Wanawake wametajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuwashauri pamoja na kuwahimiza waume zao na watoto wa kiume kufanyiwa tohara ikiwa ni njia moja wapo ya njia ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Akizungumza jana katika Kijiji cha
Mwendakulima wakati wa tamasha la kutafuta kikundi bora
kitakachohamasisha siku ya Ukimwi duniani Mratibu wa Ukimwi wa halmashauri ya
mji wa Kahama mkoani Shinyanga Elibariki Minja aliwataka wanawake
kutowaonea aibu waume zao badala yake wawaeleze.
Alisema kama wanawake watakuwa mstari wa mbele
kuwashauri wanaume ambao hawajafanyiwa tohara itasaidia sana kupunguza
maambukizi ya Ukimwi pamoja na kuifanya jamii kuelimika kanda ya
ziwa hususani Mkoa wa Shinyanga ambapo wanaume bado hawajawa na elimu ya
kutosha kufanyiwa tohara.
“Ndugu zangu wanawake naomba muwasihi na
kuwahimiza waume zenu ambao bado hawajapata tohara wapatiwe ili kujikinga na Ukimwi,
pamoja na kuwapeleka watoto wa kiume kufanyiwa tohara”,aliongeza Minja.
Alisema kama wanaume watafanyiwa tohara itasaidia
kuwapunguzia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 60 hivyo wanapaswa
kuwahamasisha wananume ambao bado wanaona aibu ya kufanyiwa tohara.
Alisema hospitali ya wilaya ya Kahama
imetenga kitengo cha kufanyia tohara kila siku hivyo ni
nafasi ya kila mwanamume ambaye bado hajafanyiwa kwenda kufanyiwa zoezi hilo
ambalo linatolewa bure bila malipo.
Kwa upande wake meneja Mahusiano wa Mgodi
wa ACACIA Buzwagi Yunia Wangoya alisema mgodi bado unaendelea
kujikita katika jamii inayowazunguka katika kushiriki kwenye shughuli za
maendeleo pamoja na kujumuika pamoja kwenye shughuli mbalimbali kama
sera yao katika kuimarisha uhusiano na jamii inayowazunguka.