Safari ya ujauzito ya miezi 9 ndio imeanza, wakati huu yamkini umeshapima na kuthibitishamimba yako. Mimba inapotungwa huleta mabadiliko mbalimbali ya kimwili na kisaikolojia kutokana na homoni za uzazi kuzalishwa kwa wingi zaidi. Mabadiliko haya hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke, na pia kwa mwanamke mmoja katika nyakati tofauti.
Kipindi hiki cha miezi 3 ya mwanzo ya ujauzito hujulikana kama first trimester na mjamzito huweza kupata mabadiliko yafuatayo ambayo huwa pia kama dalili za mwanzo za ujauzito;
Kichefuchefu Na Kutapika Hasa Wakati Wa Asubuhi
Kichefuchefu na kutapika ni moja ya hali zinazojitokeza wakati wa mwanzo wa mimba. Kutapika huku huwa hasa wakati wa asubuhi na kuacha kadri siku inavyoenda. Hutokea kwa wanawake wengi wakati wa mwanzo wa ujauzito, na hupungua kadri mimba inavyokua. Ikiwa unatapika sana karibu siku nzima kila kitu unachokula basi onana na daktari mapema.
Kukosa Hedhi
Kukosa damu ya hedhi ni ishara mojawapo kuu ya ujauzito. Mimba inapotungwa, homoni huzuia ukuta wa mji wa mimba kubomoka na hivyo hedhi haitokei. Mara chache unaweza kutokwa na damu kidogo (matone kidogo kwenye nguo za ndani kwa siku moja au mbili). Kupata hedhi ya kawaida au kutokwa damu nyingi wakati wa ujauzito huashiria hatari ya ujauzito kutoka, hivyo ni muhimu kwenda hospitali mapema.
Kutokwa na Damu Kidogo Ukeni
Unaweza ukatokwa damu kidogo ukeni (matone kwenye nguo za ndani) kwa siku moja au mbili halafu ikaacha. Hutokea kwa baadhi ya wanawake kutokana na kiinitete (embryo) kujipandikiza katika mji wa uzazi. Hali hii ni ya muda mfupi na damu hutoka kidogo sana, na pia hutokea kwa baadhi ya wanawake.
Hali ya Kuchoka Haraka Zaidi ya Kawaida
Katika kipindi hiki cha mwanzo cha ujauzito, unaweza ukawa unapata hali ya uchovu mara kwa mara. Na hii inaweza kuwa uchovu wa kawaida au kuchoka sana zaidi ya kawaida (ukilinganisha na kipindi ambacho hakuwa na ujauzito).
Kukojoa Mara kwa Mara.
Miezi ya mwanzo ya mimba, tumbo la uzazi huanza kukua na hivyo hukandamiza kibofu cha mkojo (kwa sababu mji wa mimba upo juu ya kibofu kidogo). Hali hii hufanya kibofu kijae mapema na hivyo kuleta hali ya kukojoa mara kwa mara.
Kukosa Hamu kwa Baadhi ya Vyakula
Kutopenda aina fulani ya vyakula, vinywaji na baadhi ya harufu za vitu huweza kutokea kwa mjamzito. Mara nyingi hutokana na mabadiliko ya kihomoni mwiIini. wakati mwingine unaweza kuvutiwa na aina fulani za vyakula au vitu kama barafu au udongo. Kuwa makini kupata vyakula vyenye lishe, epuka kula vitu kama udongo.
Kununa na Kukasirika (mood changes)
Hizi moods hubadilika mara kwa mara wakati mwingine .furaha, uchangamfu, na wengine inakuwa ni rahisi sana kumchukiza hata kwa kitu kidogo. Kuna wajawazito wengine hutokea kuwachukia wenzi wao pia. Hivyo ni muhimu kuwachukulia katika hilo.
Matiti Kuvimba na Kuuma
Mara nyingi mabadiliko ya kihomoni huchangia kuleta hali hii. Polepole matiti huanza kukua kujiandaa kutengeneza maziwa kwa ajili ya mtoto, mabadiliko haya huchangia kuleta hali ya matiti kuvimba na kuuma.
Mabadiliko katika Hamu ya Kufanya Mapenzi
Na hili pia hutokea, ikitofautiana kati ya wakati na wakati. Kuna wajawazito au wakati mjamzito anakuwa na mihemko mikubwa ya kimapenzi na wakati mwingine inakuwa kinyume kabisa. Ingawa inaweza isiwe kwa kiasi kikubwa katika miezi hii 3 ya mwanzoni.
Mabadiliko ya Ngozi
Ingawa inaweza isikupate, mabadiliko ya ngozi hutokea hasa kutokana na mabadiliko ya kihomoni mwilini. Chunusi huweza kutokea.
Mabadiliko haya hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke, hata siku kwa siku. Ukipata dalili zozote zinazokupa wasiwasi, onana na daktari wako haraka.