Tatizo hili pia huitwa ‘Tilted Uterus’ au ‘Tipped Uterus’, hapa kizazi hugeuka kwa nyuma. Hii ni tofauti katika hali ya kawaida ya kuangalia kwa mbele. ‘Anteverted’ ambayo wanawake wengi wapo hivyo, kizazi hulalia kibofu cha mkojo na upande wa mbele hujikunja kidogo.
Kwa mujibu wa takwimu, mwanamke mmoja kati ya watatu au watano, wana aina hii ya kizazi kilichogeuka na wengine hugeuka kabisa kwa nyuma.
Baada ya uchunguzi wa kina, daktari atagundua aina ya mgeuko kwa kuwa zipo aina mbalimbali na hutofautiana katika ukali wa tatizo.
Matatizo haya huwatokea zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa lakini pia inaweza kuwa ni hali ya kuzaliwa nayo.
CHANZO CHA TATIZO
Kama tulivyoona, hali hii inaweza kuwa ni ya kawaida kwa baadhi ya wanawake kutokana na kuzaliwa hivyo lakini inaweza kuwa tatizo kwa baadhi ikiwa inasababishwa na mambo yafuatayo;
Upasuaji wa kizazi wakati wa kuzaa au kuondoa uvimbe, kushikamana kwa kizazi kutokana na maambukizi sugu ya kizazi au baada ya upasuaji wa kizazi au viungo jirani na kizazi ambapo tabaka la ndani la kizazi kuwa kwa nje, uvimbe kwenye kizazi, maambukizi sugu katika mfumo wa kizazi. Chanzo kingine ni kuzaa kwa njia ya kawaida.
DALILI ZA TATIZO
Kugeuka kwa kizazi ni tatizo ambalo mwanamke hawezi kuligundua mara moja hadi afanyiwe uchunguzi wa kina ndipo huthibitishwa.
Pamoja na kulalamika kutoshika ujauzito kutokana na kugeuka kwa kizazi ambapo chanzo chake kinaweza kuwa maambukizi ya kizazi ‘PID’ au kushikamana kwa kizazi, uvimbe na mengineyo ambayo tayari tumeshaona.
Mwanamke hulalamika pia maumivu wakati wa tendo la ndoa, maumivu ya tumbo chini ya kitovu mara kwa mara, maumivu ya kiuno, maumivu makali wakati wa hedhi na kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi.
TATIZO LA KUTOKUSHIKA UJAUZITO
Mwanamke ambaye amezaliwa hivyo kwamba kizazi chake kimegeuka huwa hakuna shida katika suala la kushika ujauzito, ila kwa yule ambaye kizazi kimegeuka kutokana na matatizo kama upasuaji, uvimbe, maambukizi, kasoro za tabaka la ndani la kizazi anaweza kupata tatizo hili kwa kiasi kikubwa kutokana hasa na mirija au njia za uzazi kuziba.
TATIZO WAKATI WA UJAUZITO
Wanawake wajawazito wenye tatizo hili la kugeuka kizazi hupatwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu wakati wa ujauzito, kadiri mimba inavyokua hubana kibofu cha mkojo na kusababisha maumivu wakati wa kukojoa au mkojo kutoka kwa shida katika kipindi hiki cha ujauzito.
Kwa hiyo unashauriwa kama una tatizo hili uwahi haraka hospitali kwa uchunguzi wa kina na tiba.
UCHUNGUZI
Uchunguzi hufanyika katika Hospitali za Wilaya na Mikoa kwa madaktari wa akina mama, vipimo mbalimbali hufanyika kutegemea na jinsi tatizo litakavyogundulika.
Vipimo vya ‘Ultrasound’, ‘Pelvic Examination’, ‘Speculum Examination’ ndivyo vinaweza kufanyika na vingine inategemea jinsi daktari atakavyoona inafaa.Mwanamke anaweza kwenda hospitali kutokana na sababu mbalimbali zinazohusiana na tatizo hili, mfano maumivu ya kiuno, maumivu chini ya tumbo, kuvurugika kwa hedhi, kutoshika mimba. Daktari ataona vipimo gani atafanyiwa.
 
Top