MAMA MJAMZITO
MAMA MJAMZITO
Hali ya mwanamke kuwa na afya bora wakati wa ujauzito na kujifungua salama, huu ndiyo uzazi salama.
Uzazi salama hutokana na matunzo na lishe bora ya mwanamke wakati wa utoto wake, ukuaji na ujauzito. Pia hutegemea kuzaa kwa mpango, kupata huduma muhimu wakati wa ujauzito na kujifungulia mahali salama.
Kiwango cha uzazi salama duniani kipo chini na wanawake wengi hupoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi. Miongoni mwa sababu zinazopelekea vifo hivi ni pamoja na;
Kazi nyingi na ngumu wakati wa ujauzito, kuoza wasichana katika umri Mdogo, ukosefu wa elimu ya maisha ya jamii wakati wa ujana, kutoa mimba, kuzaa katika umri mkubwa zaidi ya miaka 35, huduma muhimu za jamii kuwa mbali au duni pamoja na lishe duni wakati wa utoto, ujauzito na wakati wa kunyonyesha.
Mpenzi msomaji, ni vyema kuvifahamu viashiria vya hatari wakati wa ujauzito, viashiria hivyo ni pamoja na; kutoongezeka uzito kwa wakati wote wa ujauzito (mama anatakiwa aongezeke angalau kilo sita wakati wa ujauzito). Kutoongezeka uzito ni dalili mbaya kwa mama na mtoto.
Kuvimba miguu, mikono na uso. Hii kwa mjamzito ni dalili ya kifafa cha mimba au upungufu wa damu mkali.
Viashiria vingine vya hatari ni homa Kali na kutapika, kutoka damu ukeni wakati wa ujauzito, kifafa cha mimba, upungufu wa damu, kujaa maji kwenye mji wa mimba pamoja na kuumwa sana kichwa (dalili ya shinikizo la damu).
Pindi mama mjamzito anapoona viashiria hivyo, ni vyema zaidi akaonana na wataalamu wa afya ya uzazi na mtoto ili waweze kumpatia huduma stahiki na hivyo kuepukana na vifo au matatizo yanayotatulika.
Vifo vya wajawazito na watoto wachanga vinaweza kupunguzwa, kila mtu afanye au atimize wajibu wake.
 
Top