WIKI iliyopita tuliona jinsi fangasi wanavyoambukiza na kusababisha madhara mbalimbali sehemu za siri.
Leo tunakwenda mbele zaidi kwa kuangazia akina mama wenye ujauzito ambao hupata fangasi hawa kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na kupungua kwa kinga ya mwili.
Hata hivyo, ieleweke kuwa si kila mjamzito hupatwa na maambukizi haya ya fangasi wa Candida albicans.
Matumizi ya dawa za kupanga uzazi  maarufu kama vidonge vya majira huweza kusababisha mtu kukumbwa na maambukizi ya fangasi hawa.
Lakini pia wale wenye upungufu wa kinga mwilini (HIV/AIDS) nao wana hatari ya kupata magonjwa sugu kama kisukari, saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya mononucleosis na nk.Wengine wanaopata maradhi ni wale waliopata matibabu ya homoni (hormonal replacement therapy) kutokana na sababu mbalimbali au matibabu ya kusaidia kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazi. Wenye utapiamlo (malnutrition) nao wanaweza kupata tatizo hili.
Wengine wanaoweza kupata ugonjwa huu ni wale wenye tabia ya kuvaa nguo au mavazi yanayoleta joto sana sehemu za siri kama nguo za kuogelea (swim wear), chupi zilizotengenezwa kwa kitambaa aina ya nailon au zinazobana sana nk.
Lakini wale wanaojamiiana kwa njia ya kawaida kufanya kitendo hicho kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) au matumizi ya vilainishi vyenye glycerin wakati wa kufanya tendo la ndoa wana uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya maradhi haya. UCHUNGUZI NA VIPIMO
Kabla ya vipimo vya uchunguzi, mgonjwa atafanyiwa vipimo vya uchunguzi wa uke  kitaalamu huitwa per Vaginal Examination (PV exam) kuona kama kuna uvimbe wowote ndani ya utupu huo au kama ana maumivu wakati wa kujamiiana.
Daktari ataangalia kama kuna uchafu wowote unaotoka, wingi wake, rangi yake, harufu yake, uzito wake na aina ya uchafu unaotoka kama ni sahihi kutokana na maelezo ya mgonjwa. Kwa kifupi daktari ataangalia mambo mengi kama vile kuna uvimbe wowote wa tezi za sehemu ya siri yaani mitoki, shingo ya kizazi, bartholin glands nk. Ataangalia sehemu ya haja kubwa kama kuna skin tags, bawasiri (haemorrhoids) nk.  Inashauriwa kuwa kabla ya kufanya vipimo, daktari amjulishe mgonjwa aina ya kipimo, lengo lake na jinsi kitakavyofanyika ili kumuandaa kisaikolojia. Daktari anaweza kuchukua kipimo na kuotesha kwenye maabara ili kuangalia aina ya uoto huo kama ni wa fangasi aina ya Candida albicans, ama la, atafanya kipimo cha mkojo (Urinalysis), na cha ugonjwa wa kisukari, HIV/AIDS, ugonjwa wa  kuvimba tezi la koo (goiter) na kadhalika.
 
Top