Wanawake wengi hutarajia kujifungua watoto wenye siha njema pindi wanapokuwa wajawazito ingawa hawatendi kulingana na matakwa yao. Kuhudhuria kliniki ni moja ya takwa wanaloshindwa kulitimiza. Wajawazito hufikiri kuhudhuria si lazima mpaka wapatwe na matatizo ya mimba zao.
Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO) linasema sababu zinazofanya wanawake wasipate au kutafuta huduma wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua ni pamoja na umaskini, umbali, kutokuwa na taarifa, kutokuwepo kwa huduma na mila potofu.
Kulingana na Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa, takwimu zilizochapishwa mnamo Oktoba 2007 zinaonyesha kuwa mwanamke mmoja hufa karibu kila dakika, yaani wanawake 536,000 kwa mwaka, kwa sababu ya matatizo yanayohusianishwa na ujauzito. Matatizo mengi ya ujauzito yanaweza kugundulika mapema na kutibiwa mapema ikiwa mjamzito atahudhuria kliniki kwa ukawaida.
Shirika la Afya Ulimwenguni linaongeza kusema kuwa, ingawa takwimu za huduma za kliniki kwa wajawazito zimeongezeka maeneo tofauti ya dunia kwa muongo mmoja uliopita, ni asilimia 46 tu ya wajawazito hupata huduma hiyo kwa nchi zinazoendelea.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, mjamzito asiye na matatizo ya mimba anapaswa kuhudhuria kliniki si chini ya mara 4 katika kipindi chote cha ujauzito ila kwa mjamzito mwenye matatizo ya mimba anapaswa kuhudhuria kliniki mara nyingi iwezakanavyo kulingana na hali yake.
Mahudhurio manne yapo kama ifuatavyo:-
Hudhurio la kwanza linapaswa kuanzwa chini ya wiki 16(Miezi minne), Hudhurio la pili ni kati ya wiki ya 20-24(Miezi mitano hadi sita), Hudhurio la tatu ni kati ya wiki 28-32(Miezi saba hadi nane) na Hudhurio la nne ni kati ya wiki 36-40(Miezi 9 hadi 10).
Nchini Tanzania, wanawake wanapaswa kuhudhuria kliniki mahudhurio manne hadi kujifungua na mahudhurio manne ndani ya wiki sita(siku 42) baada ya kujifungua yaani hudhurio la kwanza ndani ya masaa 48, hudhurio la pili ndani ya siku 7, hudhurio la tatu ndani ya siku 28 na hudhurio la nne ndani ya siku 42.
FAIDA ZA KUHUDHURIA KLINIKI
-> Kutia hamasa na kuimarisha afya ya mwili, akili na jamii ya mama kwa kutoa elimu juu ya lishe, usafi, kupumzika n.k
-> Kutambua na kutibu mapema matatizo ya afya ya mama na kasoro za maumbile.
-> Kumsaidia mama kuunda mkakati binafsi wa uzazi wake, ikihusisha kumfunza mjamzito juu ya dalili za hatari kwake na kwa mtoto atakayezaliwa.
-> Kumpa mama ushauri wa mambo ya afya kama jinsi ya kunyonyesha vizuri kujitunza baada ya kujifungua na jinsi ya kumtunza mtoto mchanga.
-> Kutengeneza ufahamu kwa wajawazito juu ya dalili zisizo za kawaida kabla na baada ya kujifungua.
-> Kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
-> Kuzuia maambukizi mengine kwa kutoa elimu ya afya.
VITU VINAVYOFANYIKA KATIKA MAHUDHURIO YA KLINIKI
HUDHURIO LA KWANZA
Hudhurio la kwanza linapaswa kuanzwa mapema tu pale mwanamke anapojijua ana ujauzito/mimba na inapendekezwa isiwe zaidi ya wiki ya 16(Miezi minne). Ni muhimu kwa mjamzito kwenda na mwenzi wake katika hudhurio la kwanza. Wahudumu huwapa wazo la kwenda kufikiria nyumbani juu ya mahali atakapojifungulia kulingana na hali yake ya kiafya na katika mahudhurio yanayofuata mjamzito anaweza kuwa na muafaka wa mahala atakapozalia.
Kwenye hudhurio hili mjamzito hupimwa na kutibiwa matatizo ya upungufu wa damu, kaswende & malaria pamoja na kupata chanjo ya Pepopunda kama inavyotakiwa. Hushauriwa na kupimwa UKIMWI. Endapo mjamzito atakutwa na virusi vya UKIMWI(VVU) atapelekwa kwenye kitengo husika na kuanza matibabu yatakayomkinga mtoto aliye tumboni dhidi ya VVU kutoka kwa mama. Bila matibabu hatari ya mjamzito kumuambukiza mtoto ni kwa asilimia 40, asilimia 10 wakati wa ujauzito, asilimia 20 wakati wa uchungu na kujifungua na asilimia 10 wakati wa kunyonyesha. Pia mjamzito hushauriwa juu ya umuhimu wa matumizi ya neti ya mbu iliyotiwa dawa ya kuua mbu/wadudu ili kujikinga na Malaria, ingawa atapewa vidonge vya Salfadoxine Pyrimethamine(SP) kama kinga dhidi ya Malaria.
Mjamzito anapaswa kupewa dawa zenye madini ya chuma na asidi ya foliki kwenye mahudhurio yote bila kujali wingi wake wa damu. Faida za madini ya chuma ni pamoja na kuimarisha kinga ya mwili, kutengeneza chembechembe nyekundu za damu, kuimarisha uwezo wa kuwa makini na kuongeza uwezo wa kufanya kazi vizuri. Na faida za asidi ya foliki ni pamoja na kutengeneza damu, kumkinga mtoto dhidi ya ugonjwa wa mgongo wazi na kuhakiki mfumo wa fahamu.
HUDHURIO LA PILI, TATU & NNE
Mahudhurio haya yana malengo ya kusitawisha afya ya mjamzito & kumpa nafasi ya kuamua ni wapi atajifungulia, kugundua matatizo mapema au hali hatari kama mimba ya mapacha, kupanda kwa shinikizo la damu, upungufu wa damu.
Wahudumu wa afya huangalia idadi ya watoto walioko tumboni, mlalo wa mtoto na kuchunguza matatizo(kasoro) zingine za ujauzito. Katika mahudhurio haya mjamzito huamua rasmi kituo cha kutolea huduma atakachojifungulia kulingana na hali yake ya kiafya. Ikiwa mjamzito hajajifungua baada ya wiki ya 40(Miezi 10) anapaswa kuchunguzwa kwa makini na kupewa rufaa haraka iwezekanavyo.
VIDOKEZO HATARISHI AMBAVYO HUCHUNGUZWA KWENYE MAHUDHURIO YA KLINIKI
(1) WINGI WA DAMU
Mjamzito akiwa na wingi wa damu chini ya asilimia 81(11.5 g/dl) ina maana ana upungufu wa damu. Kama mama atakuwa na upungufu wa kiwango cha damu, ujauzito huweza kuharibika. Kama hilo halitatokea basi mtoto atakayezaliwa anaweza kuwa na uzito mdogo kuliko inavyotakiwa na hata kuzaliwa kabla ya muda wake(kuzaa mtoto njiti). Mtoto anayezaliwa akiwa na uzito wa chini(< 2.5kg) anakabiliwa na hatari ya kufa mara 40 zaidi kuliko yule aliyezaliwa akiwa na uzito wa kawaida. Mjamzito mwenye upungufu wa kiwango cha damu anaweza kushambuliwa kirahisi na maradhi kama Malaria. Kama mjamzito atahudhuria kliniki wataalamu wa afya ya uzazi hugundua tatizo hilo na kutoa ushauri kuhusu mahitaji ya lishe na pia kurekebisha upungufu huo kwa kutumia vidonge maalumu vyenye madini ya chuma na asidi ya foliki.
(2) UZITO
Ongezeko hili la uzito hutokana na kuongezeka kwa kiwango cha damu na majimaji mwilini, mafuta, matiti kwa maandalizi ya kunyonyesha baada ya kujifungua, kukua kwa nyumba ya uzazi, uwepo wa maji ya uzazi, kondo la nyuma na uzito wa mtoto mwenyewe. Ongezeko linalopendekezwa kwa mwanamke mwenye uzito unaofaa anapokuwa na mimba ni kilogramu 9 hadi 12 kufikia wakati wa kujifungua. Hata hivyo wasichana au wanawake ambao hawakuwa wakila chakula cha kutosha wanapaswa kuongeza kilogramu 12 hadi 15 na wale wanene wanapaswa kuongeza kilogramu 7 hadi 9 tu.
(3)SHINIKIZO LA DAMU(PRESHA)
Shinikizo la damu katika kipindi cha ujauzito hubadilika kutegemea na umri wa ujauzito. Kitaalamu ujauzito hugawanywa katika vipindi vitatu vya wiki 12(miezi mitatu) kila kimoja.
Ndani ya miezi mitatu ya mwanzo(First trimester) mjamzito hupatwa na kichefuchefu na kutapika hasa wakati wa asubuhi(Morning sickness) endapo kutapika kukizidi (Exaggerated morning sickness/Hyperemesis gravidurum) ni lazima mjamzito apate matibabu. Miezi mitatu ya pili(Second trimester) mjamzito huanza kusikia/kuhisi kucheza kwa mtoto na uzito wa mama huongezeka sana. Kuongezeka kwa uzito kila wiki ukiwa ni zaidi ya gramu 500 hicho kinaweza kuwa ni kiashiria cha kupanda kwa shinikizo la damu kwa mjamzito. Miezi mitatu ya tatu(Third trimester) hiki ni kipindi ambacho kichanga cha tumboni hukua, mjamzito anaweza akaanza kutojisikia vizuri akitembea, akipumua, akilala n.k.
Ni vyema kufuatilia presha na mwenendo wake katika vipindi hivyo. Kwa ujauzito wa kawaida, presha ya chini kabisa inapaswa isipungue milimita za zebaki 90/60 na ile ya juu isizidi milimita za zebaki 140/90. Hata hivyo ufahamu wa presha kuwa juu au chini utategemea pia kiwango kilichopatikana wakati wa hudhurio la kwanza na mahudhurio mengine yaliyopita.
(4)VIDOKEZO VINGINE
Mjamzito hupimwa mkojo kuangalia protini(albumin), sukari katika mkoj. Kuangalia kundi la damu na rhesus. Hali ya chanjo hasa Pepopunda. Kuangalia kama mtoto anacheza hasa baada ya wiki ya 20, umri wa mimba kwa wiki, kimo cha mimba kwa wiki, mapigo ya moyo ya mtoto. Pia mjamzito hupewa dawa za minyoo.
DALILI ZA HATARI KWA MJAMZITO
(1) Kuishiwa pumzi, kuchoka sana, kizunguzungu kila wakati ambazo zinaweza kuwa dalili za upungufu wa damu.
(2) Kichwa kuuma sana na kuwa na malue lue zinaweza kuwa dalili za kupanda shinikizo la damu.
(3) Kutetemeka, homa na kutapika sana zinaweza kuwa dalili za Malaria.
(4) Kucheza kwa mtoto kupungua au kutokuwepo kabisa(dalili ya mtoto kufia tumboni).
(5) Mtoto aliye tumboni kutanguliza viungo vingine tofauti na kichwa.
(6) Kupoteza fahamu na degedege.
(7) Kutokwa uchafu ukeni wenye harufu mbaya.
(8) Kutokwa na ute wa tumboni ukeni.
(9) Kutokwa damu ukeni.
(10) Kuvimba kwa mwili hasa miguu, mikono na uso.
(11) Kuumwa sana na tumbo.
(12) Kusikia maumivu anapokojoa au kutopata mkojo kama kawaida.
MAMBO YA KUZINGATIA KWA MJAMZITO
(1) LISHE
Kila siku mjamzito anahitaji kula matunda, mboga(hasa zilizo na majani ya rangi nzito ya kijani & rangi ya machungwa au nyekundu), maharagwe mbalimbali(kutia ndani soya, dengu & njegere), nafaka(kutia ndani ngano, mahindi na shayiri hasa zile ambazo hazijatolewa maganda au zilizotiwa vitu vingine), chakula kinachotokana na wanyama(samaki, nyama ya kuku, nyama ya ng'ombe, mayai, jibini, maziwa hasa yale ambayo yametolewa mafuta). Mafuta, sukari na chumvi vinapaswa kutumiwa kwa kiasi. Kunywa maji mengi, epuka vinywaji vyenye kafeini na vyakula vilivyotiwa dawa za kuhifadhi na kemikali nyinginezo(kama za kutia rangi na ladha). Udongo wa mfinyanzi(pemba) na vitu vingine visivyoliwa vyaweza kusababisha utapiamlo na kumtia sumu mtoto na mama.
(2) MATUMIZI YA POMBE NA MADAWA YA KULEVYA
Mjamzito akinywa pombe, akitumia madawa ya kulevya au kuvuta tumbaku huzidisha hatari ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu wa akili na mwili. Ingawa wengine hudai eti kunywa pombe kidogo hakuwezi kudhuru, mara nyingi wataalamu hupendekeza wajawazito wasinywe hata kidogo.
(3) MATUMIZI YA DAWA/VIDONGE VYA MATIBABU YA MAAMBUKIZI
Hakuna dawa zinazozopaswa kutumiwa ila tu zile zilizopendekezwa na wataalamu wa afya wanaojua kuhusu mimba hiyo na ambao wanatambua athari za dawa hizo. Vitamini fulani pia zinaweza kudhuru kwa mfano kiasi kikubwa sana cha Vitamini A chaweza kumlemeza mtoto aliye tumboni. Pia ni muhimu kwa mjamzito kuepuka matumizi ya dawa za kupulizia mfano dawa za kuulia wadudu.
(4) USAFI NA MAMBO MENGINE
Ni muhimu kudumisha usafi wa kawaida kama kunawa mikono na kuosha vyakula kabla havijapikwa. Mara nyingi kufanya ngono hakuleti tatizo lolote ila tu katika majuma ya mwisho-mwisho ya mimba au kukiwa na mtiririko wa damu, maumivu tumboni au ikiwa mimba ya awali ilitoka.
Msomaji wangu, usisite kusoma makala haya pia kwakuwa yanaendana na kilichoandikwa sasa: Umri mzuri kwa mwanamke kupata mtoto (kuzaa)
 
Top