KIFUA kikuu ambacho ni maarufu kwa kuitwa TB, ni ugonjwa unaosababishwa na kiumbehai. Bakteria wa Mycobacterium Tuberculosis (TB) anaweza kushambulia sehemu yoyote ya mwili, lakini mara nyingi hushambulia mapafu.

Mtu anaweza kuwa na kifua kikuu kikali au tulivu. Kifua kikuu kikali au ugonjwa wa TB inamaanisha kuwa bakteria wanashambulia mwili na mfumo wa kinga unashindwa kuwazuia wasisababishe ugonjwa.

Watu wenye kifua kikuu kikali kwenye mapafu yao wanaweza kuambukiza bakteria mtu mwingine yeyote anayekuwa karibu yake kwani anapokohoa, kupiga chafya au kutema mate, mtu aliye karibu anaweza kuwavuta bakteria wa kifua kikuu wakati wa kupumua na kuambukizwa.

Watu wanaweza kuambukizwa bakteria wa kifua kikuu pia wasiokuwa wakali mwilini mwao. Iwapo mtu ana kifua kikuu tulivu, ina maana kuwa mwili wake umefanikiwa kupambana na bakteria wa kifua kikuu kwa ukamilifu na kuwazuia wasisababishe ugonjwa. Watu wenye kifua kikuu tulivu hawajisikii wagonjwa, hawana dalili, na hawawezi kuwaambukiza kifua kikuu watu wengine.

Kwa baadhi  ya watu, bakteria wa kifua kikuu wanakuwa tulivu maisha yote bila ya kuwa wakali. Lakini kwa watu wengine kifua kikuu tuli kinaweza kuwa kikali iwapo mfumo wa kinga wa mtu unadhoofika- kwa mfano kwa VVU.

Kifua kikuu kinaweza kubainishwa kwa kuingiza kiasi kidogo cha dawa inayoitwa Tuberculin kwenye ngozi ya mkono wa mtu. Iwapo ngozi itavimba ni dalili kwamba pengine mtu huyo ameambukizwa kifua kikuu.

Hata hivyo, njia hii haiaminiki kwa ukamilifu katika kubaini maambukizo ya kifua kikuu miongoni mwa watu walioambukizwa, kwa sababu mfumo wao wa kinga uliodhoofika hauwezi kuleta kinga imara dhidi ya protini alizoingizwa na kusababisha ngozi kuvimba. Kipimo hicho kinabaini kifua kikuu kikali na tulivu, kumaanisha kwamba kipimo hicho si sahihi kubainishia ugonjwa wa kifua kikuu kikali kwa watu wanaoishi katika maeneo ambapo kifua kikuu (na hivyo maambukizo ya kifua kikuu tuli) kimeenea sana.

Ubainishaji wa kifua kikuu kwenye mapafu unaweza kufanywa kwa x-ray au kipimo cha makohozi, ingawa na kipimo hiki hakiwezi kutoa ishara dhahiri ya maambukizo ya kifua kikuu kikali kwa mtu mwenye VVU, kwa sababu mifumo ya kinga haina nguvu ya kusababisha kuvimba dhidi ya bakteria.

Kutokeapo kifua kikuu cha mapafu cha ziada (ambapo ugonjwa unaathiri viungo vingine zaidi ya mapafu), sampuli za majimaji au tishu zinaweza kupimwa. Iwapo kuna shaka kuhusu ubainishaji wa kifua kikuu, kipimo cha ‘kalcha’ cha bakteria wa kifua kikuu kinaweza kupandwa kwenye maabara.

Hata hivyo, njia hii inahitaji vifaa maalumu na ghali na inaweza kuchukua wiki sita hadi nane kuleta matokeo. Iwapo vifaa tiba havipo, ubainishaji wa kifua kikuu mara nyingi hutegemea dalili.

DALILI Dalili za kifua kikuu hutegemea sana ni mahali gani bakteria wa TB wanakuwa. Kwa kawaida bakteria wa kifua kikuu wanakuwa kwenye mapafu na kusababisha kifua kikuu cha mapafu. Kifua kikuu cha mapafu kinaweza kusababisha kifua kikali kinachochukua zaidi ya wiki tatu, maumivu ya kifuani na kukohoa damu au makohozi. Dalili nyingine za ugonjwa wa TB ni pamoja na udhaifu au uchovu, kupungua uzito,   kukosa hamu ya kula, baridi, homa na kutoka jasho usiku.

Kifua kikuu tuli hakina dalili. TIBA Kwa kawaida, mgonjwa wa kifua kikuu anatumia vidonge kila siku wakati wa matibabu yanayosimamiwa. Ugonjwa wa kifua kikuu kikali unaweza kutibiwa kwa mchanganyiko wa antibiotics . Mchanganyiko sahihi wa dawa za kifua kikuu hutoa kinga na tiba.

Tiba inayofaa humwezesha haraka mgonjwa wa kifua kikuu kutoambukiza na kwa hiyo huzuia kuenea zaidi kwa kifua kikuu. Kufanikisha tiba ya TB, huchukua miezi sita hadi minane ya matumizi ya dawa ya kila siku. Dawa za aina mbalimbali zinatakiwa kutibu kifua kikuu kikali. Kutumia dawa mbalimbali kufanya kazi nzuri ya kuua bakteria wote na huenda ikakinga dhidi ya usugu kwa dawa.

Dawa zinazotumika zaidi ni Isoniazid, Rifampin (Rifadin, Rimactane), Ethambutol (Myambutol) na Pyrazinamide. Kuhakikisha matibabu kamili, mara nyingi inapendekezwa kuwa mgonjwa ameze vidonge mbele ya mtu atakayesimamia matibabu. Njia hii inajulikana kuwa DOTS (matibabu yanayofuatiliwa moja kwa moja, muda mfupi).

DOTS hutibu kifua kikuu kwa 95% ya wagonjwa. KINGA Dawa inayoitwa Isoniazid (INH) inaweza kutumiwa kama kinga kwa wale walio hatarini zaidi kuambukizwa kifua kikuu au kwa wale wenye kifua kikuu tulivu. Watu wenye kifua kikuu tulivu ambao si wagonjwa, wanaweza kutumia vidonge vya Isoniazid kwa miezi mingi ili kuwakinga wasipate kifua kikuu kikali.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwa watu wenye VVU na kifua kikuu tulivu (lakini si kifua kikuu kikali) wapewe kinga ya Isoniazid kama inavyotakiwa. Kifua kikuu chenye usugu wa dawa mbalimbali (MDR-TB) na Kifua kikuu chenye usugu wa dawa uliokithiri (XDR-TB) Iwapo aina fulani ya bakteria wa kifua kikuu ni sugu kwa dawa mwafaka za antibiotic hujulikana kuwa kifua kikuu chenye usugu wa dawa mbalimbali au MDR- TB.

Iwapo kitakuwa sugu kwa dawa za antibiotic tatu au zaidi za kundi la pili, kinajulikana kuwa kifua kikuu chenye usugu wa dawa uliokithiri, au XDR- TB. Usugu wa dawa kwa kawaida hutokea wakati wagonjwa wa kifua kikuu hawatumii na hawataki kutumia dawa walizoandikiwa kama walivyoelekezwa na mabadiliko ya bakteria ambao ni sugu kwa dawa wanaruhusiwa kuzaliana.  MDR- TB ni tatizo kubwa sana na gumu kutibu.

Katika matibabu ya kawaida (wakati mwingine yanaitwa matibabu mwafaka) kwa kifua kikuu, wagonjwa wanatumia vidonge vya isoniazid na rifampicin (dawa jarabati sana zilizopo kwa kifua kikuu) pamoja na dawa nyingine kwa kipindi cha miezi sita hadi minane. Itaendelea wiki ijayo.
 
Top