shambulio la moyo/Heart attack
SHAMBULIZI LA MOYO NI NINI
Shambulizi la moyo au kwa kiingereza heart attack au kwa kitaalam myocardial infarction ni matokeo yatokanayo na ukosefu wa ghafla wa damu kwenye misuli ya kwenye moyo hali ambayo husababisha uharibifu wa kudumu wa misuli hiyo ya moyo.

SABABU
Damu hufanya kazi ya kusafirisha virutubisho kutoka kwenye mfumo wa mmeng`enyo, hewa safi kutoka kwenye mapafu pamoja na vitu vingine kama homoni mbali mbali na kuvipeleka kwenye chembehai zote mwilini. Kutoka kwenye chembehai hizo damu huchukua hewa chafu na uchafu mwingine na kuupeleka kwenye maeneo ambako uchafu huo hutolewa nje ya mwili.

Kama ilivyo kwa kila kitu mwilini moyo nao ni mkusanyiko wa chembe hai zilizotengeneza msuli unaoitwa moyo. Na kama ilivyo kwa chembehai zote mwilini, chembehai ziliounda moyo nazo huhitaji virutubisho na hewa safi wakati wote. Kwa maana nyingine ni kuwa moyo nao kama msuli huhitaji kujisambazia damu ili uweze kufanya kazi.
 

Mshipa wa damu ambao hufanya kazi ya kusambaza damu kwenda kwenye moyo wenyewe huitwa mshipa wa coronary. Inapotokea mshipa huu ukawa na hitilafu yoyote itakayopelekea damu kushindwa kufika kwenye chembehai zote za moyo madhara hutokea kwenye chembehai hizo za moyo.

Madhara yatokanayo na chembehai za moyo kukosa hewa safi na chakula ni kuumia kwa chembehai hizo na kushindwa kwa sehemu husika ya moyo kufanya kazi yake kama kawaida.
 

Soma:Zijue faida za kula samaki
 

MATATIZO YANAYOWEZA KUTOKEA KWENYE MISHIPA INAYOPELEKA DAMU KWENYE MOYO
Matatizo yanayoweza kusababisha mshipa wa damu wa coronary kushindwa kufikisha damu kwenye chembehai zote za moyo ni kama vile;mshipa wa damu umeziba

Kupungua upenyo wa ndani wa mshipa huo kutokana na kujaa kwa lehemu (cholesterol), kuvimba kwa kuta za ndani za mshipa huo, au kujaa kwa madini chumvi ya calcium.
   
Damu kuganda na kutengeneza mabonge kwenye maeneo yenye upenyo mdogo Kubana kwa mshipa kutokana na hitilafu kwenye mfumo wa fahamu na mshipa wa fahamu unaoratibu utendaji kazi wa mshipa huo wa damu.
 

Sababu yoyote kati ya nilizotaja hapo juu hupelekea kushindwa kabisa  kupita au kupita kwa kiasi kidogo tu cha damu kwenye mishipa hiyo na kufika kwenye eneo ambalo ilikusudia kwenda. Kukosekana kwa damu kwenye maeneo mbali mbali ya moyo hupelekea chembehai za eneo hilo kukosa hewa safi na virutubisho hali ambayo husababisha athari za kuhatarisha uhai wa chembehaihizo.

Madhara haya hutokea kwa chembehai nyingi za eneo moja la moyo na hivyo kupelekea eneo kubwa la moyo kuwa limeathirika.

Shambulizi la moyoKama ilivyokua kwenye ngozi, majeraha yanayotokea kutokana na madhara ya kwenye chembehai za moyo huchukua muda kupona. Inakadiriwa kuwa eneo la moyo lililoathirika huhitaji miezi nane kuweza kupona na kurudi kwenye hali yake ya kawaida. Chembehai hizo zilizodhurika kwa pamoja hupona na kuacha kovu kwenye eneo la moyo lililoathirika.

 MADHARA YA TATIZO
Madhara ya tatizo hutegemea ukubwa wa eneo la moyo lililoathirika pamoja na urefu wa muda eneo hilo lilikosa hewa safi aina ya oksijeni.

Madhara huwa ni makubwa zaidi kama mshipa wa damu umeziba kabisa ukilinganisha na kama ni kiasi kidogo tu cha damu kinachopita kwenye mshipa wa damu na kufika kwenye maeneo yote ya moyo.

Eneo lililoathirika hupona na kuacha kovu ambalo huvuruga utaratibu wa kawaida wa ufanyaji kazi wa moyo. Kutokana na uwepo wa kovu moyo hupunguza uwezo wake wa kufanya kazi ya kusukuma damu kupeleka kwenye sehemu mbali mbali za mwili. Uwezo wa moyo kufanya kazi hupungua kulingana na ukubwa wa eneo la moyo lililoathirika na kuachwa na kovu au makovu.

Kama eneo la moyo lililoathirika ni kubwa sana basi moyo hushindwa kabisa kufanya kazi hali ambayo hupelekea muathirika kupoteza maisha kutokana na damu kushindwa kusukumwa kwenda kwenye chembehai za ogani muhimu kwa maisha kama vile ubongo.
 

Soma:Mambo ya kuzingatia uwe baba bora kwa familia na jamii nzima 

DALILI ZA TATIZO

dalili za attack

  •     dalili za shambulizi la moyoKupata maumivu makali ya ghafla kwenye kifua, mkono au chini kidogo ya titi
  •     Kuhisi kama maumivu yanatembea kutoka kifuani kuelekea kwenye mgongo, taya au mkono
  •     Kuhisi kama umeshiba sana au kama unapaliwa
  •     Kupata kiungulia
  •     Kutoka jasho sana ghafla, kusikia kichefuchefu au kutapika.
  •     Kusikia kizunguzungu
  •     Mwili kuwa dhaifu ghafla
  •     Kushindwa kupumua vizuri
  •     Kuwa na wasiwasi sana
  •     Kusikia mapigo ya moyo ambayo hayaendi vizuri (yaani moyo kudunda bila mtiririko wa kawaida)

Maumivu ya shambulizi la moyo huwa yanadumu kwa takribani dakika 25 mpaka nusu saa bila kuacha hata kama umepata tiba za kawaida za kutibu maradhi ya shinikizo la juu la damu. Maumivu haya huendelea hata ukiamua kupumzika.

Watu wengi wenye maradhi ya kisukari pamoja na wengine wachache wasio na kisukari hupata shambulizi la moyo ambalo halina maumivu wala dalili zozote.

TATIZO HUGUNDULIKA VIPI
Baada ya kupata dalili nilizoorodhesha awali inashauriwa kwenda hospitalini haraka kwa kuwa mafanikio ya tiba hutegemea ni muda gani umepita tangu tatizo lilipoanza mpaka tiba ilipopatikana.

Ukifika hospitali daktari atasikiliza historia ya tatizo na kufanya vipimo muhimu ambavyo vitahakikisha uwepo wa tatizo la shambulizi la moyo.

MATIBABU
Baada ya kumuona daktari na vipimo kufanyika matibabu huanzishwa haraka. Kwa matokeo mazuri inatakiwa matibabu yaanze katika kipindi cha masaa mawili tangu dalili zilipoanza. Kadiri muda unavyopita ndivyo madhara ya kudumu yanavyoweza kutokea kwenye eneo kubwa zaidi la moyo.

Lengo kuu la matibabu ni kuzuia madhara zaidi yasiendelee kutokea kwa kuhakikisha mishipa ya damu inafanya kazi vizuri kabisa na kufikisha damu kwenye chembehai zote za moyo.

Matibabu haya huhusisha dawa pamoja upasuaji kama hospitali inauwezo wa kuufanya upasuaji huo.

Matibabu hayo pia hulenga kuzuia matukio mengine ya shambulizi la moyo yanayoweza kutokea baadae.


Soma:Zijue faida za maganda ya ndizi kwa afya yako

KINGA
health checkTatizo hili mara zote huwa ni la dharura na kwa wengi wetu kutokana na miundombinu ya nchi yetu huwa ni vigumu kupata matibabu kwa wakati. Hii husababisha madhara makubwa kwa wengi wetu vikiwemo vifo.

Kwa maneno mengine inapokuja kwenye tatizo hili kinga ni bora kuliko tiba. Namna pekee ya kuhakikisha unaepuka tatizo hili ni kwa kuhakikisha unaishi maisha yanayowezesha mwili kuwa na afya bora kama vile kula mlo kamili, kupunguza vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta na wanga, kufanya mazoezi na kuhakikisha uzito wa mwili siku zote unakua kwenye uwiano unaotakiwa na urefu wako.

Tusisahau kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa miili yetu na mfumo wa damu hauna matatizo yoyoEditable vector background with space for your text - heart andte ya kiafya.

Kwa wale ambao wamepata tatizo hili na wale ambao wana maradhi yanayohusisha mfumo wao wa damu ni vyema kuhakikisha kuwa wanazingatia masharti yote waliyopewa na madaktari pamoja na kunywa dawa.

Tukumbuke siku zote kuwa shambulizi la moyo ni tukio la dharura na ni muhimu kuhakikisha kuwa tiba inapatikana haraka iwezekanavyo kwani kadiri muda unavyopita ndivyo uwezekano wa kuokoa maisha yako unavyopungua.

Ukihisi unapata dalili yoyote kati ya nilizoorodhesha awali hakikisha unaenda hospitali haraka
 
Top