Kipindupindu ni ugonjwa wa kuharisha na kutapika unaosababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoitwa kwa lugha ya kitaalam “Vibrio cholera”.
CHANZO CHA UGONJWA
• Vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu.
• Vimelea vilivyomo kwenye kinyesi cha mtu bila yeye binafsi kuonyesha dalili zozote za ugonjwa.
DALILI ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU.
Mgonjwa wa Kipindupindu huwa na dalili zifuatazo:
• Kuharisha mfululizo au mara kwa mara bila tumbo kuuma ambako kunaweza kuambatana na kutapika.
• Kinyesi au matapishi huwa ya maji maji yasiyo na harufu, yanayofanana na maji yaliyooshewa mchele.
• Kusikia kiu sana, macho kudidimia na ngozi kusinyaa ambavyo hutokana na upungufu wa maji mwilini.
• Kuishiwa nguvu, kuhema haraka haraka na kulegea. Hali hii hutokana na upungufu wa maji na madini mwilini.
KIPINDUPINDU KINAVYOENEA.
• Kula chakula au kunywa kinywaji chochote kilicho na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu kwa mfano:-
- Kunywa maji yasiyochemshwa.
- Kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira ambayo siyo safi.
- Kula matunda yasiyooshwa kwa maji safi na salama.
- Kunywa pombe za kienyeji zilizoandaliwa katika mazingira machafu au kunywea katika vyombo vichafu.
- Kula mboga za majani, kachumbari na saladi bila kupikwa au kuziosha kwa maji safi na salama.
• Kula chakula au kumlisha mtoto bila kunawa mikono kwa sabuni na maji safi na salama yanayo tiririka.
• Kuosha au kuhudumia mwili wa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa kipindupindu bila kujikinga.
• Kunawa mikono kwenye chombo kimoja kwa mfano ndani ya bakuli au beseni kabla ya kula chakula.
• Kutotumia choo au utupaji ovyo wa kinyesi.
• Kutonawa mikono baada ya kutoka chooni.
• Kuweka mazingira katika hali ya uchafu mfano kutupa taka ovyo bila kuzingatia kanuni za afya..
• Kula vyakula vilivyopoa na visivyofunikwa.
• Kutiririsha maji ya chooni ardhini na hivyo kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji na chakula.
· Inzi huchangia kueneza ugonjwa wa kipindupindu kwa tabia zake za kutua chooni kwenye kinyesi, uchafu na hata vyakula na vinywaji.
MADHARA YA KIPINDUPINDU
• Hofu miongoni mwa jamii katika sehemu yenye mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
• Kifo kutokana na ukosefu wa maji na madini mwilini baada ya kuharisha na kutapika sana.
• Kushuka kwa uchumi kutokana na familia/jamii kuacha shughuli za uzalishaji mali ili kumuhudumia mgonjwa na kushiriki katika misiba.
• Serikali hutumia fedha nyingi kwa ajili ya dawa, posho kwa watumishi katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
JINSI YA KUJIKINGA NA KIPINDUPINDU
• Kujenga choo bora na kukitumia Ipasavyo
• Kufunika tundu la choo na kufunga mlango baada ya matumizi yake.
• Kunawa mikono kwa maji safi na salama kwa kutumia sabuni baada ya:.
- kutumia choo.
- kumtawaza mtoto na kabla ya kula au kumlisha motto.
• Kula chakula kikiwa bado moto na kufunika chakula kilichoandaliwa tayari kwa kuliwa.
• Kunywa maji yaliyochemshwa na kuhifadhiwa katika chombo kisafi na salama.
• Kusafisha vyakula vinavyoliwa vibichi (kama vile matunda na mboga) kwa kutumia maji safi na salama yanayotiririka.
• Kuhakikisha usafi wa mazingira ya vilabu/baa, wahudumu na vyombo vitumikavyo. Pombe za kienyeji ziandaliwe kwa maji yaliyochemshwa.
• Weka mazingira katika hali ya usafi.
· Kumbuka, kuchuja maji yaliyochemshwa kunaweza kuchafua maji kwa kuingiza vimelea.Hivyo, chuja maji kabla ya kuyachemsha.
KUHUDUMIA MGONJWA
Mgonjwa wa kipindupindu hupoteza maji mengi na madini muhimu mwilini anapoharisha na kutapika. Ili kuokoa maisha ya mgonjwa ni muhimu kuchukua hatua zifuatazo:
• Mpe mgonjwa dawa ya mchanganyiko wa sukari na chumvi(ORS), maji, uji mwepesi, supu nk. mara kwa mara.
• Mpeleke mgonjwa haraka iwezekanavyo katika kituo cha afya/zahanati/ hospitali au kituo cha kutibu kipindupindu kilicho karibu nawe.
• Matapishi na kinyesi cha mgonjwa ni hatari kwa afya yako. Kwa hiyo nguo na vitu vingine vilivyochafuliwa na mgonjwa vilowekwe kwenye kemikali maalumu (mfano Jik) au vichemshwe ili kuua vimelea vya kipindupindu na kasha visafishwe kwa sabuni.
• Ndugu waliokuwa wakiishi na mgonjwa au wale wanaomhudumia wahakikishe wanapata dawa za kinga dhidi ya kipindupindu.
Angalizo:
Ni lazima wakati wote kuwa msafi ili kuzuia vimelea vya ugonjwa visiingie kinywani kwako kwa njia zilizotajwa hapo juu.
Tahadhari:
Maiti ya mgonjwa wa kipindupindu ni hatari, usijishughulishe na kuosha maiti hiyo bali izikwe haraka kwa kufuatwa ushauri wa wataalam wa afya.