Watu wengi tumekuwa tukitumia chumvi kama moja ya kiungo muhimu katika chakula na chenye kuongeza ladha ya chakula, lakini kiuongo hiki ambacho pia hufahamika kama ‘Mkuu wa Jikoni’ kinaweza kuwa na madhara ya kiafya pale ambapo kitatumika kupita kiasi. 
Kwa kawaida mwili wa binadamu huihitaji kiwango fulani cha chumvi, lakini shida ni pale ambapo mtumiaji atatumia chumvi nyingi kuliko kiwango ambacho mwili unahitaji. 
Kuna baadhi ya magonjwa ambayo yamebainika kuchangiwa na matumizi ya chumvi kupita moja ya magonjwa hayo ni pamoja na matatizo ya shinikizo la damu, jambo ambalo huweza kusababisha mtu kupata matatizo ya shambulio la moyo pamoja na hatari nyingine za magonjwa ya moyo, na ndio maana mara nyingi hushauriwa matumizi ya chumvi kwa kiwango cha chini ili kuepukana na matatizo kama haya.
 
Kutokana na madhara hayo ni vizuri sasa ukaanza kuepuka matumizi ya chumvi kwa kupunguza kiwango cha matumizi yako ya chumvi, na endapo unapenda kufanya mabadiliko haya basi ni vizuri ukaanza nayo taratibu.
 
Anza kwa kupenda kujiaminisha na kuhisi kuwa chakula kina ladha hata pale ambapo chumvi haijakolea, lakini kama huwa una kawaida ya kuongeza chumvi nyingi mezani, basi ni vyema ukaanza kwa kuondoa kile kikopo kidogo cha chumvi mezani wakati wote na hasa wakati wa chakula.


Mbali na hayo, pia jaribu kuwasihi watu wanaopika au wewe mwenyewe unapopika kupunguza kiwango cha chumvi unachoongeza wakati wa mapishi yako, onja wakati ukiwa unapika ili kuepuka kiwango kingi cha chumvi ambacho kinaweza kuwa hatari kwa afya yako.

Hata hivyo, kuna viungo vingine ambavyo huweza kutumika kama mbadala wa chumvi na havina madhara kwa binadamu, viungo hivyo ni pamoja na limao pamoja na ndimu, huku kiungo kingine kinachoweza kuchukua nafasi ya chumvi kwenye chakula chako ni mdalasini.
 
Top