JUMLA ya watoto 76 wamezaliwa katika mkesha wa Mwaka Mpya katika jiji la Dar es Salaam, huku akinamama wakishauriwa kutobeba mimba katika kipindi cha baridi ili kujifungua wakati wa msongamano mdogo hospitali.

Watoto hao wamezaliwa katika Hospitali za Amana, Mwananyamala, Temeke na ya Taifa Muhimbili, huku kati yao 14 wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.

Katika Hospitali ya Amana, Ofisa Muuguzi wa Zamu, Rose Mkondola alisema watoto waliozaliwa katika hospitali hiyo ni 25 huku waliozaliwa kwa upasuaji ni watano, ambapo watoto na wazazi hali zao zinaendelea vizuri.

Alisema kipindi hiki, idadi wa akinamama wanaojifungua ni wachache, kutokana na wanawake wengi hubeba mimba katika kipindi cha baridi na hivyo kujifungua katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi.

“Hali zao zinaendelea vizuri na baadhi yao wameruhusiwa, kipindi hiki akinamama wamekuwa wachache kwa sababu ni kama huwa wana msimu, huwa tunawashauri wasibebe mimba katika kipindi cha baridi kwa sababu msongamano unakuwa mkubwa na wahudumu wachache kwa hiyo ni vurugu,” alisema.

Kwa upande wa Hospitali ya Mwananyamala, Muuguzi Kiongozi Rehema Kessy alisema watoto waliozaliwa hospitalini hapo ni 23, ambapo kati yao wa kiume ni 18 na wa kike watano.

Alisema hali za watoto na mama zao ni za kuridhisha, kutokana na huduma nzuri walizopata hospitalini hapo. Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kaimu Muuguzi wa Wadi ya Wazazi, Renalda Kisheo alisema, watoto waliozaliwa katika hospitali hiyo ni tisa, wa kiume watatu na wa kike sita.

Alisema watoto saba kati yao, walizaliwa kwa njia ya upasuaji huku wawili wakizaliwa kwa njia ya kawaida. Hata hivyo, alisema mtoto mmoja alifariki baada ya kuzaliwa.

“Wote wako salama wazazi na watoto wao, isipokuwa huyo mtoto mmoja ambaye alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa, lakini wagonjwa wote wanaendelea vizuri,” alisema.

Muuguzi wa Hospitali ya Temeke, Rolester Kinunda, alisema katika hospitali yake wamezaliwa watoto 19, kati yao wakiume 10 na wa kike 9. Kinunda alisema kati yao, mmoja amezaliwa kwa njia ya upasuaji na wazazi na watoto wao wanaendelea vizuri.
 
Top