Hali ya mwili au sehemu ya viungo katika mwili kujaa maji na kuwa na muonekano kama vile uvimbe kitaalamu hujulikana kama Edema.
Vipo
vitu au sababu mbalimbali zinazopelekea mwili au sehemu ya viungo katika
mwili zijae maji. Sababu hizo ni pamoja na, magonjwa ya moyo (
congestive heart failure ) ambapo kutokana na moyo kushindwa kufanya
kazi zake vizuri, husababisha damu ishindwe kufika katika viungo vingine
vya mwili mfano miguuni. Hii itasababisha mwili ukusanye au uhifadhi
maji mengi zaidi ya mahitaji halisi na matokeo yake husababisha mwili
uwe kama umevimba.
Matatizo
ya Aleji ( Allergic Reactions ). Inawezekana mwili umepatwa na chembe
chembe ambazo haziendani na muundo mzima wa mwili, mfano wa chembe
chembe hizi ni vyakula, mafuta ya kujipakaa au hata sumu baada ya
kung’atwa na mdudu. Hivi vyote huweza kukusababishia mwili ujae maji
haya ambayo huwa na muonekano wa uvimbe katika sehemu husika ya mwili.
Magonjwa
ya ini ( liver cirrhosis ), ambayo hupunguza utendaji kazi wa ini ikiwa
ni pamoja na utengenezaji wa vitu muhimu vinavyopatikana katika damu
mfano protin (albumin).
Upungufu wa protini mwilini unaoweza kusababishwa na matatizo ya kuwa na lishe duni au magonjwa ya ini.
Magonjwa
ya figo. magonjwa ya figo hupunguza utengenezaji wa damu mwilini
kutokana na kuathiriwa kwa vitu muhimu katika figo vinavyohusika na damu
( erythropoietin ).
Inawezekana
mtu mwili wake ukajaa maji kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya
mwili, mfano ni wamama wajawazito ambao baadhi yao huwa wanavimba miguu
kutokana na miili yao kuwa na ongezeko la mahitaji ya damu ili kuweza
kuutoshereza mzunguko mzima hadi kufika kwa kiumbe/viumbe walioko
tumboni.
Mpenzi
msomaji, baada ya kufahamishana miongoni mwa mambo yanayoweza kupelekea
mtu apate hali hii ya mwili kujaa maji pia ni vyema kujua namna ambavyo
maji haya hujitokeza na kusababisha muonekano wa uvimbe.kwa mfano, ni
kwa nini unapong’atwa na mdudu ndiyo uvimbe unajitokeza?, nini
kinatokea katika mwili wako hadi ngozi inajaa au kuvimba?. Katika mfano
huo ngozi hujaa maji au kuvimba baada ya uwezo wa mishipa ya damu
kuruhusu maji kupita ( permiability ) kubadilika ambapo mishipa hii ya
damu huruhusu maji mengi zaidi yapite au yahame kutoka katika
mchanganyiko wa damu na kuhamia katika tishu au nyama za mwili nje ya
mishipa ya damu. Maji haya kwa kuwa hayapo katika mishipa basi
husababisha sehemu hiyo ya mwili iwe kama imevimba, ila kwa upande wa
pili hali hii huruhusu pia kinga za mwili au seli zinazohusika na ulinzi
wa mwili zifike kwa wingi zaidi katika sehemu hiyo (mfano ulipong’atwa)
na kuweza kupambana ili kuziwezesha seli hizo zirejee katika utendaji
kazi wake wa kawaida, kwani maji hayo huwa na kiwango kikubwa cha seli
zinazo ulinda mwili ambazo ni seli hai nyeupe za damu ambazo kitaalamu
huitwa leucocytes.
Mambo
niliyoyaeleza hapo juu ni baadhi tu ya yale yanayoweza kumfanya mtu
mwili wake ukajaa maji na hivyo kuonekana kama umevimba. Endapo mtu
atakuwa na tatizo hilo mara nyingi utatuzi au matibabu yake
yanategemeana na kisababishi cha hali hiyo ni nini, hivyo matibabu
hutofautiana. Endapo unatatizo hili fika katika kituo cha kutolea huduma
za afya kilicho karibu na wewe ili uweze kupata huduma zinazostahili
mapema.