KANSA au kwa jina jingine, Saratani, ni kundi la magonjwa
yanayosababishwa na mgawanyiko usio sawa na usiodhibitika wa seli na
kuunda uvimbe unaovamia na kuzidhuru tishu za mwilini. Kansa
isiyotibiwa, inaweza kuwa ugonjwa unaoshambulia tishu nyingine mwilini
na kusababisha kifo.
Kwa kawaida, kansa huusababishia mwili madhara pale inapoharibu seli na
kuzifanya zigawanyike bila kudhibitika na kuwa uvimbe wa tishu
unaojulikana kama tumor, isipokuwa katika kansa ya damu ambapo kansa
huzuia utendaji wa kawaida wa damu kwa kuzifanya seli ziwe na mgawanyiko
usio wa kawaida katika damu.
Historia ya Kansa
Asili ya neno kansa linatokana na daktari bingwa wa Ugiriki aliyeishi
kati ya miaka 460 na 370 (K.K) anayejulikana kwa jina la
Hippocrates. Hippocrates alitumia maneno 'Carcinos' na 'Carcinoma'
kuelezea uvimbe unaotengeneza mchubuko (Carcinos) kwa upande mmoja, na
uvimbe usiotengeneza mchubuko (Carcinoma) kwa upande wa pili.
Maneno haya ya Kigiriki, yana maana ya mdudu kaa. Hii ni kwa sababu
ugonjwa ho wa kansa ulipogunduliwa kwa mara ya kwanza ulifananishwa na
mdudu kaa kwa kuwa ulikuwa ikisambaa kila upande kama miguu ya mdudu
kaa.
Kati ya miaka 25 na 50 (K.K), Daktari Bingwa mwenye asili ya Roma,
aliyejulikana kwa jina la Celsus alitafsiri maneno hayo kwa neno la
Kilatini, kwa kuita 'Cancer' likiwa na maana ya mdudu kaa. Miaka kati ya
130 na 200 (B.K), Daktari Bingwa mwingine kutoka Ugiriki, alitumia neno
'Oncos' likiwa na maana ya ‘kuvimba’ kuelezea uvimbe tofauti
usiosambaa.
Hata hivyo, maneno ya Hippocrates na Celsus, ya 'Carcinos' na 'Cancer'
yenye maana ya mdudu kaa ambayo bado yanatumika hadi leo kuelezea uvimbe
unaosambaa, neno la Galen 'Oncos' linatumika tu kama sehemu ya somo
linalohusu kansa (Oncology) au madaktari wa kansa (Oncologist).
Ni nini chanzo cha ugonjwa wa kansa?
Mwili wa binadamu umeundwa kwa trilioni za seli ambazo hukua,
kugawanyika na kufa kwa mpangilio maalumu. Mwenendo ulioratibiwa vyema
unasimamiwa na vinasaba (DNA) vilivyo ndani ya seli. Vinasaba hivyo,
vinapatikana katika kila seli, na huongoza matendo yote yanayofanywa na
seli. Katika seli ya kawaida, wakati vinasaba vinapoharibika, seli
hukarabati au seli hufa.
Lakini katika seli za kansa, kinasaba kilichoharibika huwa hakiwezi
kukarabatiwa na seli haifi kama inavyotakiwa, badala yake huendelea
kutengeneza seli nyingine ambazo hazitakiwi na mwili na hivyo seli hizo
mpya zote huwa na kinasaba kisichokuwa cha kawaida tofauti na seli
salama.
Watu huweza kurithi kinasaba kisichokuwa cha kawaida, ingawa mara
nyingi uharibifu wa kinasaba husababishwa na makosa yanayotokea wakati
seli ya kawaida inapotengenezwa au kutokana na sababu za
kimazingira. Ingawa inajulikana wazi kwamba kuna baadhi ya vitu
vinavyoweza kuharibu kinasaba na kusababisha kansa, kama vile kemikali,
uvutaji sigara, kuchomwa na jua na kadhalika, lakini bado hakuna uhakika
wa moja kwa moja kuhusiana na kinachosababisha kansa.
Wakati mtu anapokuwa mtoto mdogo au bado akiwa ndani ya tumbo la mama, seli hujigawanya kwa haraka ili kumfanya akuwe.
Baada ya mtu kukua, seli nyingi hugawanyika kwa ajili ya kuchukua nafasi ya zile zilizozeeka na kufa au kwa ajili ya kukarabati majeraha.
Baada ya mtu kukua, seli nyingi hugawanyika kwa ajili ya kuchukua nafasi ya zile zilizozeeka na kufa au kwa ajili ya kukarabati majeraha.
Kansa huanza wakati seli katika sehemu mojawapo ya mwili zinapoanza
kukua bila kudhibitiwa. Ukuaji wa seli za kansa hutofautiana na ukuaji
wa kawaida wa seli za mwili, na badala ya kufa pale zinapozeeka, zenyewe
huendelea kukua na kuzaa seli nyingine mpya zisizokuwa za kawaida.
Seli za kansa pia hushambulia kwa kuingia ndani ya tishu nyigine jambo
ambalo halishuhudiwi katika seli za kawaida. Kwa kawaida seli za kansa
husambaa katika sehemu nyingine za mwili ambako huko nako, huanza kukua
na kuunda uvimbe (tumor) mpya na baada ya muda kupita uvimbe huo
huchukua nafasi ya tishu mpya.
Kwa hiyo, kukua kusikodhibitiwa na kusiko kwa kawaida kwa seli, na
tabia ya seli hizo kuzishambulia tishu nyingine, ndiko hasa husababisha
seli za kansa.
Takwimu za ugonjwa wa kansa
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Tanzania ina idadi
ya watu milioni 44.9. Kutokana na takwimu zilizopo, watu 100 kati ya
100,000 hugundulika kuwa na ugonjwa wa kansa kila mwaka.
Hali hii ina maana kwamba watu wasiopungua 44,000 hugundulika kuwa na
kansa kila mwaka nchi nzima. Hadi sasa katika nchi nzima ya Tanzania,
kuna kituo kimoja tu kinachotoa tiba ya saratani kwa mionzi; Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road iliyopo Dar es salaam. Hata hivyo, katika muda
si mrefu kituo kingine kitafunguliwa katika Hospitali ya Bugando,
Mwanza.
Takwimu za ugonjwa huo ulimwenguni, zinaonyesha kwamba watu zaidi ya
milioni 12 hugunduliwa kuwa na kansa kila mwaka. Kati ya wagonjwa wote
hao, asilimia 60 hutokea katika mabara ya Afrika, Asia, Amerika ya Kati
na Kusini. Kimsingi, kansa huua watu wengi zaidi kuliko jumla ya wote
wanaokufa kwa magonjwa ya Ukimwi, malaria na kifua kikuu (TB). Kwa
mfano, katika mwaka 2012 pekee, watu takriban milioni 8.2 walikufa kwa
ugonjwa huo wa kansa duniani.
Sifa za ugonjwa wa kansa
Si kila uvimbe ni kansa, bali kuna uvimbe ambao si kansa, ambao
kitaalam huitwa 'Benign Tumors', kama vile Tezi dume (Benign Prostate
Hyperplasia). Uvimbe huweza kugawanyika na kukua, na pia hutengeneza
mirija mipya ya damu ili kujipatia lishe wenyewe. Kitendo hiki kitaalam
huitwa 'Angiogenesis.'
Hata hivyo, uvimbe huu usiokuwa kansa, unaweza kuleta matatizo kama
vile kukua sana na kuvibana viungo na tishu nyingine mwilini. Aidha,
uvimbe kama huu, huweza kukua na kuingilia mifumo ya umeng'enyaji,
fahamu na damu/limfu na huweza kutoa homoni zinazobadili utendaji wa
kawaida wa mwili.
Ingawa uvimbe usiokuwa kansa unaweza kuwa hatari kwa afya, lakini
hauwezi kuzishambulia seli nyingine au kusambaa katika viungo vingine
mwilini. Uvimbe wa aina hii, mara nyingi hutibika na huwa hauhatarishi
maisha.
Hata hivyo, aina zote za kansa zina sifa tatu zinazofanana. Sifa hizo
ni ukuaji wa seli usiodhibitika, uwezo wa kuvamia na kushambulia tishu
nyingine na uwezo wa kusambaa katika viungo vingine mwilini kupitia
mishipa ya damu au mikondo ya limfu. Kitendo hicho cha vidudu vua
ugonjwa wa kansa kusambaa mwilini kupitia mkondo wa damu na limfu,
kitaalam huitwa 'Metastasis'.
Aina za kansa
Hadi sasa kuna aina zaidi ya 200 za kansa kulingana na kiungo gani cha mwili kimeathirika au eneo la mwili linaloshambuliwa.
Baadhi ya kansa huwashambulia zaidi wanawake, kwa mfano kansa ya matiti na kuna baadhi ambazo huwashambilia zaidi wanaume.
Baadhi ya kansa huwashambulia zaidi wanawake, kwa mfano kansa ya matiti na kuna baadhi ambazo huwashambilia zaidi wanaume.
Baadhi ya kansa huwashambulia watu wa kundi fulani katika jamii
kutokana na aina yao ya maisha au kazi wanazofanya kila siku, na hali
kadhalika kuna baadhi ya kansa au saratani zinazoshambilia watoto zaidi
kuliko watu wazima, kwa mfano kansa ya damu aina ya 'Lymphoblastic'.
Zifuatazo ni baadhi ya aina za kansa kulingana na tabia hizo hapo juu:-
- CARCINOMAS. Hii ni saratani ambayo hushambulia viungo mbalimbali vya mwili vilivyo ndani na nje, kwa mfano mapafu, matiti, utumbo na kadhalika.
- SARCOMAS. Hii ni saratani inayopatikana kwenye mifupa, misuli na tishu mbalimbali mwilini.
- LYMPHOMAS. Hii ni saratani zinazoanza kwenye mikondo na vifundo vya limfu na kwenye tishu za kinga ya mwili.
- LEUKEMIAS. Hii ni saratani zinazoanza ndani ya ute wa mifupa (bone marrow) na kukusanyika kwenye mishipa ya damu.
- ADENOMAS. Hii ni saratani zinazochomoza kwenye tishu na tezi zinazotoa homoni mbalimbali hasa tezi zilizopo kichwani.
Ni nini huchangia kuwepo kwa ugonjwa wa kansa?
Asilimia 60 ya magonjwa yote ya kansa yanahusishwa zaidi na mtindo wa
maisha ambao vipengele vyake ni ulaji, mazoezi ya mwili na matumizi ya
pombe na tumbaku. Vitu vingine vinavyochangia, ni pamoja na virusi na
bakteria, madini mazito, mionzi na sumu kadhaa.
Vyakula huchangia kwa kiasi kikubwa saratani za kinywa na koo, matiti,
tezi ya kiume, utumbo mpana, mapafu, tumbo, ini, kongosho na
kizazi. Ulaji unaoweza kuchangia ugonjwa huu, ni pamoja na ulaji wa
nyama nyekundu kupita kiasi, nyama zilizosindikwa, vyakula vilivyokuzwa
kwa kemikali nyingi kama mbolea, vyakula vyenye mafuta mengi ambavyo
huweza kusababisha uzito mwingi na vyakula vilivyoota ukungu, kwa mfano
karanga.
Kitaalam, nyama nyekundu ni muhimu kwa binadamu, lakini inakuwa tatizo
pale inapoliwa zaidi ya nusu kilo kwa wiki. Ulaji wa nyama nyekundu
mfano ng'ombe, unaongeza uwezekano wa kupata saratani ya utumbo mkubwa.
Tafiti zimeonesha kuwa kula nyama nyekundu hadi nusu kilo kwa wiki
haiongezi uwezekano wa kupata saratani, lakini kila gramu 50
zinazoongezeka, huongeza uwezekano wa kupata saratani kwa asilimia 15.
Nyama zilizosindikwa pamoja na zile zilizohifadhiwa kwa kuongezwa
chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi kama nyama za kopo,
soseji na bekoni zinaongeza sana uwezekano wa kupata saratani. Hakuna
kiasi chochote cha nyama iliyosindikwa kinachoweza kutumika bila
kuongeza uwezekano wa kupata saratani.
Viazi vya kukaanga mfano viazi mviringo (ulaya), huongeza hatari ya
kupata saratani hasa vikikaangwa kwenye mafuta yenye haidrojeni na
lehemu. Viazi ni moja ya vyakula vyenye wanga sana na wakati wa
kukaangwa hutoa 'Acrylamide' ambayo ni kisababishi cha kansa hasa kwenye
mfumo wa fahamu.
Vinywaji baridi/Laini kama vile soda na juisi za viwandani navyo
vinaweza kusababisha kansa. Utafiti uliofanywa mwaka 2010 na Jarida la
'Cancer, Epidemiology, Biomakers & Prevention' unaonyesha kuwa mtu
aliyetumia soda mbili au zaidi ndani ya wiki moja, ana uwezekano wa
kupata saratani ya kongosho kwa asilimia 87 kuliko mtu ambaye hatumii
kabisa vinywaji hivyo laini.
Tafiti nyingine zimeonyesha uhusiano kati ya matumizi ya sukari na
saratani za tumbo na utumbo mpana, ingawa sukari haifanyi seli nzuri
zisizo na kasoro kuwa kansa ila sukari ni chakula ama chanzo cha lishe
cha seli za kansa. Pombe na tumbaku. Matumizi ya pombe na tumbaku
huchangia sana ongezeko la sarayani za koo na mapafu. Hapa nchini
Tanzania, ongezeko ni kubwa kwa sababu ya matumizi ya vitu hivyo.
Kwa mfano, asilimia 90 ya wagonjwa waliopelekwa Hospitali ya Ocean
Road, Dar es Salaam, walikuwa na historia ya kutumia vilevi vikali,
tumbaku, pilipili kwa wingi na aina nyingine ya vitu vinavyosababisha
saratani. Pombe inaongeza sana uwezekano wa kupata saratani hasa zile za
koo, kinywa, ini na matiti.
Uzito Uliozidi kiasi unamweka pia mtu kwenye hatari ya kupata magonjwa
mengi sugu, kama vile kisukari, msukumo mkubwa wa damu, magonjwa ya
moyo, figo, na saratani za matiti, kongosho na kizazi. Utaratibu mzuri
wa kula, husaidia kupunguza uzito au kuzuia ongezeko kubwa la mwili.
Virusi na Bakteria husababisha kansa ya ini, mdomo wa mji wa mimba,
mdomo, ngozi, tumbo, mfupa wa taya na kibofu cha mkojo. Tabia kama
kufanya mapenzi kwa mdomo, kama vile kunyonya uke au uume, huchangia
kuenea kwa saratani za iana hiyo.
Ni nini kifanyike kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa huo?
Ni nini kifanyike kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa huo?
Wataalamu wanashauri kwamba hatari ya kupatwa na kansa inaweza kupungua
kwa kubadilisha muundo wa maisha ya mtu binafsi, kwa mfano kujiepusha
na uvutaji wa sigara, kujiepusha kukaa juani kwa muda mrefu, kula lishe
bora na kufanya mazoezi mara kwa mara.
Aidha, vyakula vitokanavyo na mimea ni kinga nzuri ya kuzuia saratani.
Kutumia zaidi vyakula vitokanavyo na mimea husaidia kuondoa uwezekano wa
kupata saratani za aina mbalimbali. Inashauriwa kula angalau vipimo
vitano vya mboga mbalimbali kwa siku.
Hakikisha katika kila mlo unaotumia kunakuwa na nafaka zisizokobolewa
kama vile unga wa ngano usiokobolewa sana, unga wa dona, mchele wa
brauni, ulezi na kadhalika na aina mbalimbali za mikunde kama vile
maharage, kunde, choroko na mbaazi.
Mazoezi ya mwili yanapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Inashauriwa kufanya mazoezi ya mwili ya wastani kama vile kutembea haraka haraka angalau dakika 30 kila siku, na mwili ukishazoea, unashauriwa kuongeza hadi kufikia dakika 60 kila siku.
Kama unafanya mazoezi ya nguvu sana, basi iwe angalau dakika 30 kila siku. Punguza sana mtindo wa maisha ambao unakufanya uketi bila mazoezi kama vile kuangalia televisheni kwa muda mrefu.
Mazoezi ya mwili yanapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Inashauriwa kufanya mazoezi ya mwili ya wastani kama vile kutembea haraka haraka angalau dakika 30 kila siku, na mwili ukishazoea, unashauriwa kuongeza hadi kufikia dakika 60 kila siku.
Kama unafanya mazoezi ya nguvu sana, basi iwe angalau dakika 30 kila siku. Punguza sana mtindo wa maisha ambao unakufanya uketi bila mazoezi kama vile kuangalia televisheni kwa muda mrefu.
Tumia nafasi zote zilizopo za kuzoeza mwili kama vile kupanda ngazi
badala ya kutumia lifti, kusaidia kazi za nyumbani, kutembea kwenda
sokoni au dukani kama si mwendo mrefu na kadhalika.
Ni nini dalili za ugonjwa wa kansa?
Kwa kawaida saratani huanza taratibu, na huchukua muda mrefu kuonyesha
dalili zake zote. Aidha, dalili za awali haziambatani na maumivu yoyote,
hivyo kusababisha wagonjwa wengi kuchelewa kutafuta matibabu.
Magonjwa mengi ya saratani hutibika yakigundulika mapema. Shirika la
Afya Ulimwenguni (WHO), linaema asilimia 30 ya saratani zinaweza
kuzuilika. Hivyo ni muhimu kwa kila mtu kumuona mapema mhudumu wa afya
kila anapoona dalili zisizo za kawaida katika mwili wake, kama vile
dalili za kutokwa na damu ukeni kwa mwanamke baada ya kufanya tendo la
ndoa, baada ya kukoma mzunguko wa hedhi, au nje ya mzunguko wa hedhi.
Kukojoa mara nyingi zaidi ya kawaida au mkojo kutoka kwa shida; uvimbe
wa zaidi ya wiki tatu shingoni, kwapani, tumboni, ngozi au matiti;
kubadilika kwa kawaida ya kupata choo (kufunga choo); matiti kubadilika
umbile, uvimbe, ngozi au kutoa maji maji.
Kukohoa au sauti ya kukwaruza kwa zaidi ya wiki tatu; shida au maumivu wakati wa kumeza chakula au vinywaji; kutokwa na damu kwenye choo, mkojo, makohozi au pua; kutokwa na ute, maji maji au usaha ukeni; uchovu bila kufanya kazi; kupungua uzito ghafla bila sababu na kukosa hamu ya kula chakula.
Kukohoa au sauti ya kukwaruza kwa zaidi ya wiki tatu; shida au maumivu wakati wa kumeza chakula au vinywaji; kutokwa na damu kwenye choo, mkojo, makohozi au pua; kutokwa na ute, maji maji au usaha ukeni; uchovu bila kufanya kazi; kupungua uzito ghafla bila sababu na kukosa hamu ya kula chakula.
Jinsi ya kudhibiti kabisa kansa
Ikiwa kansa au saratani ishatokea na kuanza kusambaa mwilini, mambo
muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ili kudhibiti usambaaji huo ni pamoja na
kutibiwa kwa kufanya upasuaji, tibakemo (matibabu kwa dawa); kupata
matibabu kwa njia ya eksirei (matumizi ya mnururisho wa kuweka ioni ili
kuua seli za kansa na kunywea uvimbe); kupata matibabu ya tiba maradhi;
kupata matibabu ya monokloni ya kingamwili au njia nyingine.