubwa inapotokea na kusababisha kifo cha kijana mmoja basi kuna wengine 10 wanakuwa na majeraha makubwa hivyo kufanya vilema wa maisha yao yote.

Matatizo ya Uzazi na Kujamiiana

Matatizo ya uzazi na kujamiiana yanatia ndani magonjwa yaenezwayo kwa njia ya kujamiiana kama VVU/UKIMWI, Kaswende na Kisonono.

Ukuaji na maendeleo ya kimwili wakati wa ujana huambatana na ukuaji kingono unaosababisha kuwepo kwa mahusiano ya karibu kati ya jinsia mbili tofauti iwe ni nje au ndani ya ndoa.

Matokeo ya ngono zembe kipindi cha ujana ni pamoja na mimba zisizohitajika, magonjwa ya zinaa pamoja na VVU.

Inakadiriwa 30% ya watu milioni 40 (sawa na watu milioni 10.3) wanaoishi na VVU na UKIMWI ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-24, na nusu ya maambukizi mapya zaidi ya 7,000 hutokea kila siku miongoni mwa vijana.

Idadi kubwa ya vijana hawajui hali zao za maambukizi ingawa bado wanashiriki vitendo vya ngono.

Vijana wanapaswa kujua jinsi ya kujikinga na kuwa na njia ya kufanya hivyo. Hii ni pamoja na kuwa na uwezo wa kupata kondomu ili kuzuia maambukizi ya ngono ya virusi na sindano safi kwa wale wanaojidunga dawa za kulevya.

Upatikanaji bora wa vituo vya kupima VVU na ushauri nasaha, na wale watakaonekana kuwa na maambukizi ya VVU wapate tiba zinazohitajika.

Mimba na kuzaa utotoni ni hatari kwa vijana wa kike. Inakadiriwa asilimia 20 ya vijana wa kike kati ya umri wa miaka 15 na 19, tayari wameshazaa.

Vijana wa kike wanapokuwa na mimba za mapema wanakuwa katika hatari ya matatizo kipindi cha ujauzito na kipindi cha kujifungua. Hatari ya maradhi na vifo ni kubwa kwa watoto wachanga waliozaliwa na mama vijana kuliko kwa watoto wachanga waliozaliwa na wanawake wenye umri mkubwa.

Ukosefu wa habari na ujuzi, upatikanaji duni wa mbinu za kuzuia mimba, ikiwa ni pamoja kondomu, na mazingira magumu kwa kulazimishwa ngono vinaweka vijana katika hatari kubwa ya mimba zisizotakiwa na maambukizi.

Matumizi ya Pombe, Tumbaku na Madawa ya Kulevya

Madhara ya kunywa pombe miongoni mwa vijana ni tatizo kubwa katika nchi nyingi. Pombe hupunguza uwezo wa kujitawala na kuongezeka kwa tabia hatarishi, kama vile ngono zisizo salama au kuendesha gari bila tahadhari.

Ni sababu ya msingi ya majeruhi pamoja na ajali za barabarani, vurugu (hasa kwa mpenzi) na vifo vya mapema. Pia inaweza kusababisha matatizo ya afya katika maisha ya baadaye na kuathiri umri wa kuishi.

Matumizi mabaya ya tumbaku na vitu haramu huongeza hatari ya saratani, magonjwa ya moyo, na magonjwa ya kupumua baadaye katika maisha.

Watu wengi wanaovuta sigara wameanza kutumia walipokuwa vijana na baada ya kutimiza miaka 18 waliendelea kuvuta kwa ukawaida.

Utafiti uliofanywa na WHO unadai kwamba vijana wanaoanza mapema kutumia vilevi mbalimbali basi wanaanza mapema pia vitendo vya ngono.

Magonjwa ya Afya ya Akili

Vijana wapo katika hatari kubwa ya kupata mikazo inayotokana na changamoto mbalimbali za kimaisha katika makuzi yao vitu vinavyopelekea kupatwa na magonjwa ya akili.

Matatizo ya mhemko kama vile huzuni, na matatizo ya akili kama vile dhiki, ni aina mbili za magonjwa ya akili ambayo hugundulika mapema katika ujana na huhitaji muda mrefu kupona.

Huzuni ni sababu kuu ya kuugua na kulemaa miongoni mwa vijana na kujiua ni sababu kuu ya tatu ya vifo vya vijana.

Vurugu, umaskini, udhalilishaji na hisia za kutojipenda vinaweza kuongeza hatari ya kupatwa na matatizo ya akili.

Kujenga stadi za maisha kwa watoto na vijana na kuwapatia msaada wa kisaikolojia katika shule na mazingira mengine ya jamii inaweza kusaidia kukuza na kuboresha afya ya akili.

Matatizo ya Lishe

Ujana ni kipindi muhimu kushughulikia matatizo ya lishe ambayo yanaweza kuwa yameanza utotoni/mapema katika maisha, pia kushughulikia yale yanayoanza wakati wa ujana.

Utapiamlo unatajwa kusababisha asilimia 16 ya ulemavu katika maisha ya watu wote, vilevile ikiwa ni sababu kuu ya afya mbovu.

Wavulana na wasichana katika nchi zinazoendelea wengi huingia ujana wakiwa na utapiamlo, hivyo kuwaweka katika hatari zaidi ya ugonjwa na kifo mapema. Idadi ya vijana wenye uzito uliozidi imeongezeka katika nchi zote zenye kipato cha chini na kipato cha juu.

Magonjwa Sugu

Kusimamia masharti ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile pumu, kifafa, cystic adilifu, ugonjwa wa kisukari cha vijana na ugonjwa wa seli mundu kwa vijana ni changamoto kutokana na sababu kama vile kuongezeka uhuru, shinikizo la rika na tabia ya vijana kujitokeza utambulisho.

Usimamizi wa maradhi haya unahitaji huduma za kina na msaada wa masuala yote ya matibabu na kisaikolojia kwa namna endelevu.
 
Top