Usafi na Kinywa na utunzaji wa menoAssalamu aleykum wasikiliziaji wapenzi na karibuni katika kipindi kingine cha Ijuwe Afya yako. Kipindi ambacho hujadili masuala mbalimbali yanayohusu afya na tiba kwa lengo la kupata maarifa ya kuzitunza vyema afya na siha zetu. Katika kipindi cheti cha leo tutazungumzia usafi wa kinywa na umuhumu wake na jinsi utunzaji wa sehemu hiyo ya mwili unavyoathiri afya ya mtu kwa ujumla.  Karibuni.

Afya ya kinywa ina umuhimu mkubwa zaidi ya unavyoweza kufikiria na kwa ujumla inaweza kutoa ufahamu kuhusiana na jinsi afya yako ya mwili ilivyo. Kuelezewa uhusiano uliopo kati ya afya ya kinywa na afya ya mwili mzima kunasaidia kufahamu umuhimu wa kutunza kinywa na hasa meno na fizi. Kama zilizo sehemu nyingine za mwili, kinywa nacho kimejaa bakteria ambao wengi wao hawana madhara. Kwa kawaida mfumo wa kulinda mwili na utunzaji mzuri wa kinywa kama vile kupiga mswaki na kutumia uzi kuondoa uchafu katika meno kunaweza kudhibiti bakteria walioko kinywani wabakie katika hali ya kawaida na kutodhuru kinywa. Lakini bila kutunza vyema kinywa, bakteria hao wanaweza kusababisha maambukizo na kusababisha meno kuoza na maradhi ya fizi.
Afya ya kinywa inajumuisha siha na namna ya utunzaji wa sehemu zote za mdomo hasa meno na fizi. Mbali na kinywa kutuwezesha ipasavyo kula, kuzungumza na hata kuwa na muonekano mzuri wa uso, meno na fizi zinapaswa zisiwe zimedhurika na kuwa na matatizo kama vile meno kuoza, magonjwa ya fizi, kung'oka meno na mdomo kunuka. Kuoza meno na meno kuwa na matundu ni matatizo ya kinywa yanayoshuhudiwa sana miongoni mwa watu. Sababu zinazoweza kuzuia matatizo hayo ya meno ni kudumisha usafi wa kinywa, kupata fluoride ya kutosha na kutokula kwa wingi vyakula vinavyoweza kudhuru meno na kusababisha matundu.
Afya ya meno na kinywa kwa ujumla inahusiana na afya ya mwili mzima kwa njia tofauti. Kwanza kabisa uwezo wa kutafuna chakula na kukimeza ni muhimu ili mwili uweze kupata virutubisho muhimu vya kujenga mwili. Halikahalika kuwa na kinywa chenye matatizo kunaweza kuathiri namna mtu anavyozungumza na hata kujiamini kwake. Matatizo ya meno yanaweza kumsababishia mtu gharama kubwa ya matibabu na ukarabati wa meno.
Sababu zinazoweza kuathiri afya ya kinywa
Uimara wa meno na fizi unatofautiana kati ya mtu na mtu, na umbo la taya, mdomo, meno na hata kiasi cha mate. Hayo yote ni mambo muhimu yanayoweza kuainisha kwa nini baadhi ya watu meno yao yanaoza zaidi kuliko wengine. Baadhi ya meno yanaweza kuwa na vishimo na nyufa zinazoweza kuruhusu bakteri na tindikali kupenya kwa urahisi na baadhi ya wakati umbo la taya huweza kuzuia meno yasisafishike vizuri na kuondoa vyema uchafu kinywani. Kiwango na namna mate yalivyo pia huweza kuathiri uozaji wa meno. Kwa mfano matundu na nyufa huwa haziko sana katika meno ya mbele ambako kuna mate mengi ikilinganishwa na meno ya nyuma. Bakteria wote walioko kinywani wanaweza kubadilisha wanga kuwa tindikali lakini aina ya streptococci na Lactobacili wana uwezo mkubwa wa kutengeneza tindikali. Kuwepo kinywani vijidudu vya aina hii huongeza uwezekano wa meno kuoza. Baadhi ya watu wana kiasi kikubwa cha bakteria wanaosababisha meno kuoza kuliko watu wengine na hii ni kutokana na kuzembea katika kutunza na kuimarishwa usafi wa kinywa.
Wataalamu wanatwambia kuwa, usafi wa kinywa na matumizi ya dawa za meno zenye fluoride hupunguza kasi ya meno kuoza. Usafi wa meno ni pamoja na kupiga mswaki kila siku kwa kutumia dawa za meno zenye flouride, kutumia uzi wa meno kusafisha eneo lililo kati ya meno, kuchokonea meno kwa kijiti ili kundoa mabaki ya chakula na kufanyiwa uchunguzi wa meno mara kwa mara. Flouride huzuia kupungua madini katika molekuli za meno, kuongeza madini hayo kwenye meno na kuimarisha meno ili yasiathiriwe na tindikali. Matumizi ya fluoride kwa kiwango kinachotakiwa huzuia na kudhibiti matundu kwenye meno. Flouride inaweza kupatikana kutoka katika maji ya kunywa na baadhi ya vinywaji vilivyoongezwa mada hiyo. Pia mada hiyo hutiwa katika dawa za mswaki, geli na dawa za kusafishia kinywa. Katika baadhi ya nchi mada ya fluoride huongezwa hata katika chumvi na maziwa. Kiwango cha flouride katika maji ya kunywa na vyakula kinapaswa kuzingatiwa kwa mujibu wa mahitaji ya mwili. Suala hili ni muhimu kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 6 ambao meno yao bado yanakua. Kutumiwa sana au kwa kiwango kikubwa mada hiyo husababisha matatizo katika enamel au mfupa wa jino hali inayojulikana kinaalamu kama kama fluorosis.
Vyakula na athari yake katika kuoza meno
Ijapokuwa katika nchi nyingi kuoza meno kumekuwa kukiambatanishwa na matumizi ya fluoride na utunzaji wa kinywa, aina ya vyakula anavyokula mtu pia ni jambo muhimu linalochangia meno kuoza. Jinsi chakula chenyewe kilivyo kwa mfano kama kinanata na kung'ang'ania kwenye meno pia husababisha meno kuoza. Vyakula vinavyong'ang'ania kwenye meno kama vile bisikuti na crips huongeza uwezekano wa kuoza meno kwani hubakia juu ya meno kwa muda mrefu zaidi kuliko vyakula vingine. Pia vyakula vyenye sukari zinazoyeyuka kwa haraka husafishwa kwa wepesi kinywani na mate, na kila vyakula vyenye wanga vinavyokaa muda mrefu kinywani na kuzunguka meno, ndivyo bakteria wanavyopata fursa zaidi ya kutengeneza tindikali na kuondoa madini katika meno. Kila tunapokula vyakula vyenye wanga, bakteria walioko kwenye kinywa huanza kutengeneza asidi suala linalopelekea meno kuoza. Mwenendo huu huendelea hadi baada ya dakika 10 hadi 20 baada ya kula au kunywa. Katika kipindi tusichokula au kunywa mate huzimua tindikali na kusaidia kurejesha madini katika meno. Iwapo vyakula au vinywaji vitaliwa mara kwa mara na kinywa kisipate muda wa kurejesha madini kwenye meno, hapo ndipo meno huanza kuoza. Kwa ajili hiyo tunashauriwa kutokula na kunywa wakati wote na pia kupunguza kula vyakula vyenye wanga na sukari kwa uchache tusile vyakula hivyo zaidi ya mara 6 kwa siku. Pia tunashauriwa kuhakikisha kuwa tunapiga mswaki meno kwa kutumia dawa za meno zenye fluoride, kwa uchache mara mbili kwa siku.
Mmomonyoko wa meno
Mmomonyoko wa meno ni kuharibika tishu ngumu ya juu ya meno kutokana na acidi bila kuathiriwa na bakteria wanaosababisha meno kuoza. Kuna vyakula na vinywaji vingi vyenye tindikali katika lishe zetu na kuna uwezekano suala hilo likatuathiri. Kwa mfano kupendelea sana kula vyakula au kunywa vinywaji vyenye tindikali husababisha mmomonyoko wa meno. Tatizo hilo lisiposhughulikiwa huweza kuathiri ufanisi wa kinywa na hutofautiana baina ya watu. Ili kuepukana na tatizo hilo tunashauriwa kujiepusha kupenda sana kunywa vinywaji au kula vyakula vyenye acidi na kupiga mswaki kwa uchache mara mbili kwa siku kwa kutumia dawa ya mswaki yenye fluoride. Pia tunashauriwa kutopiga mswaki mara tu baada ya kunywa au kula chakula chenye acidi kwani kufanya hivyo huweza kuyafanya meno yaharibike kutokana na kusugua meno wakati tindikali ikiwemo kinywani. Pia ni bora tujizoeshe kutafuna chingamu au ubani mara tu baada ya kula vyakula vyenye acidi ili kufanya mate yatengenezwe ambayo husaidia kuondoa acidi mdomoni.
 
Top