Mara nyingi hali hii huisha yenyewe bila kuhitaji matibabu, ingawa mara chache inaweza kuwa ya kuhatarisha maisha kiasi cha kuhitaji matibabu ya haraka.
Damu inaweza kutoka sehemu ya mbele au nyuma ya ndani ya pua. Mara nyingi damu hutokana sehemu ya mbele ya ndani ya kuta za pua (anterior nose bleeding).
Sababu
Kutokwa damu puani ni dalili inayoweza kusababishwa na magonjwa au hali mbalimbali zifuatazo :
- Kuingiza vidole puani
- Kupiga chafya au kupenga mafua kwa nguvu sana
- Shinikizo la damu la kupanda
- Saratani ya damu
- Matatizo ya damu kushindwa kuganda
- Kuumia puani kwa kujigonga, au kuvunjika mfupa wa pua
- Kutumia dawa za kuzuia damu kuganda kama aspirin, clopidogrel na warfarin.
- Saratani ya pua
- Magonjwa ya ini au figo
- Maambukizi ya bakteria au virusi kwenye pua
- Matumizi ya madawa ya kuvuta puani
- Kukauka kwa kuta za ndani za pua
Namna Inavyotokea
Kutokwa na damu puani hutokea hasa kwa watoto wa umri wa miaka 2-10 na watu wazima wenye umri wa miaka 50-80.
Hali hii hutokea ghafla damu ikianza kutoka puani polepole. Inaweza ikatoka kwenye tundu moja la pua au yote mawili. Wakati mwingine damu inaweza kutoka baada ya kutembea kwenye jua kali au kufanya mazoezi.
Damu inaweza kutoka wakati wa usiku ukiwa umelala na ukaimeza, kisha ikaonekana kwa kutapika damu au mabonge ya damu, au kupata choo chenye damu damu au cheusi sana.
Nini cha Kufanya
Mara nyingi kutokwa damu puani huacha baada ya muda mfupi bila kuhitaji matibabu. Unapotokwa damu puani fanya yafuatayo;
- Tulia, usihangaike hangaike.
- Inua kichwa chako kiwe juu ya usawa wa moyo
- Inamisha kichwa chako kuelekea mbele kidogo kuzuia kumeza damu
- Minya sehemu laini ya pua kwa vidole vyako kwa dakika 10 mpaka 15.
Unaweza ukatumia dawa za kupuliza puani ili kusimamisha damu isitoke.
Ikiwa damu inaendelea kutoka licha ya kuibana pua kwa dakika 15 au kupulizia dawa ya kuzuia damu kutoka, unatapika damu au kama hali hii inajirudia mara kwa mara basi onana na daktari haraka iwezekanavyo.
Matibabu ya hospitali hujumuisha;
Kuziba mshipa wa damu uliopasuka kwa umeme
Kuweka pamba zenye kemikali za kuzuia damu kutoka ndani ya pua. Hizi hukandamiza mishipa ya damu na kuzuia damu kuvuja. Hukaa kwa siku 1 mpaka 3 kabla ya kuondolewa.