WATAALAMU wa afya nchini, wameonya juu ya kuwepo kwa ongezeko kubwa la
magonjwa yasiyoambukiza yanayotokana na kula vyakula vyenye mafuta mengi
na hivyo kumsababishia mlaji kupata magonjwa hayo imeelezwa.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kutokana
na tatizo hilo inahitaji kufanya uchunguzi zaidi ili kutokomeza kabisa
tatizo la magonjwa ya kuambukizwa na yale yasiyo ya kuambukizwa kwa
wakati mmoja.
Katika mahojiano ya FikraPevu
na wataalamu hao wameelza kwamba wakati muda wa mwisho wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia (MDGs), ukikaribia kufika hapo mwaka 2015, ni
dhahiri kuna mjadala mpana kuhusu malengo ya maendeleo mengine ambayo
yanahitaji kufanyiwa kazi katika kipindi cha miaka ijayo.
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Mwelecele Malecela, ameeleza kuwa tatizo
kubwa la afya ya jamii nchini lipo katika kweka ulinganifu wa
kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kwa wakati mmoja.
“Wenzetu magonjwa ya kuambukizwa yamepungua lakini kwetu bado,
tunahitaji kufanya uchunguzi zaidi kuhakikisha tunapambana na magonjwa
hayo yote” alieleza Dk. Malecela.
Daktari mshauri wa Hospitali ya Hindu Mandal, Kaushik Ramaiya, ya
jijini Dar es Salaam amesema kati ya mambo manane ya Malengo ya
Maendeleo ya Milenia (MDGs), matatu yanazungumzia kuhusu afya ambayo ni
kupunguza vifo vya watoto, kuboresha afya ya uzazi na kupambana na
HIV/AIDS, kifua kikuu, malaria na magonjwa mengine.
Aidha, amesema ni vema Watanzania wakajikita kuzuia magonjwa yasiyoambukiza na yale ya kuambukiza badala ya kusubiri kuyatibu.
“Mwelekeo wetu kwa sasa ni kuzuia magonjwa kutokea hasa kwa magonjwa
yasiyo ya kuambukizwa na hiyo inawezekana kwa kuacha kufanya mambo au
kupunguza kula na vinywaji vinavyochangia watu kupata magonjwa yasiyo ya
kuambukizwa”.
Dk Innocent Mosha, wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa katika
Hospitali ya Muhimbili anasema, idadi kubwa ya Watanzania hawana ufahamu
wa kutosha juu ya matatizo hayo kuhusu ukali wa matatizo hayo na
yanavyosababisha watu wengi kutojua jinsi yanavyoweza kusababisha
madhara makubwa katika mifumo mbalimbali ya mwili katika ubongo, moyo,
figo, macho na mishipa ya damu.
Kuongezeka kwa magonjwa hayo
Hata hivyo, imeelezwa kuwa pamoja na kutajwa kwa magonjwa yasiyo ya
kuambukizwa ikiwemo moyo, mapafu, saratani, kisukari na mengine mengi,
kwa upande wa Afrika na Tanzania kwa namna ya pekee, magonjwa yasiyo ya
kuambukizwa yameongezwa kuwa ni matatizo ya akili, chembe cha damu, figo
na magonjwa yasababishwayo na ajali za barabarani.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO),
idadi ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini
Tanzania imefikia 3,712 sawa na asilimia 1.03 ya vifo vyote kwa jumla
wakati kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa figo katika Tanzania
imeripotiwa kuwa katika asilimia 14.
Waathirika
Idadi kubwa ya Watanzania watu wazima na watoto wasio na hatia ndio
wanaotajwa kuwa waathirika wanaopata mateso makubwa kutokana na aina
mbalimbali ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ikiwa ni pamoja na
magonjwa ya moyo, ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya mfumo wa mkojo,
magonjwa ya figo, mifumo ya neva, uti wa mgongo na magonjwa mengine
yanayohusiana na hayo.
Hata hivyo, pamoja na madhara hayo baadhi ya wananchi jijini Dar es
Salaam wamesema wanalazimika kutumia vyakula wanavyosikia kuwa vina
madhara kutokana na kipato kidogo wanachokuwa nacho pamoja na ukosefu wa
elimu ya kutambua madhara yake.
Chanzo
Imeelezwa kuwa ongezeko la magonjwa hayo yanatokana na kula vyakula
vyenye mafuta mengi na hivyo kumsababishia mlaji kupata magonjwa hayo
kama ilivyoripotiwa na FikraPevu katika siku za hivi karibuni.
Wataalamu wa afya wanasema mtu yeyote anaweza kupata magonjwa hayo
pasipo kujali umri na kwamba njia sahihi ya kuepuka magonjwa hayo ni
kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya, ikiwa ni pamoja na
kupunguza matumizi ya vyakula vyenye mafuta.
Tanzania inatajwa kuwa miongozi mwa Nchi zinazoendelea, kuwa na idadi
kubwa ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ambapo
zaidi ya watu (milioni Nane) hufa kila mwaka kutokana na magonjwa hayo.
Takwimu za Kidunia pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka
2012/2013, zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 35 hufa ndani ya mwaka
mmoja duniani, hali ambayo inachangaia kushuka kwa uchumi wa mataifa
mbalimbali duniani.