WAJAWAZITO wengi wamekuwa wakipata matatizo ya kupungukiwa na damu mara kwa mara kitu ambacho ni hatari kwao hasa kama wanakaribia kujifungua.
Ili kuondokana na tatizo hilo la upungufu wa damu safu hii wiki hii inatoa ushauri kwao. Wajawazito wanashauriwa kula vyakula vyenye madini ya chuma kwa wingi kama vile nyama, maini, mayai, samaki, mimea jamii ya kunde, maharage makavu, mboga za majani, matembele, na mikate iliyoongezwa madini ya chuma ili waweze kuongeza damu mwilini.
Chuma ni madini muhimu pia. Kwa hakika, mwanamke huhitaji madini mengi zaidi ya chuma anapokuwa mjamzito. Asipokuwa na kiasi cha kutosha, hali ambayo huwapata wanawake wengi katika nchi zinazoendelea, damu yake inaweza kuwa na upungufu wa madini hayo. Hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi mwanamke apatapo mimba moja baada ya nyingine, kwa kuwa hana nafasi ya kurudisha kiasi kinachohitajika cha madini ya chuma.
Kuna baadhi ya vyakula kama vile chai ya rangi ambavyo vikinywewa wakati mjamzito amekunywa vidonge vya madini ya chuma vinaweza kupunguza unyonywaji wake katika utumbo.
Kwa upande mwingine baadhi ya vyakula vyenye vitamini C kama vile matunda ya jamii ya machungwa huongeza uwezo wa utumbo kunyonya madini ya chuma mwilini, hivyo wajawazito wale matunda hayo mara kwa mara.
Mjamzito akigundulika kuwa ana upungufu mkubwa wa damu hasa kama anakaribia kujifungua hasa katika wiki za mwisho baada ya wiki ya 32 za ujauzito, anatakiwa atibiwe hospitali.
Dalili za kupungukiwa na damu kwa mjamzito zipo nyingi kama vile mboni ya macho kuwa nyeupe, ngozi ya kiganja au kucha kuwa nyeupe, kizunguzungu nk. Ni vema kupimwa kliniki kila unapohitajika.
Wengine wanaweza pia kuwa na dalili za matatizo ya moyo, hivyo wanapaswa kulazwa na kupumzika kitandani na wakati fulani kuongezewa hewa ya oksijeni hali ikiwa mbaya.
 Pamoja na kutibiwa matatizo ya moyo, huongezewa pia damu (packed red cells) kwa vile vidonge vya madini ya chuma havitafaa kurekebisha tatizo hili kwa haraka kabla ya muda wa kujifungua kufika.
Matibabu
Magonjwa kama malaria na minyoo imethibitika kuwa huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa upungufu wa damu kwa wajawazito, hivyo basi magonjwa haya hayana budi kutibiwa haraka sana ili yasilete madhara kwa mjamzito.
Wajawazito wanaoishi maeneo yenye mbu wenye malaria kwa wingi hapa nchini hupewa dawa za kinga ya SP ili kuwalinda wasipatwe na ugonjwa huu. Pia dawa za minyoo za Albendazole au Mebendazole hutolewa kwa wajawazito baada ya miezi mitatu ya mwanzo ili kuua minyoo.
Baada ya kutumia dawa hizo za minyoo, wajawazito (lakini hata watu ambao siyo wajawazito) wanashauriwa kuvaa viatu/kandambili kila wakati na kuepuka kukanyaga kinyesi chochote.
 
Top