kumbuka kwamba vyakula vyote vinaweza kuwa ni muhimu mwilini lakini huzidiana kulingana na mahitaji na hali ya mtu kwa wakati maalumu.
Mahitaji ya madini na vitamini mwilini wakati wa ujauzito huwa ni makubwa, hususani madini ya kashiamu, chuma na Vitamin B9 (folic acid).
MADINI YA KALISI (Calcium)
Wakati wa ujauzito, madini mengi ya kalisi husafirishwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa ajili ya kuimarisha mifupa na meno. Katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo, mama huhifadhi madini hayo mwilini mwake. Kiumbe kinapokamilisha umbo lake katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho, hifadhi hiyo huanza kutumiwa na kiumbe hicho, hivyo mahitaji yake kuongezeka.
Katika kipindi hiki, mjamzito anatakiwa kula kwa wingi vyakula vinavyoongeza madini ya kalisi kama vile maziwa na vyakula vitokanavyo na maziwa. Kukiwa na upungufu wa madini hayo, meno ya mama na mifupa huathirika pia.
MADINI YA CHUMA (Iron)
Mahitaji ya madini ya chuma nayo huwa makubwa kwa wajawazito. Madini hayo ni muhimu kwa utengenezaji wa damu ambayo huhitajika kwa wingi na mama pamoja na mtoto.
Madini joto hupatikana kwa kula kwa wingi vyakula kama vile nyama, samaki, mayai, vyakula vilivyopikwa kwa nafaka zisizokobolewa (ugali wa dona, mkate mweusi, n.k) na mboga za majani kama vile spinachi na brokoli. Ili kupata madini hayo ya kutosha kutokana na vyakula hivyo, inashauriwa mjamzito kutumia pia vidonge vya Vitamin C (Vitamin C food supplements).
VITAMIN B9 (Folic Acid)
Vitamini hii ni muhimu sana kwa mjamzito, ni kosa kubwa sana la kiafya kwa mjamzito kuwa na upungufu wa vitamin hii. Vitamin B9 ndiyo inayohusika na ukuzaji na uimarishaji wa mfumo wa fahamu wa kiumbe tumboni.
Aidha, Vitamin hii ndiyo inayotoa kinga ili viungo vya mtoto visiathirike na kuepusha uzaaji wa watoto walemavu au wenye kasoro za viungo kama ‘midomo ya sungura’ na kadhalika.
Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamin B9 ni pamoja na mboga za majani, juisi ya machungwa, mapeasi, vyakula vilivyopikwa kwa ngano na mchele (hasa brown rice) na mayai.
Hata hivyo, kutokana na hali ya vyakula vyetu, mjamzito hawezi kupata kiwango kinachotakiwa cha vitamin hiyo kwa kula vyakula peke yake.
Ili kupata kiwango cha vitamin hiyo kinachotakiwa, mjamzito atatakiwa kutumia pamoja na vidonge vya lishe vya Vitamin B9 ili kuepuka upungufu huo. Inashauriwa kutumia vidonge hivyo miezi michache kabla ya kushika mimba na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, kipindi ambacho vitamin hiyo huhitajika kwa wingi.
Kwa ujumla, lishe bora ni muhimu kwa mjamzito katika kipindi chote cha ujauzito wake. Matatizo mengi ya kuzaa watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali, hutokana na upungufu wa madini na vitamin muhimu mwilini katika kipindi cha ujauzito.