idadiIDADI ya watu duniani inakadiriwa kuwa bilioni 7, kutoka bilioni 2.5 mnamo mwaka 1950. Ukuaji wa haraka wa idadi ya watu umeathiri usambaaji wa magonjwa kwa njia zifuatazo:

1. Msongamano na ukuaji wa mji. Magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu husambaa haraka zaidi kwa watu wanaoishi kwa kukaribiana sana. Hadi sasa angalau 50% ya watu duniani kote wanaishi maeneo ya mijini, ambapo idadi kubwa ya watu wanaishi sehemu zilizosongamana kitu kinachosababisha idadi kubwa ya watu kukutana na kurahisisha kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza.

Kipindupindu ni ugonjwa wa kuhara unasababishwa na kumeza chakula au maji machafu yenye bakteria aina ya Vibrio cholerae. Watafiti wanakadiria kuwa kila mwaka kuna matukio takriban milioni 1.4 hadi milioni 4.3, na vifo 28,000 hadi 142,000 duniani kote. Kipindupindu ni ugonjwa hatari sana, huathiri watoto na watu wazima na unaweza kuua ndani ya masaa machache tu usipopata matibabu.

FikraPevu inatambua kwamba, ufumbuzi wa muda mrefu kwa ajili ya kudhibiti kipindupindu, ambao unaweza kuleta faida kwenye kudhibiti magonjwa yote mengine yanayoenea kwa njia ya kinyesi unategemea maendeleo ya kiuchumi na upatikanaji wa maji safi ya kunywa na usafi wa mazingira, ambayo ni muhimu katika kuzuia mlipuko wa kipindupindu.


2. Uhamiaji na kusafiri. Jinsi ilivyo vyepesi kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine ndivyo inavyorahisisha magonjwa kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Mlipuko wa magonjwa kama Ebola unaweza kusambaa eneo jingine ikiwa watu walioathirika na ugonjwa huo watasafiri eneo jingine.

3. Uharibifu wa mazingira. Changamoto za mazingira kama kubadilika kwa hali ya hewa, inaweza kusababisha kusambaa kwa magonjwa hasa yale yanayoenezwa na wadudu kama mbu, mfano Virusi vya Magharibi ya Nile huenezwa na mbu, ikiwa hali ya hewa itabadilika basi mbu hao huhama na kwenda maeneo yatayowafanya waishi vizuri na wakifika huko huendelea kusambaza virusi/ugonjwa waliotoka nao sehemu ya kwanza. Vile vile ongezeko la joto ulimwenguni hufanya wadudu wanaobeba magonjwa kustawi.

Tabia za wanadamu zinafanya baadhi ya magonjwa yaendelee kuwepo na kutokeza mengine.

Kwa mfano, wanasayansi wanaamini kwamba kwa sababu ya wanadamu kuharibu mazingira, magonjwa mapya na yaliyo hatari yametokea. Alipohojiwa katika gazeti Newsweek, Mary Pearl, msimamizi wa shirika la Wildlife Trust alieleza hivi: “Tangu miaka ya katikati ya 1970 zaidi ya magonjwa 30 mapya yameibuka, yakiwemo Ukimwi, Ebola, ugonjwa wa Lyme, na Mafua ya Ndege (SARS). Inaaminika kwamba wanadamu waliambukizwa mengi ya magonjwa hayo kutoka kwa wanyama.”

Kwenye mataifa yanayoendelea, ambapo ongezeko kubwa la watu hutarajiwa kutokea, kuna mahangaiko mengi ya kukidhi mahitaji, huku miundombinu ya afya ya umma ikiwa haijajengwa vizuri kuendana na idadi ya watu, hufanya hata usambazaji wa chakula kuwa katika hali ya hatari.

Idadi kubwa ya watu wanaoishi katika miji ya nchi zinazoendelea inaathiriwa na uchafuzi wa hali ya hewa. Takwimu za hivi karibuni zinadai kwamba 98% ya majiji katika nchi zenye uchumi wa chini na kati, yenye wakazi zaidi ya 100,000 haikidhi mapendekezo ya WHO kuhusu ubora wa hewa. Hata hivyo, kwenye nchi zilizoendelea asilimia hiyo hupungua hadi 56.

Jinsi ubora wa hewa unavyopungua, ndivyo hatari za magonjwa kama kiharusi (stroke), ugonjwa wa moyo, saratani ya mapafu; na magonjwa ya papo hapo na sugu ya njia ya hewa ukiwemo pumu, inavyoongezeka kwa watu wanaoishi mazingara hayo.

“Uchafuzi wa hali ya hewa ndio chanzo kikuu cha magonjwa na vifo. Ni habari njema kwamba majiji mengi zaidi yanapiga hatua kufuatilia ubora wa hewa na kuchukua hatua za kuboresha hivyo ni jitihada za kuigwa.” anasema Dk. Flavia Bustreo, msaidizi wa mkurugenzi mkuu wa kitengo cha afya ya familia, wanawake na watoto katika WHO.

Kila mwaka, vifo milioni 4.3 hutokea kutokana na matatizo yatokanayo na uchafuzi wa hewa ya ndani na vifo milioni 3.7 hutokana na uchafuzi wa hewa ya nje.

Tunapovuta hewa chafu kuna vipande vidogo vidogo huingia kwenye mapafu na kusababisha muwasho kwenye mapafu na hudhuru moyo na huweza kusababisha ugonjwa wa moyo na kupanda kwa shinikizo la damu.

Msongamano mkubwa wa watu unaosababisha watu kugusana unaweza kusababisha kuenea kwa magonjwa ya ngozi yanayoambukizwa kwa kugusana. Ikiwa msongamano wa watu utazuia kwa muda waendesha vyombo vya moto kama magari basi madereva hao wanaweza patwa na msongo wa mawazo na hasira kwa kucheleweshwa vitu vinavyoweza kuathiri akili moja kwa moja.

Idadi ya watu inavyozidi kukua husababisha kuongezeka kwa mahitaji ya chakula, ili kukabiliana na tatizo hili kilimo cha mashamba makubwa kinapendekezwa, kilimo hiki kinaweza kurahisisha kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kama surua, kimeta, kifua kikuu na homa ya uti wa mgongo.

Surua ni ugonjwa hatari sana unaombukizwa kwa njia ya hewa unaosababishwa na virusi. Ni rahisi sana kuambukizwa ugonjwa wa surua ambao huwaua watoto wengi. Kila mwaka watu milioni 30 hupatwa na surua. Kinachoshangaza, ni miaka 40 sasa imepita tangu chanjo ya ugonjwa huo ianzwe kutolewa.

Kimeta ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria ya spora. Ingawa si rahisi kuambukizwa ugonjwa wa kimeta kutoka kwa mtu mwingine, ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya hewa. Dalili za mapema za ugonjwa wa kimeta zinafanana na zile za mafua. Baada ya siku kadhaa, mgonjwa hushindwa kupumua na hushikwa na mshtuko. Mara nyingi aina hiyo ya kimeta huua.

Kifua kikuu ni ugongwa unaosababishwa bakteria viitwavyo Mycobacterium tuberculosis. Ugonjwa wa kifua kikuu unaenezwa kwa njia ya hewa kutoka katika mtu ambaye anaugua na hajaanza matibabu, mtu huyu akipiga chafya, kukohoa au kutema makohozi ovyo anaweza kuambukiza watu wengine.

Watu walio katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo wanaweza kujizuia kwa kutumia viuavijasumu. Ni muhimu mgonjwa atibiwe mapema; kuchelewa hupunguza uwezekano wa kupona.
Homa ya uti wa mgongo ni maambukizi yanayosababisha uvimbe wa meninji, kifuniko cha ubongo na uti wa mgongo. Mara nyingi husababishwa na maambukizi ya bakteria, virusi, au fangasi lakini pia uvimbe unaweza kusababishwa na kemikali kuwasha utando wa ubongo na uti wa mgongo, araknoida ndogo kutokwa na damu, kansa na hali nyingine.

Homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na bakteria aina ya Meningococcus (Meningitidis Neisseria) ndio homa ya uti wa mgongo inayowapata watu wengi zaidi na huenea mtu kwa mtu kwa njia ya matone ya pumzi ya mtu aliyeambukizwa anapopumua karibu yako. Asilimia 50 za wagonjwa hupoteza maisha ikiwa hawataanzishiwa matibabu mapema iwezekanavyo.

Bakteria husambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya matone ya pumzi au koo kutoka kwa mtu aliye na maambukizi. Kukaa kwa muda mrefu na mwenye ugonjwa, kubusiana,

Kupiga chafya au kukohoa juu ya mtu au kuishi nyumba zilizobanana (kama vile mabweni, kuchangia vyombo vya vyakula na mtu aliyeambukizwa huwezesha kuenea kwa ugonjwa.

Dalili kuu za ugonjwa huu ni homa kali, degedege, kukamaa kwa shingo, kichwa kuuma, kutapika na kutopenda mwanga. Homa ya uti wa mgongo huathiri mfumo wa fahamu kama vile kutosikia vizuri, upofu, mtindio wa ubongo na huweza kusababisha kifo.
 
Top