Miguu kutoa harufu mbaya ni tatizo sugu linalowakabili baadhi ya watu katika jamii, wengi wakiwa wanaume.
Katika nyakati hizi za mvua, tatizo hili linaonekana kuzidi kuwa
sugu, hali inayosababisha kuwepo na harufu mbaya hasa kwenye mikusanyiko
ya watu kama vile kwenye daladala.
Lakini watu wengi wenye tatizo hili huwa wagumu kukubaliana na hali
yao hata kutafuta tiba mahususi inaweza kuwaondolea kero hiyo.
Licha ya kuwepo sababu mbalimbali zinazochangia kutokea hali hiyo,
ukweli utabaki kuwa uchafu ndiyo chanzo kikuu cha miguu kutoa harufu.
Kwa kiasi kikubwa uchafu huo ndio unasababisha kuzaliwa kwa vijidudu
vinavyoleta harufu mbaya kwenye miguu na kuwakera wanaokumbana na harufu
hiyo.
Pamoja na tiba nyingine za kitaalamu ambazo mtu mwenye tatizo hili
anaweza kupata, usafi ni jambo kubwa analopaswa kuzingatia zaidi hasa
kipindi hiki cha mvua.
Ukigundua una tatizo hili, hakikisha unasafisha miguu yako mara kwa mara ukiiacha mikavu muda wote ili kuepusha unyevunyevu.
Kila unapovaa viatu vya kufunika, hakikisha unavaa soksi safi na
kavu. Epuka kurudia soksi au kuvaa ambazo hazijakauka vyema kwani
zinaweza kusababisha miguu kunuka mara dufu.
Usivae viatu vilivyoloa na endapo ikatokea umenyeshewa, hakikisha
unavianika kwenye hewa ili vikauke kupunguza uwezekano wa kutokea
harufu.
Kama utahisi tatizo ni kubwa zaidi ni vyema utumie sabuni zenye dawa
za kuua vijidudu pamoja na mafuta maalumu yanayoweza kutumika miguuni.
Ikishindikana, nenda kwa wataalamu wa afya.
Kwa ushauri na namna ya kumaliza tatizo hilo wasiliana nasi kwa namba 0784778788