Mchoro wa moyo unaoonyesha madhara ya ghafla yanayoweza kusababisha kifo
Ni jambo la kushtua inapotokea habari kuwa mtu wa karibu, ndugu, rafiki au mtu maarufu ambaye ulishiriki naye jambo fulani muda mfupi uliopita, amekufa ghafla.
Taarifa za kifo chake ambacho kimetokea ghafla kabla ya kupita saa 24 tangu mlipoachana naye, hushangaa.
Kifo hiki cha ghafla ni cha kiasili na cha kawaida kinachoweza kumpata mtu yoyote pasipo kuwapo na ugonjwa unaojulikana au kuwa na dalili za muda mrefu.
Kitaalamu inaelezwa kuwa kifo cha namna hii hutokea baada ya mgonjwa kudondoka au kupoteza fahamu saa moja baada ya kujitokeza dalili wakati akiwa usingizini.
Mara nyingi, vifo vya ghafla huambatana na matatizo au magonjwa ya moyo na tatizo hili huwapata zaidi watu walio na umri wa miaka 30 au zaidi.
Yapo matatizo mengine ya kiafya yasiyohusiana na moyo lakini yanayoweza kusababisha kifo cha aina hii.
Kila mwaka duniani kote watu wengi hufariki ghafla hasa katika nchi ambazo zimepiga hatua kiuchumi kutokana na maradhi ya moyo.
Wataalamu wa afya hufanya uchunguzi wa kina kila inapobidi ili kubaini sababu za kifo cha aina hiyo. Baadaye taarifa hizo husaidia katika utafiti kujua mambo gani katika jamii ambayo ni hatarishi au nini kilidhurika kwenye mwili wa mtu aliyekufa ghafla. Ni vyema ifahamike kuwa kuna tofauti kati ya kifo cha ghafla na mshtuko wa moyo.
Mshtuko wa moyo ni pale misuli ya moyo inaposhindwa kufanya kazi na kusimama ghafla na baada ya kupewa huduma ya kwanza kwa kutomasa moyo, huweza kuisha na moyo huendelea kufanya kazi yake.
Sababu za vifo vya ghafla
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk. Meshack Shimwela anasema zipo sababu tofauti zinazosababisha vifo vya ghafla, baadhi ikiwa ni maradhi ya moyo, mapafu, ubongo, mfumo wa upumuaji na wakati mwingine sumu.
Dk. Shimwela alisema moyo inasababisha vifo kwa asilimia kubwa kwa sababu mishipa au milango ya moyo inaweza kupasuka; athari za dawa kwenye moyo; moyo kukosa hewa safi au kiungo kimoja kukosa usambazaji wa damu.
CHANZO:MWANANCHI
 
Top