embryoWAKATI baadhi ya wanawake wakililia kupata walau mtoto mmoja, wapo wanaoamua kukatisha uhai wa viumbe hivyo vikiwa vingali tumboni kwa kuharibu mimba.

Utafiti uliofanywa hapa nchini mwaka 2013 na Taasisi ya Guttmacher ya Marekani kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ya hapa nchini pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), ulionyesha kuwa ndani ya miezi kumi na mbili pekee kwa mwaka huo, mimba 405,000 zilitolewa, kiwango ambacho ni kikubwa sana.

Utafiti huo umeonyesha kuwa, kwa kila wanawake 1,000 wenye mimba, wastani wa mimba 36 hutolewa kinyume na sheria za nchi.

Mwanzoni mwa mwaka 2012, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilitoa takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), zikionyesha kuwa kiwango cha utoaji mimba duniani kimebakia kuwa asilimia 28 kwa kila wanawake 1,000.


Pia uwiano wa kiwango cha mimba zinazotolewa bila utaalamu kimepanda kutoka 44% mwaka 1995 hadi 49% mwaka 2008, shughuli hizi uambatana na Utoaji mimba usio salama unaochangia kwa kiasi kikubwa vifo vya uzazi duniani, kwani unafanyika nje ya taratibu za hospitali, kliniki na upasuaji, au bila kuwa na wataalamu wa kitabibu wenye sifa.

Zifuatazo ni baadhi ya Takwimu zilizobainishwa katika utafiti huo kutoka (WHO)

Katika nchi zinazoendelea hasa zile zenye sheria kali za utoaji mimba, utoaji mwingi unaofanyika si salama huku 97% zinatolewa kwa njia hiyo Afrika.

Profesa Beverly Winikoff kutoka Gynuity, taasisi iliyoko New York inayohamasisha utoaji mimba salama aliandika katika jarida hilo la Lancet: "Utoaji mimba usio salama ni moja kati ya sababu kuu tano zinazochangia vifo vya uzazi na kusababisha kifo kimoja katika kila vifo vya uzazi saba au nane mwaka 2008.”

Utafiti huo unaonyesha kuwa mwaka 2008, 86% ya utoaji mimba ulitokea katika nchi zinazoendelea na karibu nusu ya hizo hazikuwa salama.

Taarifa hizo zinaendelea kuthibitisha kile kinachofahamika kwa miongo mingi kuwa wanawake wanaotaka kutoa mimba wasizozitaka wanatafuta utoaji kwa gharama yoyote hata kama ni kinyume cha sheria au inahatarisha maisha yao maana wanawake wanaendelea kufa kwa idadi kubwa kwa sababu ya utoaji mimba usio salama.

Msichana wa chuo Kikuu cha Tanzania Institute of Accountancy (TIA) cha jijini Dar es Salaam, Sarah Joshua, yeye anasema kichocheo kikuu cha utoaji wa mimba kwa wasichana na wanawake wengi wa siku hizi ni kutokana na uwazi unaotolewa wa elimu ya uzazi.

“Kinadada hasa wakipewa elimu hii na kuielewa vizuri huchukulia kupata mimba na kutoa mimba ni jambo la kawaida, maana wengine wanaweza hata kusingizia kuwa wamepata matatizo yatokanayo na mimba, mradi tu waweze kutoa, kwani wengi wao wanaonekana wanapata huduma hiyo katika vituo vya afya,” anaelezea Sarah.

Anaendelea kwa kusema kwamba, wahusika hujipa moyo pia kwa kuwaza kuwa, watapatiwa huduma ya kiafya kutoka vituo vya afya pindi mambo yakienda vibaya kwa kuleta madhara wakati wa kutekeleza tendo hilo.

Wakati sheria na elimu ya uzazi vikitajwa kuwa kinara cha uchochezi, Fikra Pevu imewahi kuandika sababu zingine za utoaji mimba na madhara yake, pia wachangiaji wa mtandao wa kijamii wa Jamii Forums nao wanatoa maoni tofauti kuhusiana na suala hilo.

Sheria ya nchi inaeleza kuwa kumpatia msichana au mwanafunzi mimba mwanaume anapaswa kufungwa kwa miaka 3o jela, hali hii inawafanya wawili hawa kuelewana na kuwa na hatima ya kutoa ujauzito mapema kabla ya kujulikana.

Masomo, kupata mimba katika umri mdogo, kupata mimba nje ya ndoa, kutokuwa tayari kulea mtoto, kuficha watu wasijue kuwa amewahi kufanya ngono, shinikizo kutoka kwa wanaume au kutotaka kuzaa mtoto kutokana na mimba iliyotungwa kwa kubakwa ni sababu nyingine ambazo zinachangia utoaji wa mimba.

Aidha, Elimu za afya zinazotolewa katika jamii, kwa akina mama wanapohudhuria hospitali kupatiwa huduma za afya, wasichana wakiwa shuleni, akina baba wanapoambatana na wake zao kwenda kupata ushauri kiafya, njia hizi huwaleta karibu na kupata upeo wa kuona jambo la utoaji mimba ni la kawaida kutokana na uelewa.

Watoto wa kike waliochini ya miaka 18 hutoa mimba kwa kuogopa kufukuzwa shule, kufuata ushauri wa marika, hofu ya kuvunja uhusiano na wapenzi wao, ukali wa wazazi na sababu za kidini.

Watoto wa kike kushindwa kuutunza ujauzito na mtoto atakayezaliwa kwa maana vijana wengi hawana ajira na kuendelea kuwa na ujauzito kunaweza kusababisha wazazi kumsusa msichana huyo na kuacha kumhudumia.

Sababu nyingine inayotajwa ni athari za kijamii, ambapo msichana anaweza kutengwa na marafiki, familia na jamii kiujumla lakini pia kuna athari za kiuchumi kutokana na maradhi. Ikiwa msichana atapata matatizo makubwa fedha nyingi zitahitajika kugharamia matibabu yake na kupunguza fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye elimu yake na mambo mengine.

Watu wengi wanasema kuwa, licha ya kuwepo kwa elimu ya afya ya uzazi iliyoonekana kuwa kichocheo cha utoaji mimba kutokana na baadhi ya mafundisho, pia sheria kwa kufungwa wanaowapa mimba wasichana walioko masomoni au chini ya umri wa miaka 18 kwa baadhi ya nchi tukiwemo Tanzania, pia imetajwa sana kuwa chanzo cha kutoa mimba kwa wanawake wengi wa leo.

Baadhi ya tamaduni haziruhusu mtoto kuzaliwa kabla ya kuolewa, hivyo msichana akipata mimba hana chaguo lingine zaidi ya kutoa mimba. Hofu ya kutengwa na familia na jamii kiujumla humfanya msichana kutoa mimba.

Kama takwimu zulivyoonesha kuwa kwa wanawake wengi utoaji wa mimba wanaoutumia ni nje ya sheria na taratibu, hivyo njia za kienyeji uweza kupelekea muhusika kupatwa na magonjwa hasa maambukizi ya bakteria na kutokwa na damu sana hadi kifo.
 
Top