Upungufu wa nguvu za kiume ni mojawapo ya tatizo la kiafya linaloumiza sana kisaikolojia wanaume wengi. Kufahamu ukweli wa jambo hili ni moja ya nyenzo ya kuweza kukabiliana nalo.

Ukosefu wa nguvu za kiume ni moja ya mambo, ambayo yanazungumzwa sana mtaani kila kukicha. Ni tatizo ambalo linasababisha mifarakano katika mahusiano.

Waathirika wa tatizo hili hukumbana na kunyanyapaliwa na baadhi ya wanajamii, ambao hudiriki hata kuwanyooshea kidole na kuwakejeli wakidhani kuwa wamejitakia kumbe ni tatizo la kiafya linaloweza kumpata mtu yoyote yule.

Tumewahi hata kusikia wengine wakipoteza maisha huku chanzo kikiwa ni kutumia dawa za kuongeza nguvu, yote ni katika harakati za kujipigania kuepukana na tatizo hilo.

Waathirika hawa wamekuwa wakipoteza fedha nyingi na mara nyingine hujikuta wakiingia katika matatizo makubwa ya kiuchumi baada ya kukutana na vipeperushi au matangazo ya dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Wengi hujikuta wakitapeliwa na waganga feki, ambao wamejaa mijini na vijijini. Katika mitaa utaona mabango mengi ya waganga wa kienyeji wasio na sifa wala usajili wakijitangaza kuwa na dawa za kuongeza nguvu za kiume

Katika magazeti hasa yale ya udaku, utakutana na matangazo madogo yakitangaza dawa mbalimbali ya kienyeji za kuwaongeza nguvu za kiume.

Baadhi ya dawa hayo hazijulikani wapi zilithibitika ni salama, na huuzwa kwa vificho na hakuna uwazi katika matibabu yao.

Lakini kukurupuka na kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kiholela ni hatari sana, kwani baadhi ya dawa hizo ndiyo chanzo cha kuumiza mwili na kuathiri viungo kama figo. Leo kwa kuanzia, nitaeleza namna mfumo wa sehemu za uzazi ulivyo na namna uume unavyoweza kuwa na nguvu ya kusimama na kusisimika. Baadaye nitafikia hatua kuelezea chanzo hasa cha kukosa nguvu za kiume.

Tendo la uume kuwa na nguvu na kuweza kusimama ni kitendo, ambacho kina mtiririko wa matukio mengi ya kimwili na huwa ni hatua moja kwenda nyingine. Kitendo cha kusimama kinahusisha mfumo wa fahamu kama vile ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, mfumo wa damu ambao ni moyo, damu na mishipa) na mfumo wa tezi zinazomwaga vichocheo kama vile homoni.

Zipo kemikali nyingi za kibaiolojia za mwilini zikiwamo protini, virutubisho na vitamini mbalimbali tunavyopata katika lishe, husaidia pia katika tendo hili.

Kwa kawaida sehemu za uzazi wa kiume huwa na misuli laini kama sponji, ambayo huwa na mishipa midogo mingi ambayo imejikunja kunja kama mizizi ya mmea. Wakati wa kusimama damu iliyosafi humiminika kupitia mishipa ya ateri, ambayo hutanuka kuruhusu damu ya kutosha kupita kwenda katika misuli laini kama sponji ambayo huwa imetulia tuli kuruhusu damu kuingia katika mishipa hiyo.

Wakati huohuo, ile mishipa inayotoa damu chafu kurudi kusafishwa yaani veini huwa zimebanwa ili damu hiyo isitoke katika misuli laini ya uume.

Kuingia huku kwa damu na kujaa na damu ya veni, kuzuiwa kutoka ndiyo inayofanya uume kuongeza urefu na ukubwa, yaani kuweza kusimama.

Kuna matukio ya kimwili yasiyo ya hiari yaliyomo ndani ya mfumo wa fahamu, ambayo inakinzana, mmoja hufanya kazi ya kuchochea hisia za mwili na nyingine hutuliza hisia za mwili.

Lakini kusimama huku hakutokei tu bali kunahitajika kusisimuliwa vichocheo hisia, ikiwamo kusikia, kuona, kuhisi harufu na utambuzi wa hisia za tendo.

Mchemko wa kupata hisia za kujamiiana katika kituo kilichopo ndani ya uti wa mgongo ni matokeo ya eneo la uzazi sehemu ya kiume kusisimuliwa.
 
Top