Ahlan wasahlan wapenzi wasikilizaji
ni matumaini yangu kuwa hamjambo na karibuni kujiunga nami katika
kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Kipindi ambacho lengo lake kuu ni
kujadili masuala mbalimbali yatakayotupa ufahamu kwa ajili ya
kuziimarisha afya zetu na kulinda miili yetu Kama mnakumbuka katika
kipindi chetu kilichopita tulibainisha masuala tofauti na jinsi
yanavyoathiri afya zetu. Masuala hayo tulisema ni kama vile mazingira
yanayotuzunguka, watu tunaoishi nao, jinsia zetu, jenetiki, mila na
desturi na hata idadi ya vituo vya afya na hospitali katika jamii zetu.
Pia tulizungumzia lishe bora na mlo uliokamilika na tukamalizia kwa
kuwabainishia wasikilizaji wetu vidokezo muhimu au healthy tips
zinazotuelekeza namna ya kula vyema ili kulinda na kuziimarisha afya
zetu. Katika kipindi chetu cha leo tutazungumzia uhusiano uliopo kati ya
vyakula, afya na magonjwa.
Kama ambavyo tumezoa kusikia katika
jamii zetu kuwa karoti husaidia kuona vizuri, spinachi huimarisha
misuli, maziwa hujenga mifupa na kadhalika, hayo yote yanaonesha
uhusiano uliopo kati ya vyakula na afya zetu. Kuna uhusiano wa moja kwa
moja kati ya vyakula tunavyokula, afya zetu na maradhi. Hii ni kwa
sababu vyakula tunavyokula vinaweza kuwa ni lishe bora kwa miili yetu au
kinyume chake. Vilevile kiwango cha chakula tunachokula na kuupatia
mwili wetu pia kina taathira ya moja kwa moja kwa afya zetu. Kuwa na
ufahamu kuhusiana na chakula tunachokula, lishe na afya kunatupa uwezo
wa kuweza kuchagua chakula cha aina gani tule na kwa kiwango gani suala
ambalo kwa ujumla huusaidia moja kwa moja kuimarisha afya zetu,
kuiepusha miili yetu na baadhi ya maradhi na hata kutibu baadhi ya
magojwa tunayopata. Baadhi ya magonjwa kama matatizo ya moyo na mishipa
ya damu, asthma, kisukari na hata kensa pia yanaweza kuwa na uhusiano,
ambao ni mabadiliko yanayosababishwa na uvimbe wa muda mrefu mwilini au
chronic inflammatory reaction, mabadiliko ambayo huanzia katika tishu ya
mafuta. Wataalamu wanasema lishe ina taathira kubwa katika suala hilo.
Tabia nzuri au mbaya ya kula, huweza kumfanya mtu kuwa mnene na mafuta
ya ziada mwilini mwake hugeuka na kuwa kama uvimbe wa muda mrefu, suala
ambalo huweza kusababisha maradhi kwenye moyo na mishipa ya damu,
asthma, kisukari na hata kensa. Kwa kula lishe bora na salama pamoja na
kujiepusha na unene wa kupindukia tunaweza kuusaidia mwili kutokuwa na
mafuta mengi jambo ambalo huzuia baadhi ya maradhi kama hayo
tuliyoyataja. Uhusiano kati ya chakula na afya umeleta changamoto kubwa
katika masuala ya afya na kumefanyika tafiti nyingi katika uwanja huo.
Kwa mfano utafiti uliofanywa na Martha Clare Morris na timu yake huko
Chicago Marekani kuhusiana na uhusiano uliopo kati ya ugonjwa wa
usahaulifu wa Alzheimer, unaweza kukufanya hata wewe ndugu msikilizaji
kujiuliza mara mbili kabla ya kuamua chakula utakachokula. Watafiti hao
kwanza wamegundua kuwa, vyakula vyenye vitamin E vinahusiana moja kwa
moja na kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa Alzheimer. Vyakula
hivyo ni pamoja na nafaka zilizorutubishwa, mboga za rangi kijani,
tikiti maji, mbegu (seeds) mbalimbali na jamii ya karanga. Pia
wamefahamu kuwa, watu wanaokula samaki kwa wingi kwa uchache mara moja
kwa wiki, huwa wamepunguza kwa asilimia 60 hatari ya kupatwa na gonjwa
hilo la usahaulifu au Alzheimer kuliko wale ambao hawali kabisa samaki
au hula samaki mara chache. Sio vibaya kutambua kwamba, ugonjwa huo
huwapata karibu watu milioni 24 duniani kila mwaka hasa watu watu
wazee.
Hebu sasa tuangalie uhusiano uliopo kati
ya ugonjwa wa moyo na chakula. Baadhi ya vyakula vyenye mafuta mengi
husababisha kwa kiasi kikubwa maradhi ya moyo kwani kiwango kikubwa cha
mafuta aina ya trans fats yaliyopo kwenye vyakula hivyo kwa mfano
vyakula vya fast food, yanaweza kuziba mishipa ya damu na baada ya muda
kuongeza kiwango chakolestero mwilini. Suala hilo katika miaka ya hivi
karibuni limeleta wasiwasi mkubwa hasa kutokana na kuongezeka idadi ya
vijana wenye umri mdogo wenye unene wa kupindukia, hali inayosababishwa
na kula vyakula vyenye mafuta vinavyopikwa majiani au nje ya nyumba
vinavyojulikana kimombo kama fast food. Vyakula hivyo ni kama chips au
viazi vya kukaanga, kuku wa kukaanga, samaki wa kukaanga, bisikuti,
piza, keki na vinginevyo. Mafuta ya aina hiyo hutokana na mafuta ya
majimaji na yale ya samli na huweza kusababisha magonjwa ya moyo.
Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa afya ya Jamii wa Chuo Kikuu cha
Havard nchini Marekani na kuchapishwa katika Jarida la Jumuiya ya
Magonjwa ya Moyo ya Marekani umeonyesha kuwa, aina ya mafuta ya trans
fats huongeza mara tatu magonjwa ya moyo kwa wanawake. Inafaa kukumbusha
hapa kwamba ugonjwa wa moyo ni ugonjwa unaoongoza kwa kuua duniani. Kwa
mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, ugonjwa wa moyo na mishipa ya
damu husababisha asilimia 63 ya vifo vyote vinavyotokea dunia, huku
tafiti zikionyesha kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya vyakula
vyenye mafuta mengi na ongezeko la maradhi ya moyo.
Kilichopo hewani mpenzi msikilizaji ni
kipindi cha 'Ijuwe Afya Yako' kinachowajia kupitia idhaa ya kiswahili
Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kama tulivyoahidi huko nyuma katika
kipidi hiki pia tutakuwa tukizungumzia baadhi ya tafiti na chunguzi
mbalimbali zilizofanywa kuhusiana na masuala ya afya.
Hivi karibuni uchunguzi mpya umeonyesha
kwamba kula zabibu au vyakula vyenye zabibu ndani yake hupunguza
shinikizo la damu, husaidia moyo kufanya kazi zake vyema na kupunguza
hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo. Kwa mujibu wa uchunguzi huo
uliotangazwa kenye mkutano wa Majaribio ya Biolojia huko California,
zabibi zina uwezo wa kupunguza shinikio la damu, husaidia mwili uweze
kuvumilia sukari (glucose tolerance) na kupunguza kiwango cha mafuta
aina ya triglycerides mwilini ambayo ni chanzo cha matatizo ya moyo.
Wataalamu wanasema zabibu pia zinaweza kupunguza uvimbe, uharibivu
unaotokana na free radicals zinazozalishwa mwilini, na shinikizo la
moyo. Hayo yote yakitokana na mada zijulikanazo kama phytochemicals
zilizoko kwenye matunda ya zabibu. Matunda hayo huzuia tatizo
linalojulikana kama Metabolic Syndrome. Metabolic Syndrome ni
mchanganyiko wa matatizo ya kitiba yanayoongeza uwezekano wa kupatwa na
maradhi ya mishipa ya damu pamoja na kisukari. Hivyo wataalamu
wanatushauri tule zabibi au kuongeza zabibu katika vyakula tunavyokula
kila siku, ili tujikinge na ugonjwa huo, maradhi ya moyo na kisukari
aina ya pili (type 2 diabates). Haya shime wapenzi wasilizaji tule
zabibu kwa ajili ya afya zetu.Tumetahadharishwa kwamba kulala chini ya
masaa 6 kila usiku kunaweza kusababisha mtu afe mapema. Wataaalamu
wamesema kwamba watu ambao kwa kawaida huwa wanalala masaa hayo machache
wengi wao hupatwa na vifo vya mapema kwa asilimia 12 zaidi ya wale
wanaolala kawaida kwa masaa 8, vifo ambavyo hutokea katika umri wa baada
ya miaka 25. Pia imeonyeshwa kwamba kulala kwa zaidi ya masaa 9 pia
kunapelekea vifo vya mapema ingawa kulala huko kunaweza kukawa na
uhusiano na matatizo ya kiafya. Utafiti huo umetolewa kwa kuchunguzwa
uhusiano uliopo kati ya kifo na usingizi kwa kutegemea chunguzi 16
zilizofanywa kwa kuwahusisha watu milioni 1 na nusu katika nchi za
Uingereza, Marekani , Ulaya na Mashariki mwa Asia. Profesa Francesco
Cappiccio aliyeongoza utafiti huo wa Chuo Kikuu cha Warwick cha
Uingereza anasema, jamii za sasa zilizoendelea zimekuwa taratibu
zikipunguza muda wa kulala, na tatizo hili linawapata sana watu
wanaofanya kazi masaa mengi. Amesema suala hili linaonyesha kwamba hayo
yote yanatokana na mashinikizo ya kimaisha yanayowapelekea watu wafanye
kazi masaa mengi na kuchukua shifti nyingi za kazi. Amesema kwamba,
kuporomoka kwa afya kunaambatana na kulala masaa mengi zaidi. Usingizi
ni kama karatasi ya litmus inayoonyesha afya na hali ya mwili na akili
ya mtu kwani usingizi unaathiriwa na magonjwa na hali mbalimbali ukiwemo
msongo wa mawazo au depression, anasema mtaalamu huyo. Tunashauriwa
tusilale masaa machache wala mengi kupita kiasi bali tulale kwa masaa ya
wastani ambayo ni masaa 8.
Na utafiti unaotuhitimishia kipindi
chetu cha afya leo ni ule unaosema kwamba, kuna uhusiano kati ya kucheka
na kuishi maisha marefu. Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la
Saikolojia la Sayansi umeonyesha kwamba, watu wenye tabasamu pana
linalojulikana kama 'Dunchenne smile', huishi maisha marefu. Ernest L.
Abel aliyeongoza utafiti huo amesema kwamba, watu ambao wanaonyesha
hisia zao na kuziakisi kwa tabasamu pana, kimsingi huwa ni watu wenye
furaha zaidi kuliko wale wenye kutabasamu kidogo. Hivyo watu hao
hufaidika na suala hilo na kwa kawaida huishi maisha marefu. Wataalamu
wanasema kwamba watu wenye kutabasamu sana kwa kawaida huwa wana furaha,
shaksia madhubuti, ndoa zao hudumu zaidi, wana ufahamu mzuri zaidi wa
mambo na huwa na maingiliano mazuri na watu wengine.
Na kufikia hapo wapenzi wasikilizaji hatuna la ziada.