Hakuna ubishi kuwa mama anapokuwa katika hali hii hupenda kuishi maisha yasiyo na bughudha ama rabsha. Pamoja na kuwa watu wengi hukubaliana na changamoto zinazowapata wanawake katika kipindi hiki, kumekuwapo na makosa kadhaa wanayofanya wakati mwingine bila kujua athari zake.
Makosa haya husababisha wanawake hawa kujisikia vibaya au wakati mwingine kujenga chuki kwa mtu husika. Najua hata wewe inawezekana umekuwa ukifanya makosa haya bila kujua kama ni kero kwa mjamzito husika. Hivyo kama jibu ni ndiyo, si vibaya ukasoma hapa chini kuona je ni mambo gani hutakiwi kumwambia mwanamke anapokuwa kwenye hali hii ya ujauzito.
Wataalamu kutoka mtandao wa parenting.com wameainisha baadhi ya mambo hayo kuwa ni:
1. Hivi ulijipanga kupata mimba au imekuja tu?
Unategemea kupata jibu gani kutokana na swali hili. Mara nyingi unapomuuliza mwanamke mwenye hali hii humaanisha vitu vingi. Hivyo kwa mujibu wa wataalamu unachotakiwa kumwambia ni ‘hongera’.
2. Hivi una hakika huna mapacha kweli?
Eeeh akiwa na mapacha we unataka nini? Au we nani hadi uulize swali kama hilo. Kwa kulitazama tu unadhani swali hilo linafurahisha?
Hata kama unamuona ana tumbo kubwa pengine isivyo kawaida hutakikiwi kumwambia kitu kama hicho, hasa ikizingatiwa kila mtu huwa na mapokeo yake.
3. Utakuwa umebeba mtoto wa...
Hili ni kosa jingine linalofanywa na watu wengi, bila kujua kama linamkera mwanamke mjamzito. Inawezekana mtoto unayemtabiria siyo aliyekuwa kichwani kwake. Au wakati mwingine anaweza akaona kama unamfanyia uchuro. Kama unahisi huna jambo la kuongea naye, siyo vibaya ukampa nafasi ya kupumzika.
4. Hivi huyo mtoto anacheza kweli?
Swali kama hili linaweza kusababisha ugomvi mkubwa baina ya muulizaji na muuliza hasa inapotokea, mama mjamzito akawa na mimba kubwa.
Kwani wengi huhisi kuwa, mtoto wake aliyetumboni atakuwa anatabiriwa kifo, jambo ambalo siyo zuri kulisikia hata masikioni.
Unataka kujua kama anacheza ama hachezi kwani we ni daktari? Wakati mwingine ni vyema kupima maneno yako kabla hayajatoka nje ya kinywa chako.
5. Naweza kulishika tumbo lako?
Watu wengi hupenda kufanya mambo kwa kuiga. Inawezekana umeona kwenye video watu wakifanya hivi. Lakini unafahamu kuwa katika tamaduni nyingi mambo ya kushika tumbo la mjamzito hukatazwa.
Kwani wakati mwingine kwa kulishika tu, inaaminika unaweza kusababisha madhara katika afya yake. Hivyo inatosha kumsalimia na kumjulia hali. Kama yeye hajambo basi ni wazi kuwa hata mtoto wake atakuwa anaendelea vizuri.
6. Hivi na wewe utaweza kunyonyesha kweli?
Swali kama hili linavunja moyo. Unapobeba mimba, kimsingi unakuwa umejipanga. Kwani ni wazi kuwa unaelewa fika kila hatua utakayopitia. Hata kama siyo kwa kuipitia basi hata kwa kuisikia kutoka kwa watu wengine.
Hivyo siyo sawa kumuuliza swali kama hili, kwani mwingine anaweza kukuuliza umenionaje hasa? Na unaweza ukawa umemkera bila ya wewe kufahamu.
7. Kwa hiyo unatarajia wa kike au wa kiume
Hii ni tabia ya watu wengi kutaka kujua maoni binafsi ya mtu mwenye ujauzito. Licha ya ukweli kuwa kwa mama mtoto ni mtoto, huna haja ya kutaka kujua maoni yake kwani kwa kawaida ni Mungu pekee ndiye mwenye hiyo.
Kwa kutaka kujua maoni yake, unaweza kuwa umemkera. Hivyo ili hilo lisitokee ni bora ukaa kimya kama huna cha kuongea naye.
Si vibaya tukiwaacha wapendwa wetu hawa wabebe mimba kwa raha zao, kwani maswali mengine hukatisha tamaa.