Ni kinga dhidi ya magonjwa ya moyo, presha, vidonda vya tumbo, saratani ya figo, kukosa choo
Ndizi
mbivu ni tunda ambalo linafahamika na kila mtu, lakini sina hakika kama
watu wengi wanafahamu umuhimu na faida za tunda hili ambalo
linapatikana kirahisi sana nchini. Bei yake ni kati ya shilingi 50 na
150 tu, kiwango cha pesa ambacho kila mtu anaweza kukimudu.
Iwapo
ulikuwa hujui umuhimu wa kula ndizi mbivu, leo utalazimika kubadili
mtizamo wako na kuziangalia ndizi kama tunda muhimu katika kuupa nguvu
na kuulinda mwili wako dhidi ya maradhi hatari ambayo hayana tiba. Watu
wa michezo pia wanapaswa kuliona tunda hili kuwa ni muhimu sana katika
kuipa miili yao nguvu.
KINGA DHIDI YA SHINIKIZO LA DAMU NA MARADHI YA MOYO
Kwa
mujibu wa utafiti wa kisayansi, ndizi ni chanzo kikubwa cha Potassium,
madini ambayo ni muhimu sana katika kuweka shinikizo la damu mwilini
katika hali yake ya kawaida (Normal Blood Pressure), na ufanyaji kazi
mzuri wa moyo. Kwa kuwa ndizi moja ina wastani wa 467mg za madini aina
ya Potasiamu na 1mg ya sodiamu (chumvi), ndizi moja tu kwa siku inaweza
kukupa kinga ya maradhi ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo.
Ukweli
kuhusu vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya Potasiamu katika
kushusha shinikizo la damu mwilini, umethibitishwa na tafiti nyingi za
kisayansi. Kwa mujibu wa jarida moja la masuala ya afya nchini Marekani,
zaidi ya Wamarekani 40,000 wa kike na kiume, walifanyiwa utafiti kwa
muda wa miaka minne na ikagundulika kwamba watu wanaokula vyakula vyenye
kiasi kikubwa cha madini ya Potasiamu na kirutubisho cha Fiber
(Ufumwele), wako katika hatari ndogo ya kupatwa na kiharusi.
Aidha,
utafiti mwingine uliofanywa na taasisi moja ya masuala ya tiba
ijulikanayo kama Archives of Internal Medicine, ya nchini Marekani, pia
ilithibitisha kwamba ulaji wa vyakula vyenye kiasi kikubwa cha ufumwele
(fiber) kama vile ndizi, husaidia sana kutoa kinga dhidi ya maradhi ya
moyo. Na katika suala hili, zaidi ya watu 10,000 walifanyiwa utafiti kwa
muda wa miaka 19.
KINGA DHIDI Y VIDONDA VYA TUMBO
Kwa
muda mrefu sana imethibitishwa kwamba ndizi ina virutubisho vyenye
uwezo wa kupambana na asidi tumboni hivyo kutoa kinga dhidi ya vidonda
vya tumbo (stomach Ulsers) na kutoa ahueni kwa mtu ambaye tayari
ameathirika. Katika utafiti mmoja, ilkibainika kwamba mtu akila
mchangayiko wa ndizi mbivu na maziwa freshi, huzuia utokaji wa asidi
tumboni inayosababisha vidonda vya tumbo.
Kwa mujibu wa utafiti
wa kisayansi juu ya suala hili, ndizi hutoa kinga na ahueni ya vidonda
vya tumbo kwa njia mbili. Mosi: virutubisho vilivyomo kwenye ndizi
huzipa uhai seli zenye kazi ya kutengeneza utandu ambao hutoa aina
fulani ya urojo (mucus) unaotumika kama kizuizi dhidi ya asidi tumboni.
Pili:
kuna virutubisho vingine kwenye ndizi ambavyo kwa kitaalamu
vinajulikana kama ‘Protease’ ambavyo husaidia kuondoa bakteria tumboni
ambao wanaelezewa kuwa ndiyo chanzo cha vidonda vya tumbo. Hivyo kama
wewe hujaptwa na vidonda vya tumbo, kwa kula ndizi mara kwa mara unajipa
kinga madhubuti na kama tayari umeathirika na vidonda, kwa kula ndizi
utajipa ahueni kubwa.
NDIZI KAMA TIBA KWA WENYE MATATIZO YA CHOO
Ndizi
ni muhimu sana katika kulainisha na kusafisha tumbo na kumuwezesha mtu
kupata choo. Mbali ya kusaidia upatikanaji wa choo kwa wenye matatizo
hayo, lakini pia hutoa ahueni kwa wagonjwa wa kipindupindu. Mtu
aliyepatwa na kipindupindu hupoteza kiasi kikubwa cha madini ya
Potasiamu, hivyo kwa kula ndizi ataweza kurejesha mwilini maidni yake
yaliyopotea na kuupa mwili nguvu yake.
UIMARISHAJI WA NURU YA MACHO
Wakati ulipokuwa mdogo, bila shaka uliwahi kuambiwa na mama kuwa mtu
akila karoti, atakuwa akiona vizuri. Bila shaka hakukosea, lakini sasa
ukiwa mtu mzima unaambiwa kwamba ulaji wa matunda, ikiwemo ndizi, ndiyo
kinga hasa dhidi ya matatizo ya kutokuona vizuri uzeeni. Utafiti wa hivi
karibuni unaonesha kwamba ulaji wa matunda kwa wingi kila siku,
hupunguza kwa asilimia 36 matatizo ya kutokuona vizuri kutokana na mtu
kuwa na umri mkubwa.
KINGA DHIDI YA SARATANI YA FIGO
Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa na Jarida la Kimataifa la
masuala ya Saratani (International Journal of Cancer) la nchini
Marekani, umeonesha kwamba ulaji wa mara kwa mara wa matunda halisi,
hasa ndizi mbivu, ni kinga madhubuti ya mwili. Zaidi ya wawake 50,000
wenye umri kati ya miaka 40 na 76 waliofanyiwa utafiti, ulionesha kuwa
wale waliokula wastani wa milo 2.5 ya matunda na mboga kila siku,
walipunguza hatari ya kupatwa na saratani ya figo kwa asilimia 40.
Baadhi
ya vitamini na madini yaliyomo kwenye ndizi ni pamoja na Vitamini B6,
Vitamin C, Potassium, Dietary Fibre na Mnganese. Hivyo utaona kwamba
tunda la ndizi ni muhimu kwa sababu limesheheni vitamini na madini
muhimu katika mwili wa binadamu. Kuanzia leo itazame ndizi kama tunda
muhimu sana katika ustawi wa afya yako na ni kinga dhidi ya maradhi
unayoweza kuyaepuka kesho kwa kula tunda hili kwa wingi leo!