WIKI
iliyopita tulieleza matatizo ya fangasi sehemu za siri na jinsi
wanavyowasumbua waliokumbwa na maradhi haya, tunaeleza ni wanawake gani
hupatwa na tatizo hili. Leo tunaendelea kuwaelimisha na tunaanza
kufafanua wale wanaopatwa na ugonjwa huu, endelea:
Wengine wanaopatwa na fangasi hawa sehemu za siri ni wale wanaotumia
sana dawa za kuua bakteria (antibiotics, steroids) ambazo zina tabia ya
kushusha kinga ya mwili.Mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini kwa
mwanamke husababisha mabadiliko katika sehemu za siri na hivyo kufanya
kuwepo kwa ukuaji wa kasi wa fangasi hawa.
Ujauzito (kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na
kupungua kwa kinga ya mwili) huweza kusababisha mtu kuwa na fangasi
hawa. Hata hivyo, ieleweke hapa kuwa si kila mjamzito hupatwa na
maambukizi haya.
Matumizi ya dawa za kupanga uzazi (vidonge vya majira) au mtu kuwa na
upungufu wa kinga mwilini kutokana na magonjwa sugu kama kisukari,
saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya Mononucleosis na nk,
husababisha mtu kupata maambukizi ya fangasi hawa.
Wengine wanaoweza kuambukizwa fangasi hawa ni wale wenye ugonjwa wa
Ukimwi (HIV/AIDS), wanaopata matibabu ya homoni (hormonal replacement
therapy) kutokana na sababu mbalimbali au wenye matibabu ya kusaidia
kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazi (infertility treatment),
wenye utapia mlo (malnutrition), wenye kuvaa nguo au mavazi yanayoleta
joto sana sehemu za siri kwa muda mrefu kama nguo za kuogelea
(swimwear), nguo za ndani (chupi) zilizotengenezwa kwa kitambaa aina ya
nailoni, nguo za ndani zinazobana sana n.k.
Au wale wanaojamiiana kwa njia ya kawaida mara tu baada ya kujamiana
kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) au matumizi ya vilainishi vyenye
glycerin wakati wa kujamiana pia yamehusishwa na maambukizi haya.
Wanawake wenye umri wa miaka kati ya ishirini na thelathini wapo kwenye
hatari kubwa ya kupata maambukizi haya wakati wale ambao wameshaacha
kupata hedhi au wale ambao hawajaanza kupata hedhi kabisa hawako kwenye
hatari kubwa.