Nimekua nikipata malalamiko mengi kwa akina mama wanaojifungua kwamba matiti yao yanatoa maziwa kidogo au hayatoi kabisa. hii imewafanya kushindwa kunyonyesha au kuingia gharama kubwa kuwanunulia maziwa ya lactogen fomula dukani au kutumia maziwa ya ngombe.

lakini pia tukumbuke kwamba maziwa ya mama hua hayana mbadala kabisa yaani virutubisho vinavyopatikana kwenye maziwa yale havipatikani popote hivyo kama una shida ya kutoa maziwa basi tumia maziwa mbadala huku ukitafuta suluhisho la maziwa yako.vifuatavyo ni vyanzo vya vya kushindwa kutoa maziwa.

Matumizi ya dawa za uzazi wa mpango; wanawake wengi hutumia njia hizi baada ya kujifungua bila shida yeyote lakini kuna baadhi yao njia hizi huingilia mfumo wao wa  kutoa maziwa hasa zikitumika kabla mtoto hajafikisha miezi sita. hii husababishwa na kuongezeka kwa homoni za uzazi yaani progesterone na oestrogen ambazo hushusha homoni ya kutoa maziwa yaani prolactin hormone.kama umekumbwa na hali hii basi acha mara moja njia hiyo na utumie njia zingine kama kondom,kalenda au njia nyingine isiyotumia dawa.

Matatizo ya kimaumbile; baadhi ya wanawake matiti yao hayakukamilika wakati wamakua yaani yanakua na upungufu wa vitu muhimu vinavyohifadhi maziwa kwenye matiti kitaalamu kama grandular tissues hii hufanya maziwa yatoke kwa shida sana.mama anashauriwa akamue maziwa wakati wa kunyonyesha na mara nyingi mtoto wa pili mpaka watatu wakizaliwa matiti haya yanakua yameshazoea hivyo hayasumbui tena kutoa maziwa.

Upasuaji wa matiti; kama mama ameshawahi kupasuliwa matiti yake kwa shida yeyote labda majipu, ajari, upasuaji wa kuongeza au kupunguza matiti basi kwa namna moja au nyingine hii inaweza kuharibu mfumo wake wa matiti kupitisha maziwa na kujikuta hatoi maziwa ya kutosha.ukiwa na shida hii utahitaji kutumia maziwa mbadala kwa mtoto.

Matumizi ya dawa; wakati wa kunyonyesha mama anaweza kuugua na  kutumia dawa fulani fulani ili apone ugonjwa alionao lakini kuna  baadhi ya dawa ni hatari kwani hushusha kiwango cha maziwa. mfano dawa za kama bromocriptine,methergine,pseudoephredine.

Matatizo ya homoni za uzazi; matatizo ya homoni kua juu sana au kua chini sana yanaweza kusababishwa na magonjwa ya ovari, kisukari na kadhalika. pia magonjwa yeyote ya homoni yanayochelewesha mtu kupata mimba huweza kuzuia maziwa pia. ni vizuri ukaonana na daktari kupima kiwango cha homoni na kupata matibabu.

Kutonyonyesha usiku; wakati wa usiku homoni inayohusika na kutengeneza maziwa yaani prolactin hutengenezwa kwa kiwango cha juu sana lakini pia ili mtoto alale usiku mzima bila kusumbua lazima anyonye vizuri usiku.kutonyonyesha usiku hupunguza homoni hii na kumfanya mama atoe maziwa kidogo sana siku inayofuata.

Kutonyonyesha vya kutosha; kawaida mama anatakiwa anyonyeshe angalau mara kumi ndani ya masaa 24, sasa mwili hutengeneza maziwa unapohisi matiti hayana kitu na kama mwili ukihisi matiti yana maziwa muda mwingi basi unajua maziwa hayahitajiki sana na kuanza kupunguza kiasi cha kutoa maziwa.

Kutokula vizuri; maziwa anayotoa mama yanatengenezwa na chakula anachokula wala sio miujiza fulani hivyo kipindi hiki mama anatakiwa ale mlo kamili yaani matunda, protini ya kutosha, wanga, mboga za majan na maji mengi i na ikiwezekana atumie virutubisho vinavyotengenezwa maalumu kwa ajili ya kuongeza maziwa.

Matumizi ya vyakula mbadala;  miezi sita baada ya kuzaliwa mtoto anatakiwa anyonye tu bila kupewa kitu chochote, kuna watu hua wanawapa maji wakidai eti watoto walisikia kiu sio kweli.sasa kuanza kumchanganyia maziwa ya ngombe na yale ya dukani kutamfanya anyonye kidogo kwako na mwili utapunguza kiasi cha maziwa yako...hivyo siku ukikosa mbadala utajikuta huna maziwa kabisa.

Mtoto kushindwa kunyonya; kama nilivyosema hapo mwanzo kwamba maziwa yakitoka mengi na mwili unatengeneza mengi zaidi na kama mtoto hanyonyi vizuri basi na maziwa hutoka kidogo zaidi.hali hii inaweza kusababishwa na dawa ya usingizi ambayo alipewa mama wakati wa kupasuliwa ambayo huamuathiri mtoto pia, au matatizo ya kuzaliwa nayo kama tongue tie[ulimi kushikwa chini ya mdomo, hii inaweza kurekebishwa na daktari] au mtoto kuugua.
 
Top