Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni kutegea sikio kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Leo tutazungumzia madhara ya kuvuta sigara, tabia ambayo imezoeleka na watu wengi ingawa ina madhara mengi. Ili kuweza kuyajua madhara hayo kwa undani, usiondoke kando ya redio yako hadi mwisho wa kipindi hiki.

Kemikali zenye madhara zilizo kwenye sigara
Ufutaji sigara huathiri mwili kwa njia tofauti na madhara yake ni makubwa kiafya. Inakadiriwa kuwa, hadi sasa kumegunduliwa kemikali zipatazo 7,000 katika moshi wa sigara ambapo 250 kati ya hizo ni sumu na 70 zinasababisha kansa. Mvutaji mdogo hutumia nusu ya pakiti ya sigara kwa siku na kujikuta akiathiri mwili wake kwa kemikali hizi mara 3500 kwa mwaka. Mada na kemikali zilizo kwenye sigara huathiri karibu kila kiungo mwilini kuanzia seli hadi mfumo wa kulinda mwili.

Kemikali zilizoko kwenye moshi wa sigara huingia katika mapafu na kuenea katika mwili mzima na kusababisha madhara makubwa kwa njia mbalimbali. Ingawa mada hizo haribifu zilizoko kwenye moshi wa sigara ni nyingi, lakini tatu ni hatari zaidi zikilinganishwa na nyingine. Mada hizo ni nikotini, carbon monoxide na tar. Nicotine huufikia ubongo sekunde 7 hadi 10 baada ya moshi wa sigara kuvutwa na kemikali hiyo hutapakaa katika sehemu nyingi za mwili hata katika maziwa ya mama. Nikotini ni kemikali sumu ambayo kwa muda mrefu sana inatumiwa kama dawa ya kuuwa wadudu na sumu ya panya. Inachukua nafasi ya pili kama sumu kali kabisa kutokana na athari yake mbaya kwa mwili wa binadamu.

Tar ni kemikali inayosababisha kansa mwilini inayopatikana katika tumbaku ambayo huharibu jeni muhimu zinazozuia ukuaji holela wa seli ili zisiwe za saratani. Hii ni katika hali ambayo Carbon monoxide ni gesi yenye madhara inayopatikana katika moshi wa sigara ambayo hujishikiza katika hemoglobin kwenye seli nyekundu za damu na kuzizuia zisiweze kubeba vyema oksijeni kama inavyotakiwa. Suala hilo husababisha mtu apatwe na dalili za kuwa na sumu ya gesi hiyo mwilini.
Tunapaswa kujua kuwa, kuvuta sigara huwasababishia maradhi mbalimbali wenye kuvuta sigara kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na wasiuovuta. Miongoni mwa maradhi hayo ni magonjwa ya moyo, kiharusi, kansa ya mapafu, matatizo katika mfumo wa kupumua yanayojulikana kama COPD na mengineyo.

Magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na uvutaji sigara
Nchini Marekani pekee kuvuta sigara kunakadiriwa kusababisha vifo karibu vya watu laki 5 kwa mwaka. Duniani kote watu milioni 5 hupoteza maisha yao kila mwaka kutokana na kuvuta sigara ambapo kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka na kufikia vifo milioni 8 ifikapo mwaka 2020.

Wataalamu wanasema kuwa, kama watu wataacha kuvuta sigara vifo vitapungua kwa theluthi moja nchini Marekani. Sigara pia husababisha kwa karibu asilimia 90 ugonjwa wa kansa ya mapafu, ambapo huwapata zaidi wanaume kuliko wanawake.

Uvutaji sigara husababisha madhara mbalimbali mwilini miongoni mwayo ni: Kuharibu utando mlaini katika njia za hewa. Kwa kawaida njia ambayo pumzi hupita hufunikwa kwa utando laini ambao huzuia vumbi linaloingia pamoja na hewa kwenye mapafu.

Kemikali zinazopatikana katika moshi wa sigara huganda katika utando huu na kusababisha njia hiyo kuwa nyembamba kutokana na kuongezeka takataka na kemikali dani yake, na hivyo kumfanya mvutaji sigara apate shida ya pumzi.

Sigara pia husababisha au kushashiisha vidonda vya tumbo, kwa kuwa kemikali zilizoko kwenye sigara huchochea utengenezaji wa tindikali tumboni.

Uvutaji sigara pia kusababisha matatizo katika mfumo wa upumuaji ambapo wavutaji hupata shida katika koo na mapafu hivyo kupata kifua mara kwa mara na maumivu na mwishowe kupata madhara makubwa katika mfumo mzima wa upumuaji kutokana na kuharibika kwa alveoli za mapafu (Emphysema). Hii ni kwa sababu harufu kali ya moshi huharibu alveoli ndogo ndogo katika mapafu na kupunguza kwa kiasi kikubwa eneo ambalo oksijeni hukutana na damu.

Hali hii hutokea taratibu sana na kwa muda mrefu.
Wavutaji wote huwa na tatizo hilo kwa kiwango tofautia, lakini kwa kuwa nje ya mwili kuna oksijeni ya kutosha, watu wengi huwa hawajui kwamba wana hali hiyo. Pia kwa kuwa mapafu yana takriban alveoli milioni 300 hivyo ni vigumu kugundua hali hii na baadhi hujua suala hilo pale wanapofanya mazoezi au kupanda ngazi na kuhisi ugumu wa kupumua.

Mbali na kupata pneumonia na asthma, wafutaji sigara pia huwa na udhaifu wa mifupa (Osteoporosis. Hii ni kwa sababu katika moshi wa sigara kuna mada ijulikanayo kama cadmium inayoweza kusababisha matatizo katika mifupa kwa kuwa hupunguza asilimia 30 ya calcium katika mifupa.

Kwa wanawake, tabia ya kuvuta sigara huzuia ufanisi wa homoni ya estrogen na kitu chochote kinachozuia estrogen kufanya kazi ipasavyo husababisha udhaifu katika mifupa unaosababisha maumivu ya mara kwa mara ya mifupa. Hayo si madhara pekee yanayowapata wanawake wenye kuvuta sigara bali pia, tabia hiyo husababisha wawe wanawahi kumaliza hedhi yaani Menopause.

Kwa kawaida wanawake hufikia mwisho wa kupata siku zao wanapokuwa na umri wa miaka 45 hadi 55, hali ambayo pamoja na mambo mengine humaanisha pia kuwa hawawezi tena kubeba ujauzito. Lakini wanawake wanaovuta sigara hufikia menopause miaka mitano mapema zaidi ya wasiovuta.

Madhara mengineyo ya sigara.
Sigara pia huwaathiri wanawake wajawazito na wajawazito wenye kuvuta sigara huwa katika hatari kubwa ya mimba kutoka, mtoto kufia tumboni, kichanga kuzaliwa na uzito mdogo au hata mtoto kufa mapema pindi atakapozaliwa.Wataalamu wanasema kuwa, kuvuta sigara wakati wa mimba kunapunguza uwezo wa kuzaa watoto wa kiume kwa kuathiri jeni muhimu za umbo la kiume ambapo gameti za kiume hutengenezwa.

Tayari imeshajulikana kuwa kuvuta sigara kunaathiri uzazi wa watoto wa kiume hapo baadaye, lakini bado haijajulikana ni vipi suala hilo hutokea. Si hayo tu bali sigara pia hupunguza uwezo wa seli nyekundu kubeba oksijeni katika damu kama nilivyoashiria huko nyuma. Madhara mengine ya hatari ya kuvuta sigara ni kupata saratani za aina mbalimbali. Imeonekana kuwa, wanaovuta sigara licha ya kukabiliwa na hatari ya kupata kansa ya kifua, pia huweza kupata saratani za ina nyinginezo kama za ngozi, koo, utumbo, kibofu na pia mdomo.

Kemikali za sumu zilizoko katika tumbaku ya sigara huharibu vinasaba (DNA) vya mwili wa binadamu dakika chache tu baada ya mtu kuanza kuvuta sigara. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, kemikali hizo zinazoitwa Polycylic Aromatic Hydrocarbons (PAHs) husababisha DNA ziharibike na kuongeza uwezekano wa mtu kupata kansa.

Kupungukiwa na vitamin ni tatizo jingine linalowapata wavuta sigara, kwani sigara husababisha upungufu wa virutubisho muhimu mwilini na hasaVitamini C.

Tatizo hilo hutofautiana kati ya wavutaji sigara kwa kutegemea kiasi cha sigara wanazovuta kwa siku. Pia uvutaji sigara unaweza kusababisha kisukari, kwani nikotini iliyopo kwenye moshi wa sigara huchochea sukari katika damu na kusababisha kisukari aina ya pili yaani kisukari kisicho cha kuzaliwa.

Kuvuta sigara kuna madhara kwa kila mtu lakini kwa watu wenye kisukari au wanaokabiliwa na hatari ya ugonjwa huo, uvutaji sigara huwasababishia madhara makubwa kiafya. Wataalamu wanatueleza kuwa, wagonjwa wa kisukari ambao wanavuta sigara, kiasi cha glucose kwenye damu zao huwa juu, hali ambayo husababisha ugonjwa huo usiweze kudhibitiwa kwa urahisi na kuwafanya wagonjwa wakabiliwe na hatari ya kupata madhara makubwa kama vile upofu, uharibifu wa neva, figo na matatizo ya moyo.

Watoto wadogo wanaovuta sigara huweza kupata ugonjwa wa MS
Watu ambao wanaanza kuvuta sigara wakiwa katika umri wa kabla ya miaka 17, wako katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa Multiple Sclerosis au MS.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika mkutano wa 61 wa kila mwaka wa Taasisi ya Magonjwa ya Mishipa ya Fahamu ya Marekani, zaidi ya asilimia 32 ya wagonjwa wa MS walikuwa wale walioanza kuvuta sigara katika umri mdogo. Utafiti huo umeonyesha kuwa, wanaovuta sigara katika umri mdogo wana uwezekano wa kupata ugonjwa wa MS mara 2.7 zaidi ya wengine. Utafiti huo haukuonyesha kuwepo hatari hiyo kwa wale wanaoanza kuvuta sigara wakiwa na umri mkubwa.

Ugonjwa wa multiple sclerosisi ni ugonjwa wa mfumo wa kinga ya mwili ambao hutokea pale mfumo huo unaposhambulia mfumo wa kati wa fahamu (central nervous susytem), hali ambayo hupelekea seli za fahamu kushindwa kuwasiliana.

Ugonjwa huo mara nyingi huanza kwa kupoteza hisia mbalimbali mwilini kama kuona, kuhisi, kushindwa kutembea, kupumua na mwishowe kupooza mwili mzima.

Ni vyema kujua kuwa, mbali na madhara mengine mengi, uvutaji sigara unasababisha kwa asilimia 90 vifo vinavyotokana na kansa ya mapafu.

Idadi ya watu wanaopatwa na kansa ya mapafu inaongezeka kila siku duniani na kuzidisha vifo vinavyotokana na saratani nyinginezo. Kwa kawaida kansa ya mapafu huwapata watu wanapokuwa na umri wa miaka 45, na wakati mtu anapopimwa na kukutwa na ugonjwa huo kwa kawaida huwa tayari umeshasambaa mwilini mwake. Saratani ya mapafu inahusiana moja kwa moja na uvutaji sigara.

Hatari ya kupatwa na kansa ya mapafu inaambatana moja kwa moja na idadi ya sigara mtu anazovuta. Kwa sababu hiyo tunapaswa kuacha tabia ya kuvuta sigara na kufanya juhudi kubwa kuwazuia watoto wetu na wanajamii kwa ujumla kuacha tabia hiyo hatari. Katika kipindi chetu kijacho pamoja na mambo mengine tutazungumzia njia zinazosaidia kuacha sigara. Hadi wakati huo, daima tuzitunze afya zetu.
 
Top