HISTORIA inaonyesha kwamba tumbaku ilivumbuliwa na mabaharia wa
Kihispania kwenye fukwe za Marekani mwaka 1500 (BK). Kuanzia hapo,
wafanyabiashara wa Kizungu waliichukua tumbaku hiyo kutoka Marekani na
kuisambaza sehemu mbalimbali duniani walikokuwa wakifanya biashara zao.
Iliaminika kwamba tumbaku ni zawadi kutoka kwa Mungu. Moshi wa tumbaku
uliotolewa nje baada ya kuvuta, ulidaiwa kuwa na uwezo wa kubeba
mawazo/matakwa ya mvutaji pamoja na sala kwenda mbinguni. Aidha, tumbaku
ilitumiwa kama dawa ya masikio, meno na mafua yatokanayo na baridi.
Aina za Tumbaku
Kwa sasa inaaminika kuwepo kwa aina sita za tumbaku.
- BIDIS: Hizi ni aina ndogo ya sigara zilizotengenezwa kwa mkono, na hutumiwa sana katika nchi za Bara la Asia. Mtu anapovuta aina hii ya sigara hupata lami, nikotini na kaboni monoksidi nyingi zaidi kuliko sigara za kawaida.
- BIRI: Hii ni aina ya sigara inayosokotwa kwa majani ya tumbaku au kwa kutumia karatasi iliyotengenezwa kwa tumbaku. Kwa kulinganisha na asidi ya tumbaku iliyo kwenye sigara, tumbaku iliyo kwenye biri hufanya nikotini iingie kupitia mdomo hata ikiwa biri haijawashwa.
- KRETEKS. Hii ni sigara inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa tumbaku na karafuu. Kwa kawaida asilimia 60 inakuwa ni tumbaku na asilimia 40 inakuwa ni karafuu. Mtu anapovuta aina hii ya tumbaku hupata lami, nikotini na kaboni monoksidi nyingi zaidi kuliko sigara za kawaida.
- VIKO: Hii ni tumbaku aina ya kiko. Tumbaku husagwa na kuwekwa kwenye kiko kinachotengenezwa maalum kwa ajili ya kuvuta tumbaku na mara nyingi hupendelewa kutumiwa na watu wenye umri mkubwa na ina athari zilezile za sigara za kawaida.
- UGORO. Hii ni tumbaku inayotumiwa moja kwa moja bila kutoa moshi. Aina hii hutumika kwa ama kwa kutafuna au kwa kunusa. Kwa hiyo nikotini yake huingia kwenye damu kupitia mdomoni. Ni hatari kutumia tumbaku hizo zisizokuwa na moshi kama tu tumbaku nyingine.
- SHISHA. Hii ni tumbaku inayovutwa kupitia mvuke wa maji maji. Moshi wa Shisha unaovutwa, hupitishwa kwenye maji kabla ya kuvutwa. Hata hivyo, mbinu hiyo haipunguzi kiasi cha nikotini kilichomo ndani ya tumbaku na zaidi huweza kusababisha kansa mapafu.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), linazungumzia matumizi ya tumbaku
kwa kusema: "Tumbaku inatumiwa katika njia nyingi tofauti-tofauti.
Tumbaku huuzwa katika maduka yanayouza dawa na bidhaa za vyakula vya
kuboresha afya. Hata hivyo, tumbaku ni hatari hata itumiwe kwa njia
yoyote ya gani."
Uvutaji wa tumbaku una kemikali za sumu, kama vile nikotini, lami
(tar), kaboni monoksidi, arsenic, benzopyrene na nyinginezo. Mvutaji
anameza sumu hizi angalau kwa kiwango kidogo. Madhara yake yanajumuisha
kufika wakati ambapo athari yake ni kuua kidogo kidogo viungo vya
mwanadamu na nyama nyama (tissues) za mwanadamu. Mtu anaweza kufa
kutokana na magonjwa yanayosababishwa na tumbaku kama vile kansa na
magonjwa ya moyo.
Kwa mujibu wa ripoti za WHO, kwa kila sekunde nane, mtu mmoja hufariki
dunia ulimwenguni kutokana na matumizi ya tumbaku. Inaaminika pia kwamba
watu saba kati ya wavutaji tumbaku 10, huanza matumizi hayo wakiwa
watoto.
Ripoti za shirika hilo zinasema kadri mtu anavyoendelea kuvuta tumbaku
kwa muda mrefu, hufupisha urefu wa maisha yake kwa takruban miaka 20
hadi 25. Hiyo inatokana na sababu kwamba tumbaku ina aina za kemikali
zipatazo 4,000 ambazo zina uwezo wa kudhuru afya ya binadamu. Uchunguzi
unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya chembe za moshi unaovutwa
hubakia mwilini.
Inaelezwa kwamba katika karne moja tu iliyopita, watu milioni zaidi ya milioni 100 walifariki dunia kutokana na uvutaji wa sigara.
Inaelezwa kwamba katika karne moja tu iliyopita, watu milioni zaidi ya milioni 100 walifariki dunia kutokana na uvutaji wa sigara.
Aidha, takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba watu zaidi ya milioni sita hufariki dunia kila mwaka kwa sababu ya kuvuta sigara.
Wataalamu wanaonya kwamba ikiwa mambo hayatobadilika, kufikia mwaka 2030, uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni nane kila mwaka. Aidha, wanatabiri kwamba uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu bilioni moja hivi kufikia mwisho mwa karne ya 21.
Wataalamu wanaonya kwamba ikiwa mambo hayatobadilika, kufikia mwaka 2030, uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu zaidi ya milioni nane kila mwaka. Aidha, wanatabiri kwamba uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu bilioni moja hivi kufikia mwisho mwa karne ya 21.
Athari za tumbaku zinaanzia kwa mkulima wa zao hilo, familia yake na
hatimaye mvutaji na watu wanaokaa karibu na wavutaji nao. Upo ushahidi
wa kutosha wa kisayansi kwamba moshi wa sigara usiokuwa wa moja kwa
moja, husababisha magonjwa sawa kama sigara inayovutwa moja kwa moja,
ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo na mishipa, mapafu na upumuaji
(COPD).
Kutokana na hali hiyo, maelfu ya watu wasiovuta sigara nao hufariki
dunia kila mwaka kutokana na kuishi au kukaa karibu na watumiaji wa
tumbaku. Ndiyo maana WHO wanasema: "Moshi wa sigara unaweza kumdhuru mtu
asiyevuta bila kujali kiwango cha moshi anachopumua."
Hivi sasa, hatari za kiafya za moshi wa tumbaku ni suala la makubaliano
ya kisayansi, na hatari hizo zimekuwa moja ya motisha kubwa kwa ajili
ya kupiga marufuku sigara katika maeneo ya kazi na ndani ya maeneo ya
umma, ikiwa ni pamoja na mikahawa, baa na klabu za usiku.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Wazuiaji Tumbaku Tanzania
(CTCA), hakuna mkulima wa zao la tumbaku ambaye amenufaika na kilimo
hicho. Badala yake, utafiti huo unabainisha kwamba wakulima wengi wa zao
hilo wamechoka kiafya kutokana na maradhi ya ngozi, kansa na magonjwa
ya kifua kikuu.
CTCA wanaamini kwamba kuendelea kuwepo kwa matangazo, promosheni na
ufadhili wa bidhaa za tumbaku nchini kumesababisha ongezeko kubwa la
matumizi ya tumbaku miongoni mwa vijana. Kwa mfano, utafiti uliofanywa
mwaka 2008 na taasisi binafsi ya Global Youth Tobacco Survey, ulionyesha
kuwa asilimia 1.06 ya wanafunzi mashuleni na vyuoni wanatumia bidhaa
zinazotokana na tumbaku.
Baadhi ya athari za tumbaku katika mwili wa binadamu ambazo zimethibitishwa na wanasayansi ulimwenguni:-
Nywele – Uvutaji wa sigara hudhoofisha kinga ya mwili na kisha kudhuru mizizi ya nywele mapema.
Akili – Uvutaji sigara una madhara kwa akili ya mwanadamu na namna ya
kuwasilisha hoja zake. Mtu ambaye ameathirika na sigara anapitia vipindi
vibaya vya kuhitaji kuvuta sigara kila wakati na kumfanya kuwa mgumu wa
kufikiri, kuwa makini, kusuluhisha tatizo au kufanya jambo lolote
muhimu hadi avute sigara. Pale mtu anapovuta sigara, misuli yake
inajiachia na anapata kipindi cha mapumziko mafupi ya kutokwa na akili
yanayogubika tatizo lililomkumba, lakini baada ya hapo mvutaji anaweza
kupatwa na maumivu ya kichwa na kizunguzungu.
Aidha, tumbaku husababisha uraibu (addiction). Kemikali aina ya
nikotini katika tumbaku husisimua na vile vile hutuliza hisia.
Wanasayansi wamegundua kwamba nikotini hiyo huongeza kiwango cha homoni
za mkazo. Lakini pia, kemikali hiyo humfanya mvutaji ajisikie vizuri
wakati anavuta sigara, na zaidi humpa mvutaji msongo wa mawazo na
kushuka moyo pindi anapomaliza kuvuta sigara.
Kuvuta sigara hupeleka nikotini haraka kwenye ubongo tena na tena.
Inaelezwa kwamba pafu (mvuto) moja la sigara, ni sawa na dozi moja,
hivyo mvutaji wa kawaida anaweza kuvuta dozi 200 kwa siku, ambacho ni
kiwango cha juu kuliko dawa yoyote ile. Ndiyo maana nikotini husababisha
uraibu mkubwa zaidi. Mtu aliyezoea kuvuta sigara hujihisi vibaya
anapokawia kuvuta.
Macho – Wavutaji wa sigara hupata magonjwa ya macho mara nyingi kuliko
wasiovuta. Sehemu ya macho inayopitisha mwangaza inaweza kufichwa kama
vile wingu linavyoficha jua na kusababisha upofu. Ugonjwa huu
husababishwa kwa njia mbili. Kwanza moshi wa sigara huwasha macho, na
pili; kemikali zilizo ndani ya sigara hupita kwenye mishipa ya damu na
hatimaye kudhuru macho. Sigara pia husababisha kudhoofika kwa sehemu ya
kati ya macho (retina) na hivyo kupunguza uwezo wa macho kuona vizuri na
hata kutofautisha rangi (macular degeneration).
Ngozi – Uvutaji tumbaku husababisha kukauka kwa ngozi, kubadilika rangi
ya ngozi na kuwa njano pamoja na kukunjamana kwa ngozi. Sigara huleta
magonjwa mengi ya ngozi kama vile uvimbe, kuwashwawashwa na kudhoofisha
hali ya ungaavu wa ngozi. Kemikali zinazopatikana ndani ya sigara
hupunguza uwezo wa ngozi kujirekebisha, hivyo ngozi huzeeka haraka na
kupoteza uwezo wa kulainika. Mvutaji wa sigara huonekana mzee zaidi
kuliko umri wake.
Aidha, harufu mbaya ya moshi huganda katika ngozi. Uvutaji sigara
unasababisha saratani ya ngozi. Kemikali za sigara husababisha vidonda
kwenye ngozi na ambavyo haviponi kwa urahisi, ma wakati mwingine huweza
kugeuka na kuwa saratani.
Masikio – Uvutaji sigara huweza kusababisha magonjwa ya masikio. Sababu
ni kwamba uvutaji wa sigara husababisha uchafu kuganda kwenye mishipa
ya damu, na hivyo kupunguza mwendo wa damu hadi kwenye sehemu za ndani
za masikio. Moshi na kemikali za tumbaku pia hujeruhi sehemu za ndani za
masikio na majeraha hayo yanaweza kuambukiza hata ubongo (meningitis)
na hatimaye kusababisha uziwi.
Kinywa – Tumbaku hutatiza mdomo na kuongeza uchafu unaoganda kwenye
meno, hivyo kusababisha kuoza kwa meno na harufu mbaya mdomoni. Tumbaku
huathiri chembechembe za kinywa zinazotumika kuonja ladha ya chakula,
hali inayowasababishia watumiaji wa tumbaku kushindwa kufurahia vizuri
ladha ya vyakula.
Aidha, tumbaku husababisha fizi za kinywa kutokwa na damu, na wakati
mwingine husababisha kushindwa kupona kwa vidonda mdomoni, hasa baada ya
kung'olewa kwa jino. Saratani za mdomo, ulimi na koo zinapatikana zaidi
kwa wavutaji sigara na watumiaji wa tumbaku za aina nyingine.
Mapavu – Wavutaji wa tumbaku hupata taabu ya kupumua kwa kuwa uvutaji
huharibu mapafu. Uvutaji husababisha kukohoa na kutoa malenda-lenda
pamoja na magonjwa ya mapafu (emphysema & chronic bronchitis).
Endapo mvutaji ana ugonjwa wa pumu, anaweza kuongeza hatari zaidi ya
kubanwa kifua na kuishiwa pumzi.
Uvutaji wa sigara ndiyo sababu kubwa zaidi ya saratani ya mapafu, na
pia husababisha kupasuka kwa vibifu vya hewa safi na kutoa harufu mbaya
mwilini. Wavutaji pia hupata saratani ya koromeo na kuziba njia ya hewa,
na hivyo inabidi kutobolewa kwa kishimo kwenye shingo ili kuwezesha
mgonjwa kupumua.
Nyama za mwili na mifupa – Tumbaku husababisha mzunguko wa damu na hewa
safi, kwa maana ya oksijeni kupungua kwenye nyama za mwili na hivyo
kusababisha maumivu ya nyama na viungo pale mvutaji anapofanya mazoezi
au anapokuwa michezoni.
Sigara inasababisha mifupa kuwa mnyepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kwamba kemikali zilizoko ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu. Mifupa kama hii huvunjika kwa urahisi na kuchukua muda mrefu kupona, hivyo kusababisha magonjwa ya mifupa kama vile ‘Rhematoid Arthritis.’
Sigara inasababisha mifupa kuwa mnyepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kwamba kemikali zilizoko ndani ya sigara, hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu. Mifupa kama hii huvunjika kwa urahisi na kuchukua muda mrefu kupona, hivyo kusababisha magonjwa ya mifupa kama vile ‘Rhematoid Arthritis.’
Moyo – Tumbaku ni chanzo kikuu cha magonjwa ya moyo. Uvutaji wa tumbaku
huharibu mishipa ya damu, hufanya mishipa kuvimba na kufanya upenyo wa
damu kuwa mdogo. Hali hii husababisha moyo kusukuma damu kwa nguvu na
kasi kubwa kuliko kawaida na hivyo kusababisha shinikizo la damu kupanda
(High Blood Pressure). Hata kwa wale wanaovuta sigara chini ya tano kwa
siku, wako katika hatarini pia kupata magonjwa ya moyo.
Aidha, uvutaji tumbaku husababisha damu kuganda kwenye mishipa ya damu
na kuzuia mzunguko wa damu hadi kupelekea mshtuko wa moyo(Heart attack)
tatizo linaloweza sababisha kifo cha ghafla. Moja kati ya kila vifo
vitatu ulimwenguni hutokana na magonjwa ya moyo na huua zaidi ya watu
milioni moja kwenye nchi za Afrika. Kiharusi/Kupooza(Stroke) kinaweza
tokea endapo damu itaganda kwenye mishipa ya damu ya kichwa na kuzuiia
mzunguko wa damu kichwani au pale mishipa inapozidiwa na kupasuka.
Tumbo – Sigara hupunguza uwezo wa mwili kujikinga dhidi ya viini
vinavyosababisha vidonda tumboni. Pia hupunguza uwezo wa tumbo
kustahimili nguvu ya asidi baada ya kula. Vidonda vya mvutaji huwa ni
vigumu kutibu na mara nyingi hutokea tena baada ya kupona.
Vifole na Kucha – Tumbaku husababisha kutu inayokusanyika na kuganda
kwenye kucha na vidole vya mvutaji, na hivyo kusababisha kubadilika kwa
rangi ya vidole na kucha kuwa manjano au maji ya kunde. Ngozi ya vidole
pia hukauka na kuwa ngumu kwa sababu ya joto na kemikali za sigara.
Mishipa ya Damu – Uvutaji tumbaku husababisha ugonjwa ambao kitaalam
unajulikana kama ‘Buerger's Disease.’ Huu ni ugonjwa wa uvimbe kwenye
mishipa ya damu ya miguuni na mikononi. Mishipa hii huzibwa na kuzuia
mwendo wa damu kwenye sehemu zilizoathirika. Isipotibiwa kwa haraka,
mvutaji anaweza kukatwa miguu au mikono.
Afya ya uzazi kwa mwanamke – Uvutaji tumbaku hupunguza nafasi za
mwanamke kushika mimba na kuharibu DNA kwenye shahawa za mwanaume. Ni
vigumu zaidi kwa mwanamke mvutaji sigara kutunga mimba na ni rahisi sana
kwake kumpoteza mtoto wakati wa kulea mimba (Miscarriage). Uvutaji wa
sigara pia hufanya mwanamke kuzaa mtoto iyekufa (Stillbirth) au aliye na
kasoro kama uzito usiotimia wa kawaida. Watoto hawa huwa na afya duni
baadaye kwa sababu ya kemikali za sigara ambazo hupunguza mwendo wa
mtoto kukua akiwa angali mimbani.
Aidha, sigara husababisha ugumba (menopause) kabla ya wakati wake.
Sigara inaweza kumfanya mwanamke kuwa tasa. Na pia sigara huongeza
hatari ya kupata saratani ya fuko la uzazi (Cancer of the uterus).
Afya ya uzazi kwa mwanaume – Uvutaji wa tumbaku unapunguza msukumo wa
damu kwenye sehemu za uume. Sigara pia huharibu mbegu za kiume, na kwa
hiyo watoto wanaozalishwa huwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na kasoro za
maumbile na kupata magonjwa ya saratani. Sigara pia huweza
kuwasababishia wanaume wawe tasa.
Saratani – Zaidi ya kemikali 40 zinazopatikana kwenye tumbaku
zimethibitishwa kusababisha magonjwa ya saratani kwa mvutaji,
ikilinganishwa na asiyevuta sigara. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road mwaka 2010/2011, umebainisha kwamba zaidi ya
asilimia 30 ya saratani zote, zinahusishwa moja kwa moja na matumizi ya
tumbaku na hivyo kuigharimu Serikali zaidi ya dola za Marekani milioni
40 kuhudumia wagonjwa wa saratani.
Kisukari – Uvutaji sigara husababisha aina ya pili ya kisukari (Type 2
Diabetes Mellitus), na hufanya kuwa vigumu kudhibitiwa. Hatari ya kupata
kisukari ni asilimia 30-40 kwa wavutaji, ikilinganishwa na wasiovuta.
Endapo mvutaji ana ugonjwa wa kisukari, anaongeza mara mbili hadi tatu
hatari ya kupata ugonjwa wa figo. Pia wavutaji wenye kisukari wana
hatari zaidi ya magonjwa ya moyo, macho na mfumo wa fahamu.