Image result for mjamzito image
LISHE bora ni muhimu kwa kila mtu, mwanamke na mwanaume na watoto wanatakiwa wapate lishe bora. Mwanamke aliye katika umri wa kuzaa anahitaji apate lishe bora ili kumwezesha kupata ujauzito pale anapohitaji.

Haitakiwi mwanamke atafute ujauzito kwa muda mrefu. Endapo umetafuta ujauzito kwa kipindi cha mwaka mmoja au zaidi na hujafanikiwa basi kuna tatizo. Tatizo la kutopata ujauzito linaweza kuwa kwa mwanamke au mwanaume.

Vyanzo vya matatizo ya kutopata ujauzito kwa mwanamke vipo vingi mfano matatizo ndani ya kizazi, mirija na vichocheo au homoni.

Miongoni mwa chanzo cha tatizo hasa katika mfumo wa homoni ni kutopata lishe inayofaa. Matatizo haya ya lishe yanaweza kuathiri hata uzalishaji wa mbegu kwa mwanaume.

Matatizo ya mirija na kizazi inaweza kuwa maambukizi ya muda mrefu, uvimbe na kubadilikabadilika kwa siku za hedhi.

Mwanamke mwenye matatizo kwenye kizazi na mirija hulalamika maumivu chini ya tumbo kwa muda mrefu, maumivu wakati wa tendo la ndoa, kutokwa na uchafu au majimaji ukeni.

Matatizo kwa mwanaume pia husababisha mwanamke asiweze kushika mimba. Mwanaume anaweza kukosa au kupungukiwa nguvu za kiume, kufanya tendo la ndoa na kushindwa kutoa manii, kutoa manii na kutokuwepo na mbegu za kiume au kutoa mbegu za kiume zisizo na sifa mfano hazitembei, goigoi au zina kasoro.
Aina za vyakula.

Vyakula mchanganyiko ni muhimu ambavyo vina vitamin za kutosha. Kila vitamin tutakayokuja kuiona ina umuhimu wake. Lishe bora huchangia mfumo wa homoni mwilini na kumuwezesha mwanamke aweza kupata upevushaji wa mayai.

Dalili za upevushaji ni kupata ute wa uzazi ambao ni ute mwepesi na unavutika na ute mzito. Katika matoleo yajayo tutaona vipindi ambavyo ute huu unatoka na vipindi ambavyo unaweza kushika mimba kwa hiyo usikose kusoma kila Ijumaa.

Lishe bora pia inawezesha kutoa mbegu bora na zenye sifa kwa mwanaume. Mwanamke anapotarajia kupata ujauzito unatakiwa uwe na kiwango cha kutosha cha vitamin B ambazo ni muhimu kwa mfumo wa homoni, Folic Acid husaidia kuendeleza uzalishaji wa mayai ya uzazi, Vitamin C nayo kitaalam husaidia kusafisha mifumo ya uzalishaji mayai na kuyaweka sawa.

Vitamin hizi hupatikana katika vyakula mbalimbali pamoja na hizi nyingine pamoja na madini ambayo tutakuja kuziona.

Katika nchi zinazoendelea aina hizi hupatikana kama virutubisho ‘Supplements’ ambapo mtu hutumia kwa kiwango fulani na kwa muda fulani kutegemea na aina ya virutubisho.

Virutubisho hivi siyo tu kwa mwanamke bali hata kwa mwanaume.
Vyakula muhimu kwa uzazi
Vipo vyakula vingi sana lakini kwa leo tutaona baadhi na vingine tutaona siku zijazo.
AMINO ACIDS: Jamii hii ya chakula ni muhimu kwa uzalishaji wa mayai na hata mbegu za kiume. Hupatikana kwenye vyakula vya protin mfano nyama, maharage, kunde, choroko, njegere, soya na jamii zote za kunde na nyama aina zote pamoja na mayai.
VITAMINI A: Ni muhimu pia katika uzalishaji wa vichocheo vya uzazi  na kusaidia uzalishaji wa mayai na ute wa uzazi na kuboresha hamu ya tendo la ndoa.
Vitamini A hupatikana katika mayai, maembe, ndizi mbivu, mboga za majani kama mchicha, matembele, mnavu, kisamvu na majani ya maboga na jamii zake. Hupatikana pia katika maziwa na mafuta ya samaki.
Vitamini A pia ni muhimu hata wakati wa ujauzito na kwa watoto wadogo.
Vitamin B na Folic Acid

Vitamini B zipo aina nyingi takriban sita, hatutaweza kuchambua moja baada ya nyingine leo ila tutakuja kuona kwa undani baadaye na ni muhimu sana katika uzalishaji wa mayai ya uzazi na kuepusha kasoro kwa mtoto atakayezaliwa.

Vitamin B haiwezi kufanya kazi endapo mhusika atakuwa anavuta  sigara au anabwia ugoro, anakunywa pombe ya aina yoyote pia kama muda wote hayupo sawa kisaikolojia.

Vitamin C, Vitamini E na madini ya chuma pia vina umuhimu mkubwa katika uzazi, madini kama Magnesium husaidia ubora wa uzazi na kuzuia mimba kuharibika mara kwa mara.

Jamii ya vyakula hupatikana katika mayai ya kuku, mafuta ya kupikia yatokanayo na mbegu mfano alizeti, mawese na mengineyo, karanga, maparachichi, viazi vitamu na mboga za majani.

Madini ya chuma hupatikana katika nyama mfano maini, figo, moyo, mayai, samaki na dagaa, mbegu za mafuta mfano alizeti.

Epuka matumizi ya chai ya rangi, kahawa na uvutaji wa sigara unapotumia vyakula hivi vyenye madini ya chuma.

Madini ya magnesium ni muhimu na hupatikana katika mboga za majani, mtama, mchele ndizi. Magnesium huzuia mimba kuharibika mara kwa mara na kukaa vizuri baada ya kurutubishwa.
Ushauri
Matatizo mengi ya kiafya yanazuilika endapo watu watabadilisha mtindo wa maisha katika ulaji wa vyakula, vinywaji na matumizi ya vitu visivyo vya lazima kwa afya.
Ni vema katika kila mlo mnaokula kuhakikisha unapata mboga za majani na matunda.

 Source: GPL
 
Top